Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Sixtus Raphael Mapunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa na mimi nafasi ya kuchangia jioni hii ya leo. Naomba tu nikwambie kwamba nimeongea na Mheshimiwa Mlinga ameniambia nitakapoishia, dakika zake tano nitaendelea kuongea mimi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takriban miongo miwili na nusu, yaani miaka 25 Shirika letu la Ndege la Taifa lilikuwa linafanya vibaya sana. Watu wote tulikuwa tunalitazama kwa aibu na kuna baadhi yetu walilalamika na kusema tunazidiwa na kanchi kidogo kama Rwanda, tunazidiwa mpaka na Msumbiji ambao wana ndege yao kwa wiki inakuja Tanzania mara moja. Hayo yote yalitukwaza wengi sana ambao tulikuwa na nia ya kuiona Tanzania ikisonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee sana, nampongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kuamua kwa makusudi kututoa kwenye msukosuko wa miaka 25 ambapo shirika letu la ndege la Taifa lilikuwa linayumba.

T A A R I F A . . .

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikuombe unitunzie muda wangu, halafu pili sitaijibu hiyo, inanipotezea muda wa kushusha yale ninayopaswa kuyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni. Ni ninyi ambao mlikuwa mnasema shirika hili halifai; ni ninyi mliokuwa mnasema kwamba hatuna ndege hata moja. Juzi tumenunua ndege, nyie mnakuwa tena wa kwanza kuturudisha nyuma kwa nini tumenunua ndege?

Haki yake mpeni! Ni Kiswahili safi. Hivi nani asiyejua kwamba Rais wetu amekuwa na ujasiri mkubwa wa kulifufua shirika la ndege?

Nani asiyejua humu ndani? Kinachowakwaza nini kulisema jina la Rais kwenye mambo yaliyo mema? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu ni kawaida yao, wana macho lakini hawaoni; wana masikio lakini hawasikii; na wana roho zenye chuki zisizoweza kutenda jema lolote. Sasa tukisifia mambo mazuri wanataka tuseme nini? Ni wao walikuwa wanasema hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mchana Mheshimiwa Halima Mdee alilidanganya Bunge. Nataka nimpe taarifa mchana ule, lakini kwa sababu nilijua nitapata muda sasa hivi, nikasema niutumie muda huu kwanza kumpa hiyo taarifa na kuwapa taarifa watu wengine wote ambao wanaona lakini wanajifanya hawaoni; wanasikia na wanajifanya kuwa hawasikii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Halima Mdee mchana alisema ATCL haina strategic plan na haina business plan. Mwaka 2017 tukiwa kwenye Kamati ya PIC tuliliita Shirika la ATCL. Mimi nilikuwa Mjumbe na cha kushangaza wengine waliokuwa wanapiga makofi kwenye uongo huo nao walikuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namba moja, Mheshimiwa Frank Mwakajoka tulikuwa naye; namba mbili, Mheshimiwa Esther Bulaya, tulikuwa naye; namba tatu, Mheshimiwa Maftaha, tulikuwa naye; namba nne, Mheshimiwa Kwandikwa tulikuwa naye; na namba tano, Mheshimiwa Edwin Sannda tulikuwa naye. Kwenye taarifa yao, sio yangu. Walisema mwezi Juni, 2016 Serikali iliamua kulifufua upya shirika la ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kulifufua Shirika la Ndege lilikuwa na mambo mawili ilibidi yote yafanyike kwa wakati mmoja. Jambo la kwanza kurudisha hadhi ya ATCL kipindi inaelekea kufa; na suala la pili kuifanya iendelee kwenda kwa muda mrefu ili tusirudi kwenye upungufu uliofanya shirika life. Katika kipindi cha mwaka mmoja kilikuwa mwezi Juni, 2016 na Julai, 2017 ATCL walikuwa wana mpango wa muda mfupi ulioitwa Turn Around Strategy.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017/2018 wakaja na mpango wa miaka mitano ambao ni Corporate Strategic Plan iliyokuwa na malengo yafuatayo:-

T A A R I F A . . .

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza anazidi kuongopa, anasema amepata Taarifa ya Msajili wa Hazina ya Mwaka 2007 na wakati mimi naongea strategic plan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango mkakati wa mwaka 2017 - 2022, shirika liliamua kwa makusudi kufanya mambo matatu. Jambo la kwanza, kuhakikisha wananunua ndege mpya ambayo wamefanya; jambo la pili, ilikuwa ni kuendeleza marubani ili itakapofika ndege zote tusipate anguko ambalo lilipatikana miaka 25 iliyopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa Shirika la Ndege, kutokana na mikataba mipya ya kununua ndege mpya, inasomesha marubani 62. On top of that, inasomesha marubani 12 kutokana na makubaliano ya Shirika la Ndege la Taifa la Tanzania pamoja na Shirika la Ndege la Ethiopia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naomba niseme kuhusu faida zinazoweza zikapatikana na ATCL. Wengi wamesema wakiangalia hasara ya uendeshaji wa Shirika la Ndege kwa kuangalia ununuzi wa tiketi na huduma ambazo ndege inatoa ndani ya ndege kipindi abiria wanasafiri. Shirika la Ndege ukiondoa hizi faida zinazoonekana moja kwa moja ina faida tatu kubwa, faida ya kwanza ni ancillary services. Kuna muda ukimsafirisha abiria nchi inapata faida kwa huduma ambazo katika nchi husika zinatolewa. Naomba nitoe mifano ya mashirika ya ndege ambayo hayakuwahi kupata faida ya moja kwa moja ya tiketi, lakini yalipata faida kutokana na ancillary revenue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ya kwanza ni Shirika la Ndege la EasyJet la Uingereza mwaka 2006 walipata faida ya jumla ya Euro milioni 189; Shirika la pili ni Aer Lingus ya Ireland ilipata faida ya Euro milioni 63; Shirika la Tatu ni AirAsia ya Malaysia, lilipata faida ya Euro 22. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne ni United Airlines la United States of America, mwaka 2009 lilipata faida ya bilioni 1.5 nje ya kuuza tiketi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema, watu wasiojua hii industry, wakasome waijue, wasibishe vitu wasivyovijua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.