Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tabora Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nichangie hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi. Awali ya yote nianze kumpongeza Rais wangu kwa kazi nzuri anayofanya, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Profesa Mbarawa, Mheshimiwa Engineer Nditiye, Mheshimiwa Kwandikwa na wataalam wote kwa kazi nzuri wanayofanya kwa sababu, mwenye macho haambiwi tazama. Mheshimiwa Profesa kazi ameiweza pamoja na timu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia, kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote wa Wizara zote kwa sababu, sitapata nafasi ya kuwashukuru kwa kazi nzuri wanayofanya na Manaibu wao. Kazi wanayofanya kwa nchi hii wanaitendea haki Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia hoja hii ambayo iko mbele yetu kwa kusema haya yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote niiombe Wizara ichukue ushauri wa barabara wanazotoa Wabunge kwa sababu, Wabunge ndio wanaotembea kwenye maeneo hayo na ndio wanaoyafanyia kazi. kwa hiyo, la kwangu naomba nichangie kuhusu barabara inayotoka Puge
– Ndala – Simbo – Nkinga – Ndembezi – Ziba – Manonga na Shinyanga, sijaona kama imewekewa fedha yoyote kwa ajili ya usanifu, lakini naomba nijenge hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii kuna hospitali kubwa mbili. Kuna Hospitali ya Ndala Mission, kuna Hospitali ya Nkinga, lakini azma yetu ni kufungua barabara ya Mkoa na Mkoa, barabara hii inaenda mpaka Shinyanga. Kwa hiyo, ikipatikana nafasi, kwa mwaka huu najua haitawezekana kwa sababu, haimo kwenye vitabu, lakini niombe tu kwamba, kama kutakuwa na uwezekano 2018/2019, namwomba Mheshimiwa Waziri iingie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine nishukuru kwa ajili ya kuweka upembuzi yakinifu barabara ya Tabora – Mambali – Bukene – Itobo na Kahama. Hii barabara nayo ni kubwa sana, kwa hiyo, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwamba, ameitengea fedha. Hata hivyo, barabara ya kutoka Tabora – Mambali – Bukumbi – Shitage – Kahama, hii haijaonekana, nimwombe Mheshimiwa Waziri hii barabara nayo aiangalie kwa jicho la huruma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu sana kuongea na Mheshimiwa Kwandikwa, lakini majibu aliyokuwa ananipa naona kama Wizara yake haiitambui barabara hii. Kwa hiyo, niombe nayo pia iangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ni barabara ya Sikonge – Ipole – Mpembampazi – Kitunda – Rungwa. Hii barabara ni muhimu sana. Barabara hii akiifungua ikatoka Sikonge, ikapita Ipole, ikaenda Rungwa maana yake inaenda kukutana na barabara ya Itigi inayokwenda Singida. Kwa utaalam huo pia, barabara hii akiifungua kwa kupitia Sikonge maana yake itaunganisha wageni kutoka Afrika Kusini, itaunganisha usafiri kutoka Malawi ambao wote wanaotaka kwenda Mwanza na kwenda Uganda, hii njia ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ambayo naomba niichangie ni ujenzi wa Ipole – Koga. Njia hii inasuasua, ina mkandarasi na mpaka sasa hakuna mawasiliano ya aina yoyote, imekatika kwa ajili ya mvua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna Barabara nyingine ya Kaliua – Uvinza – Kigoma, sasa hivi hamna kitu kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri anapoiacha hii ya Kaliua maana yake anatenganisha Kigoma na Tabora ambayo ndio njia rahisi ambayo inaweza kuunganisha Watanzania wote kwa kwenda Dar-es-Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo pia, Mheshimiwa Waziri bajeti ya mwaka huu kwa TANROADS pamoja na TARURA imevurugika. Mwaka huu mvua imenyesha sana, sijui Serikali imejipangaje kwa sababu, fedha iliyomo kwenye vitabu haitoshi na haitatosha. Kwa hiyo, niiombe Serikali itenge fedha ya dharura kwa ajili ya matengenezo ya barabara kwa sababu, mvua hii hatukuitegemea kunyesha kiasi hicho, lakini imenyesha Tanzania nzima na Tanzania nzima kuna mafuriko ya kila aina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe waiangalie TARURA na TANROADS kwa sababu, TARURA pia ingawaje iko chini ya TAMISEMI, lakini haina fedha na kama haina fedha ina maana kwamba, hata TANROADS haina fedha. Kwa hiyo, niiombe Serikali iangalie kwa jicho la huruma kwa sababu, tutakuwa tunawalaumu kumbe fedha hazipo kwa hiyo, wapewe fedha ya uhakika, ili waweze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna uharibifu mkubwa wa barabara, kuna mashimo makubwa ambayo hayazibiki kwenye barabara kuu. Haya nayo ni matatizo kwa sababu, hata juzi juzi ajali iliyotokea Singida ni madereva walikuwa wanakwepa mashimo. Kwa hiyo, niiombe Serikali iangalie jinsi gani ya kuziba mashimo ambayo ni marefu mno. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka kuzungumzia kidogo kuhusu ununuzi wa ndege. Ununuzi wa ndege ni jambo zuri, naipongeza sana Serikali yangu na ikiwezekana iongeze tena na tena ili Watanzania tuwe kwenye neema tusiwe tunaziona tu ndege nyingine za Emirates zinaleta watalii, basi na za kwetu ziwe na wimbo mmoja, lakini niipongeze Serikali pia kwa standard gauge ambayo nina imani itafungua mambo mengi ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongelee ukarabati wa majengo ya TBA hasa Site II, yako katika hali mbaya. Tunakaa kwa kusema hatuna mahali pa kukaa kwa sababu, sisi ni Wabunge, ni wageni, lakini tuko katika hali mbaya. Lingine uchafu uliokithiri. Kuna majumba yale yaliyowekwa sijui ni majumba, sijui manini ya taka, yamejaa mpaka yanatapika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe ushauri. Mitaani tunachangia usafi wa mazingira, kwa nini TBA wasijipange wakaleta waraka wa kuchangia angalau Sh.10,000/= kwa kuondoa uchafu wa taka mle? Kwa sababu, tukisema kila kitu bure ndio hayo; nimwombe Mheshimiwa Waziri, atume delegation yako ikakague usafi na uchafu uliopo katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe tu kwamba, kama atapata muda mzuri ni vizuri watuandikie waraka wapangaji, tuna uwezo ndio maana tukapanga. Kwa hiyo, lazima kuwe na utaratibu wa kuchangia tusifanye bure au kuogopana bure, itatoka wapi hela? Kwa sababu, usafi ni wa kwetu, kodi tunayolipa ni ndogo kiasi ambacho kuchangia Sh.10,000/= hatutashindwa. Kwa hiyo, niombe tuweke utaratibu, tutafute jinsi ya kukusanya angalau Sh.10,000/= kwa kila nyumba tutoe ule uchafu ambao upo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni miundombinu rafiki na maji. Barabara nyingi zinakatwa wakati wa kuingiza maji, hivi hakuna ramani? Inajengwa barabara ya lami kwa gharama kubwa sana, lakini ndani ya mwezi mmoja au miezi miwili miundombinu ya maji inapita pale inakata barabara, hivi sheria hatuna? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka nichangie hayo tu, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono kwa asilimia mia moja bajeti hii.