Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Tanga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nashukuru kwa Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema katika kuchangia bajeti ya Wizara hii ambayo ni muhimu katika maendeleo ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda baada ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, niseme tu kwamba kwa ufahamu wangu, Bunge siyo rubber stamp, ni kwamba kinacholetwa hapa kinatakiwa kijadiliwe halafu tukubaliane kwa pamoja. Kazi ya Bunge ni kuisimamia Serikali. Sasa siyo lazima kila kinacholetwa hapa tuunge mkono hoja tu, hapana. Wakati mwingine kama kuna marekebisho, lazima yafanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, niseme tu, jana kuna mchangiaji mmoja hapa alitoa taarifa kidogo ambayo nami naungana naye. Kama sikosei alikuwa ni Mheshimiwa Silinde. Alizungumza akasema kwamba kuna barabara hewa ambazo zimetumia shilingi bilioni 252, lakini barabara hizi hazijulikani zimejengwa wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa, tupate maelezo ya shilingi bilioni 252 barabara zake zimejengwa wapi? Kama hilo halitoshi, nami ni Mjumbe pia wa PAC, tutakuja kuangalia huko katika vitabu tuone hiyo value for money.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine imezungumzwa pia kwamba tunaboresha Shirika la Ndege, lakini ili lifanye kazi vizuri, lazima liwe na routes, lisafiri sehemu mbalimbali, ndani na nje ya nchi. Sasa hapa naiomba Serikali kwamba pamoja na kwamba tunanunua ndege, lakini tujitayarishe katika kushindana na mashirika mengine makubwa ya ndege ili ndege hizi zisije zikaitia hasara Serikali kwa sababu Watanzania wana matatizo mengi sana, lakini hatukuyaangalia hayo, tumeona kwanza tuanze na ndege. Hilo pia bado taarifa ya CAG haipo na hii taarifa ya Shirika la ATCL hailetwi Bungeni kujadiliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo nianze kuchangia mchango wangu. Nataka kuizungumzia kwanza barabara ya Pangani. Kwa maoni yangu ni kama barabara ya Pangani ni mfupa uliomshinda fisi. Kwa nini nasema hivyo? Hii barabara imepita Marais wanne. Ameanza Mwalimu Nyerere akaweka ahadi; akaja Mheshimiwa Rais Mwinyi, akaweka ahadi, akaja Mheshimiwa Mkapa akaweka ahadi, amekuja Mheshimiwa Kikwete naye ameweka ahadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbarawa namheshimu sana pamoja na wasaidizi wake, lakini mwaka 2017 walituambia kwenye bajeti kwamba wametenga shilingi bilioni nne kwa ajili ya upembuzi yakinifu (feasibility study) na mambo mengine. Asubuhi pia nilimpelekea ki-memo kutaka kujua ufafanuzi, hii inayozungumziwa katika ukurasa 271 ndiyo hiyo barabara ya Pangani? Naona ile pesa imepungua! Sasa kila siku gharama za ujenzi zinakwenda mbele lakini bajeti ya barabara ya Pangani inapungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja anijuze na anishibishe ili nitakaporudi Tanga niwaambie watu wa Tanga kwamba safari hii barabara ya Pangani itajengwa au haijengwi? Kwa sababu tumechoka na ahadi zisizotekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amekuja Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, hata alipokuja kufanya ziara Tanga ya kuweka jiwe la msingi la bomba la mafuta nilimgusia suala hili na akaahidi kama ataijenga, lakini kwenye bajeti siioni. Sasa Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa aniambie hii barabara itajengwa au haitajengwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, namkumbusha kwamba barabara hii ina Wabunge wanne au watano; imeanza Tanga Mjini, inapita sehemu ya Kigombe ambayo ni Muheza kwa Mheshimiwa Adadi Rajabu, inaingia Pangani kwa Mheshimiwa Juma Aweso, lakini inaingia vilevile Chalinze kwa Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete. Kwa hiyo, Wabunge watano wote tumekuwa tukiizungumzia hii barabara, lakini inaonekana kama tunatwanga maji ndani ya kinu. Sasa tunataka kujua, hii barabara itajengwa au