Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Devotha Methew Minja

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia dakika tano hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia watu wanasifu Wizara inafanya vizuri, lakini kwa wananchi wa Manispaa ya Morogoro hawawezi kuwasifia hata mara moja. Ni kwa nini nasema haya? Kuna barabara ya Tubuyu – Kichangani katika Manispaa ya Morogoro. Barabara ile ina kilometa nne tu imejengwa, kilometa moja imejengwa kwa shilingi bilioni 3.4; kilometa nne zimejengwa kwa shilingi bilioni 13.6. Barabara imenyooka kama chuma cha pua; barabara unaweka rula unanyoosha, haina milima, mabonde wala mito. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana Madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambao waliungana nami pamoja na baadhi ya Madiwani wa CCM. Mwaka 2017 nilisema na kwa bahati nzuri baada ya kuona kwamba hela hizi zimepigwa; tuliamua kwenda kwa wataalam wa TANROAD tukawaambia hebu tuambieni, sisi sio wataalam, tunataka kujua barabara hii kwa nini imejengwa kwa gharama hizi nyingi kiasi hiki? Nao wakawa wanashangaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakatuambia kilometa moja standard yaani barabara concrete inajengwa kwa shilingi milioni 800 mpaka shilingi bilioni moja tena kwenye maeneo ambayo ni korofi. Tukawaambia hapa zimetumika shilingi bilioni 13.6. Wakatuambia hatujawahi kuona, pengine ni kwenye barabara za ahera ndiyo zinaweza kuwa na gharama kubwa kiasi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukaanza kupambana ndani ya Halmashauri yetu, tukajaribu kuuliza matumizi ya fedha hizi. Ikumbukwe fedha hizi ni mkopo wa World Bank ambao uliletwa kwenye nadhani Halmashauri kadhaa kama saba hivi na Halmashauri ya Morogoro ikiwemo, ambazo tunategemea kwamba Watanzania watakuja kuzilipa kwa jasho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokuja na hoja hiyo Halmashauri, viongozi wa Halmashauri wakaanza kutembeza rushwa kwa Madiwani na Madiwani wakasema hawakubaliani na hali hii, wakaandika barua kwa Mkuu wa Mkoa kuthibitisha wamepewa rushwa ili wanyamaze kwenye jambo hili. Nakala wakapeleka kwa DSO na RCO wakasema sisi hatupo tayari, tupo tayari kuhakikisha kwamba tunataka kujua hatma ya fedha hizi. Ukimya mpaka leo, hakuna kilichoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukuishia hapo, tukaja Bungeni, nikazungumza, nikamwomba Mheshimiwa Jafo wakati huo akiwa Naibu Waziri. Akaenda Morogoro akaiona barabara ile, akaunda Tume. Hata Tume aliyoiunda mwaka 2017 mpaka sasa hivi hakuna kitu ambacho kimefanyika mpaka sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Jafo alikuja ameunda Tume akashangaa barabara kutumia fedha nyingi kiasi hiki, lakini mpaka sasa amekuwa Waziri ni kimya.

T A A R I F A . . .

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema baadhi ya Madiwani na ambao walikwenda TAKUKURU kutoa ushahidi kabisa kwamba wamepewa ili wanyamaze.

T A A R I F A . . .

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa. Watu wamefanya Mkoa wa Morogoro ni shamba la bibi, ni lazima tuseme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tukawa tunavizia tukutane kwenye Kikao cha RCC tuweze ku-raise hoja zetu kuhusu barabara hizi, lakini tumepigwa ile inaitwa nini?

Chenga ya mwili. Mkoa wa Morogoro haukufanya kikao cha TANROAD wala hatukufanya kikao cha RCC. Tumekuja Bungeni tunakutana na vitabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkuu wa Mkoa anakwepa kujibu hoja hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalipeleka wapi Taifa hili?