Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. James Kinyasi Millya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Simanjiro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukurasa wa 34 wa kitabu hiki utaona kuna barabara ya Arusha – Orkesumet - Kibaya mpaka Kongwa. Wakati upembuzi yakinifu na usanifu wa kina unafanyika kwenye barabara ile, inapita Wilaya ya Simanjiro, lakini walipofika kwenye Kijiji cha Nadonjukin wataalam wanatoa sababu ya kupindisha barabara ile isipite Terrat kuelekea Orkesmet wakidai kwamba kuna wanyamapori wanaopita kwenye ile barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukijaribu kuangalia kwenye nchi yetu barabara ya Morogoro –Mikumi – Ilula – Iringa, pale katikati panapita wanyamapori. Pia barabara ya kutoka Minjingu kwenda Babati, kuna Mbuga ya Tarangire na Manyara katikati. Kimataifa, kuna barabara ya Kruger Park inayopita katikati ya National Park ya Afrika Kusini ya Kruger National Park. Barabara hizi zote zinapita katikati ya Mbuga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa TANROAD wanapitisha barabara ile wakiiacha Simanjiro yenye vijiji vya Terrat, Sukro, Narkawo, Loiborsiret. Huu ni uonevu na ubaguzi wa hali ya juu. Naiomba Wizara, Mheshimiwa Waziri kwa kitabu chake hiki, ajaribu kuangalia upya kwamba lazima barabara ile ipitike. Tunavyosema nyumbu anapita kwa miezi mingapi; wanakuja mwezi wa Tatu tu kuzaliana pale. Kwa hiyo, naomba ubaguzi huu usifanyike hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Manyara tangu barabara zake zipandishwe hadhi, mara ya mwisho ni mwaka 2009. Kuna barabara ya kutoka Msitu wa Tembo kwenda Korongo kuelekea mpaka Vijiji vya Nyumba ya Mungu mpaka Ngage. Barabara hizi kwa fedha za ndani za Halmashauri na TARURA haiwezi kuhudumia barabara hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wajaribu kuangalia namna gani Mheshimiwa Waziri apandishe hadhi barabara zetu ili TANROADS waangalie barabara hiyo yote inaenda mpaka Ruvu-Remit.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye ATCL. Kwenye ripoti ya Ofisi ya Msajili wa Hazina ukurasa wa nne, Afisa huyu anasema ATCL hesabu zake hazijawahi kukaguliwa kwa muda mrefu sana, lakini sababu hiyo hiyo ndiyo inatupelekea sisi tuseme kwamba inawezekana one point five trillion ambayo haionekani kwenye Hazina ya Serikali, inawezekana imetumika kwa sababu ya kutokagua mahesabu haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muda muafaka, wale wanaomshauri Mheshimiwa Rais, washauri vizuri. Mheshimiwa Magufuli hatadumu milele, ataondoka kwenye madaraka. Ninyi ambao hamumwelekezi kwamba anakosea saa nyingine, kama yeye ndio kachukua hizo fedha, ni muhimu ndugu zangu mumshauri vizuri. Fedha za umma ni za umma na mtu huwezi kuzichukua kama unavyotaka fedha zako za mfukoni. Kuna taratibu za kuchukua fedha hizi. Ni vizuri mshauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wanafanya hivyo Waheshimiwa Mawaziri, wakumbuke kwamba akina Yona walikuwa Mawaziri, wakumbuke kwamba akina Mramba walikuwa Mawaziri iko siku Watanzania watakuja kuwaulizeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nafanya Mahakama ya Kimataifa, Rwanda, watu waliokuwa wakimzunguka Rais Habyarimana mwaka 1994, walimshauri vibaya na ndiyo maana mauaji ya Kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 yakatokea. Nawaomba Waheshimiwa Mawaziri, watu wa karibu walioko karibu na Mheshimiwa Rais, washauri Mheshimiwa Rais kwamba nchi hii ni nchi yenye sheria, haiwezekani ukaweza kuchukua fedha zote kutoka kwenye Hazina ya Taifa ukapeleka mahali ambapo hazionekani. Ni muhimu ufuate sheria ili nchi hii iweze kuwaheshimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi…

KUHUSU UTARATIBU . . .

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabila la Kimasai kati ya vitu ambavyo hatuwezi ni unafiki. Najaribu kushawishi kwa nia njema kwamba inawezekana hawa ambao wako madarakani sasa, kama hawamshauri vizuri Rais, nitoe mfano mmoja; Police Ordinance, Political Parties Act, The Constitution haimpi mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukataza mikutano ya hadhara na hawa ambao wako karibu naye wanamnyima fursa ya kumshauri vizuri. Hivyo, ni vyema waliomzunguka Mheshimiwa Rais wakamshauri vizuri. (Makofi)

KUHUSU UTARATIBU . . .

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu waliokaa upande wa pili ambao kwa muda mrefu nimekaa na ninyi CCM, saa nyingine muwe mnakumbuka Kanuni ya 64 hiyo hiyo, mnapojaribu kushawishi Bunge kwa kumsifia Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa moyo wa dhati na ninyi ndio mtakaokaa upande wa pili kumpiga mawe baadaye Watanzania wakianza kuuliza maswali. Sisi wengine tuko upande huu… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)