haijengwi? Kama haijengwi pia utupe jibu, kwa sababu tumechoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barabara ina historia ndefu. Nafikiri wakati wa miaka ya nyuma, wakati wa enzi za kupigania uhuru, wapo wapigania uhuru ambao waliitumia njia hii, lakini mpaka leo barabara nyingine za karibuni hapa zimejengwa. Hakuna barabara iliyokuwa ndefu kama kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza, imejengwa. Sasa inakuwaje kipande kidogo hiki cha Tanga – Pangani - Bagamoyo mpaka Dar es Salaam kishindwe kujengwa? Marais wanne wote wametoa ahadi mpaka leo barabara hii haijengwi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja anieleze hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme, kama hakuna fedha, tuitafute ilipo ile 1.5 trillion ili tuiingize katika barabara ya Pangani tuweze kujenga barabara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niizungumzie Bandari ya Tanga. Bandari ya Tanga ni bandari kongwe, ndiyo bandari ya kwanza kujengwa katika Afrika Mashariki na Kati, lakini bandari hii inapuuzwa. Tarehe 28 mwezi wa Pili nilialikwa katika Kikao cha Bodi ya Bandari wakawepo wafanyabiashara wa Mkoa wa Tanga na mikoa ya jirani pamoja na uongozi wa bandari, lakini ukisikiliza wafanyabiashara wanalalamika, viongozi wa bandari wanalalamika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari ile haina vifaa vya kisasa vya kushusha na kupakia mizigo. Kwa mfano, crane ya kubeba forty feet container haifanyi kazi, ni mbovu. Hata wakiomba fedha kwa ajili ya ukarabati pia haufanyiki. Sasa itakuwaje tuwe na bandari lakini haina vifaa vya kushushia mizigo, wakati tunaagiza mizigo kutoka nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo pia nitataka nijibiwe, linawezekana au haliwezekani? Ikibidi basi itafutwe fedha au Bandari ya Tanga nayo iingizwe katika bandari ambazo zinapelekewa vifaa vya kisasa na vya kutosheleza kupakia na kupakua mizigo. Kwa sababu Bandari ya Tanga inasemwa, inafanya kazi kwa hasara. Haifanyi kazi kwa hasara, haina vifaa. Hata muwe wengi vipi, hamwezi kubeba kontena la forty feet kwa mikono. Kwa nini bandari isifanye kazi kwa hasara?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini huu ni mpango wa kuiua makusudi Bandari ya Tanga kwa sababu haiingii akilini kwamba leo bidhaa zetu zote tuziingize katika Bandari ya Dar es Salaam hali ya kuwa Bandari ya Dar es Salaam yenyewe imefanyiwa ziara za kushtukiza. Mheshimiwa Waziri mwenyewe amefanya, Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya na Mheshimiwa Rais amefanya, lakini pana matatizo hayamaliziki. Kwa nini hawabadilishi bandari?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie, hata alipokuja Mheshimiwa Rais Tanga katika bomba la mafuta nilipata nafasi ya kuzungumza nikasema lazima tufanye categories za mizigo. Haiingii akilini, Bandari ya Mtwara imelala, Bandari ya Tanga imelala, ifanye kazi Bandari ya Dar es Salaam peke yake. Nikaishauri Serikali kwamba baadhi ya mizigo iwe inateremka katika kila bandari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Mikoa ya Ruvuma, Mtwara kwenyewe, Katavi, Rukwa na Sumbawanga huko pamoja na nchi za Zambia na Malawi mizigo yao ingeshuka Bandari ya Mtwara kwa sababu pana Mtwara Corridor. Bandari ya Tanga ishughulikie mizigo ya Tanga yenyewe, Moshi, Arusha, Manyara, Simanjiro na Musoma pamoja na nchi za Uganda labda na Rwanda mizigo yake ingekuwa rahisi kwa gharama kuishushia Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali mnayoisema sikivu, sijui usikivu huo uko wapi? Kwa sababu tunakubali sasa bandari moja ya Mombasa mapato yake kwa mwaka inazishinda bandari nne za Tanzania. Bandari ya Zanzibar, Dar es Salaam, Mtwara na Tanga, mapato yake ukiyajumuisha vyote kwa pamoja hayafikii Bandari ya Mombasa. Kwa nini? Wenzetu wameamua kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalozungumzia…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.