Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Edwin Mgante Sannda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. EDWIN M. SANNDA: Sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa nichukue fursa hii kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri zaidi inayofanywa. Pia nimpongeze Mheshimiwa Profesa Mbarawa, ndugu yangu Mheshimiwa Kwandikwa na mwenzangu Mheshimiwa Nditiye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo matatu madogo. La kwanza katika kuunga mkono jitihada za kuhamia makao makuu na kuchochea maendeleo ya maeneo ya makao makuu tumeona hapa kwenye CDD, mji wa makao makuu tunajenga ring roads lakini pia tunahitaji kujenga ring roads kwenye wilaya za pembezoni mfano unazungumzia Katesh - Kondoa, Babati - Kiteto ili na haya maeneo mengine ya pembezoni yaweze kuchochewa maendeleo kwa kupitia miundombinu ya barabara kama za lami. Ring roads zitengenezwe sio tu kwa makao makuu lakini nje ya mji wa makao makuu kwa kiwango cha lami. Hii itatusaidia sana katika kuchochea maendeleo ya maeneo yale ya pembezoni. Hilo ni moja ambalo ningeshauri lifanyiwe mchakato na lenyewe liweze kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni suala la TARURA. Hawa watu wa TARURA na wenyewe ni wataalam kama ambavyo TANROADS walivyo lakini barabara zinazotengenezwa na TARURA zinaonekana kama ziko chini sana ya viwango. Unatengeneza barabara hakuna mitaro wala matoleo matokeo yake mahitaji ya matengenezo yanakuwa ya mara kwa mara.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeshauri tutengeneze vigezo vya viwango kwamba kila barabara inayotengenezwa iwe na viwango kama ambavyo kwenye TANROADS wanatengeneza ili barabara hizi ziweze kudumu na kukaa muda mrefu whether ni ya light grading au iwe heavy grading lakini vigezo vya mitaro kwa maana ya mifereji na matoleo viweze kuwepo maji yapite barabara zidumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine hapohapo kwenye TARURA, nadhani ni muhimu kidogo kuongeza bajeti. Ule mgawanyo wa 30 kwa 70 sasa tuufikirie hata kama sio 50 walau 40. Najua kiwango cha barabara zinazotengenezwa na TARURA haziwezi kuhitaji gharama kubwa kama hizi barabara kuu za lami, lakini mtandao wake ni mkubwa sana. Tunahitaji tuwaongezee bajeti na wao waweze kufanya kazi ambayo itakidhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hapo hapo kwenye TARURA, wazingatie vipindi vya kutengeneza barabara. Tunapoteza hela kwa kutengeneza barabara wakati wa mvua, muda mfupi tu baadae inabidi turudie. Kwa hiyo, labda kile kipindi cha mvua ni kuangalia upungufu uko wapi halafu baada ya mvua ndiyo barabara zinatengenezwa, hasa zile za udongo na za viwango vya changarawe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, nataka kuongelea kuhusu alama za barabarani kwenye hii barabara yetu ambayo Mheshimiwa Rais anakwenda kuifungua rasmi kesho kutwa tarehe 27 Aprili. Barabara imejengwa vizuri, tunawapongeza sana lakini kuna maeneo mawili ya hatari sana, pale kwenye Daraja la Ausia na kwenye Milima ya Kolo, ni maeneo hatari kwelikweli yanahitaji kuwekwa alama za aina yake, alama kubwa kama kule kwenye madaraja mengine kama Wami ili kupunguza ajali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yale yamekuwa wakisababisha ajali nyingi sana na kupoteza maisha ya Watanzania wenzetu. Kwa hiyo, tunasisitiza na kusihi, tumeshaongea kwenye Bodi ya Barabara ya Mkoa lakini si vibaya kuliweka tena hapa, ili mradi suala hili lipewe uzito unaostahili na hatimaye alama hizo kubwa kabisa ziwekwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine na dogo la mwisho, nataka kuzungumzia habari ya mawasiliano kwenye Jimbo la Kondoa Mjini. Mawasiliano yapo karibu maeneo yote lakini yapo maeneo yenye changamoto mawasiliano hayapatikani vizuri hasa katika Kata za Kondoa Mjini, Seria pamoja na Kingale usikivu unakuwa siyo mzuri na drop calls mara nyingi zinatokea. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri na timu yake hebu naomba watuangalizie kule Kondoa nini tatizo hasa ili tuweze kulipatia ufumbuzi tatizo la mawasiliano yasiyosikika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, kwa kuwa najua sasa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.