Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kupata muda angalau wa kuchangia nami niseme mambo machache ambayo nadhani yanaweza kutusaidia hasa tunapozungumza juu ya habari ya miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kwamba Wizara hii haihusiki sana na TARURA, lakini fedha zinazotoka katika Mfuko wa Barabara ni sehemu ya fedha zinazokwenda kuimarisha TARURA ili iweze kutengeneza miradi mingi zaidi kadri inavyowezekana. Imani yangu ni kwamba fedha hizi ni pamoja na kuhakikisha kwamba tunajenga miradi mingi ya barabara ambayo inapunguza msongamano kwenye miji mikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko barabara mbili muhimu sana kwenye Jimbo la Nyamagana, barabara ya kutoka Buhongwa kwenda Igoma na barabara ya kutoka Mkuyuni kupita Nyangerengere kwenda kutokea Mahina na Nyakato Buzuruga. Barabara hizi zikijengwa naamini kwamba TANROAD wangeweza sana kufanya kazi hii na TARURA sio eneo lake sana kwa sababu ukifikiria Nyamagana tunao mtandao wa barabara kilomita 738, lakini ni kilomita 47 peke yake ndio zimejengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama hatutazingatia msingi huu wa kuona maeneo muhimu tukaimarisha ujenzi wa barabara hizi, hatuwezi kusaidia chochote na badala yake tutakuwa tunaipa TARURA mzigo ambao haiwezi kuumudu kwa miaka yote inayokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii sambamba na kwenye Jimbo la Ilemela ipo barabara ya kutoka Nyakato- Buseri - Monze yenye jumla ya kilometa 18. Leo tunakwenda mwaka wa tatu kilometa hizi toka zitengewe fedha imeshajengwa kilometa moja na point peke yake, sioni kama tuna dhamira njema ya kusaidia miji hii mikubwa ili iweze kupunguza msongamano na kuifanya ipumue kwa haraka zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo napenda kuzungumza ni juu ya uwanja wa ndege. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, toka tumeanza kuzungumza habari ya uwanja wa ndege wa Mwanza leo ni takribani miaka sita. Hivi malengo na mipango yetu ni ipi? Mimi nafahamu Serikali yenye dhamira ya kukusanya kodi nyingi kama Serikali ya Awamu ya Tano ina kila sababu ya kuimarisha maeneo ambayo ilikwishaanza. Ukiimarisha uwanja wa ndege wa Mwanza kabla hujakimbilia maeneo mengine mengi kwenda kushika huku na kule utakuwa umesaidia zaidi kuhakikisha eneo hili linaimarika kwa nguvu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tuko asilimia 65 tunasema ya ujenzi wa jengo la abiria, ya ujenzi wa jengo la kuongezea ndege, uwanja wa kukimbilia kwa maana uwanja wa kurukia kwa maana ya runway, lakini tunajenga jengo kwa ajili ya mizigo. Hapa tunachokifanya ni sawa na kuvaa suti halafu unavaa kandambili; bila kujenga jengo la abiria hakuna tunachokifanya. Ni agizo la Mheshimiwa Rais viwanja vyote vinavyozunguka maeneo ya ziwa vijengewe cold room kubwa ambazo zitasaidia sana viwanja hivi kuwa kwenye maeneo ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko hata suala la ndege, unapozungumza kuimarisha Kiwanja cha Ndege cha Mwanza ndivyo unavyozungumza kuimarisha utalii wa ndani. Hata ndege hizi zinazozungumzwa hapa sana leo kwa hii robo peke yake nilikuwa najaribu kuona zaidi ya abiria 21,000 wamesafiri na ndege hizi ikiwemo Mwanza yenyewe kwa kiwanja chetu hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tafsiri yetu ni nini kukuza na kuendelea kuboresha uwanja wa ndege wa Mwanza itasaidia sana hata pato kubwa zaidi kuongezeka kwenye Serikali. Hata hivyo, Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii atakuwa ni shahidi, kwa hii tu robo peke yake abiria hawa waliokuja Mwanza, wameenda Kigoma, wameenda Zanzibar, wameenda Bukoba, wameenda Comoro, wameenda Arusha, ni idadi kubwa sana ambayo inaingizia pato Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mpango wa Serikali ni nini? Niwaombe sana tuboreshe Kiwanja cha Ndege cha Mwanza, kazi tuliyoifanya sasa Mheshimiwa Waziri itabaki kuwa haina maana kama hatutajenga jengo la abiria. Kinachozungumzwa hapa ni mkataba wa mkandarasi kuelekea mwisho, lakini ni bilioni 61 peke yake zimebaki, hebu tutoe hizi fedha tujenge jengo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini tukifanya hivyo tutafanya kazi kubwa, naomba nishukuru na tuone matokeo ya kazi ya Serikali ya Awamu ya Tano. Nashukuru sana.