Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mchinga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa nasimama kwa mara ya kwanza katika hotuba ya bajeti, nawashukuru kwa dhati kabisa wananchi wa Jimbo la Mchinga kwa kuniamini, kwa kunichagua kwa kura nyingi sana na hatimaye kuwa Mbunge wao, Mbunge jirani kabisa na Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, itoshe kuwashukuru na kuwapongeza Wabunge wenzangu wote waliozungumzia suala la korosho. Namshukuru sana dada yangu Mheshimiwa Ghasia, leo naona amepiga hoja nzuri hapa. Namshukuru sana Mheshimiwa Chikota, Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mheshimiwa Katani na wengine, wamejenga hoja za kimsingi kuhusu zao la korosho. Kiukweli kabisa, zao la korosho ni miongoni mwa mazao yanayoliingizia Taifa hili fedha nyingi, lakini inaonekana kama tunacheza nalo, bado tunacheza! Inaonekana kama we are not Serious kwenye zao la korosho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Mwigulu Nchemba awe mtu wa kwanza kuwafuta machozi wakulima wa korosho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie alipoishia Mheshimiwa Hawa Ghasia kwenye suala la uvuvi na matumizi makubwa ya nguvu za dola katika kupambana na uvuvi haramu wakati uwekezaji tunaowekeza kwenye kuwasaidia wavuvi ni mdogo mno. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na-declare interest kwamba, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Kilimo. Wakati wa Vikao vya Kamati na Mheshimiwa Waziri jana wakati anawasilisha hoja yake alieleza mikakati ya namna wanavyopanga kushirikiana na jeshi kwenda kuzuia uvuvi haramu. Nataka nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, mwaka 1997 na 1998 Serikali hii ilitumia jeshi, lakini leo uvuvi haramu bado unaendelea. Tusiangalie tulipoangukia, tuangalie tulipojikwaa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, matumizi ya jeshi hayatatusaidia, badala yake tunakwenda kuwaumiza wavuvi, wananchi wetu watapigwa, watadhalilishwa na haya yote yana ushahidi wa kutosha. Niwashauri Waheshimiwa, kama mnataka kutumia jeshi, hakikisheni mnaandaa Leseni za Uvuvi za Mbao, kwa sababu zitakuwa haziharibiki, wavuvi wanakwenda baharini wakiwa na leseni zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, najua mwaka 1997/1998, mimi mwenyewe nikiwa mvuvi ilikuwa ukienda baharini unaambiwa onesha leseni yako! Leseni ni karatasi. Mimi nakwenda kuzamia, navua pweza kwa kutumia kioo kuzamia baharini. Nibebe leseni kule chini ya bahari si itaharibika! Kwa hiyo, niwashauri kama mmeweka mkakati wa kutumia jeshi, please andaeni leseni za mbao, hazitaharibika, tutakwenda nazo baharini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mjiandae pia kupokea watu majeruhi wengi kwa sababu najua wavuvi wengi watapigwa, watadhalilishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala hapa ameliongea Mheshimiwa Ghasia; suala la wavuvi kukata leseni, nikiwa Lindi Vijijini pale Mchinga nakata leseni; nikitoka, nikienda Kilwa, nakata leseni; katika nchi moja, mkoa mmoja mnatutenganisha! Yaani Lindi Vijijini nikitoka hatua kumi kwenda Kilwa, natakiwa nikate leseni nyingine! This is very shameful! Wavuvi wanapata wapi hii fedha? Msitutenganishe kimikoa na kiwilaya jamani! Nawaomba sana, tunaishi kindugu; kama ni wilaya kwa wilaya mtu anatakiwa akate leseni, tunawaumiza sana wavuvi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la ufuta. Mheshimiwa Mwigulu nchi yetu wewe unajua ni nchi ya tatu kwa kulima ufuta mwingi duniani. Ni nchi ya kwanza kwa kulima ufuta mwingi Afrika. Unajua! Mkoa wa Lindi ndiyo Mkoa unaolima ufuta mwingi kuliko mikoa yote Tanzania, unajua! Hivi sasa ninavyokwambia, tayari wanunuzi wa ufuta, hao wanaoitwa Choma Choma, wako Lindi wananunua ufuta.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa hatujui ni mamlaka gani inayoweza kutangaza bei elekezi ya zao la ufuta. Mpaka hivi sasa tunapoongea, ufuta unanunuliwa kwa sh. 1,300/=, sh. 1,800/=, kwa decision ya mnunuzi. Serikali iko kimya, Mkuu wa Wilaya yupo kule, Mkuu wa Mkoa yupo kule! Naomba Mheshimiwa Waziri, toeni tamko, bei ya ufuta mwaka huu ni shilingi ngapi? Mtuambie! Watu wanauza sh. 1,300/=, sh. 1,800/=, kwa kweli tunawaumiza sana wakulima wa ufuta. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwenye suala la mifugo. Mkoa wa Lindi mmepeleka ng‟ombe wengi, wafugaji wengi; tulitegemea kungekuwa na mpango mzuri kabisa wa kupanga matumizi bora ya ardhi; wakulima wakae wapi, walime wapi na mifugo ifugiwe eneo gani. Nasikitika sana, najua Wizara iliomba shilingi bilioni tatu za kupanga matumizi bora ya ardhi, mmepewa shilingi milioni 25.
Naomba Waheshimiwa Wabunge tuhakikishe Wizara hii inapewa hizi fedha, shilngi bilioni tatu. Shilingi milioni 25 hawawezi kupanga hawa matumizi bora ya ardhi, ku-demarcate maeneo kwa ajili ya wafugaji na wakulima. Otherwise migogoro ya wakulima na wafugaji itaendelea, haitakwisha na tutaendelea kuishuhudia kila siku Kilombero na maeneo mengine. Hata kule Lindi ambako ni wastarabu sana, lakini kuna viashiria vyote kwamba kama hali hii itaendelea na kwenyewe tutaanza kuweka kwenye eneo la kimgogoro!
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, naomba take this issue very serious, hakikisheni mnapata fedha za kutosha mfanye demarcation ya maeneo kati ya wakulima na wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie tu, nasikitika sana na Mheshimiwa Nape hapa hayupo, ni Mbunge mwenzangu kwenye Halmashauri moja kwenye wilaya moja; nasikitika, najenga hoja hapa za wavuvi hawanioni, hawanisikii; najenga hoja hapa za wakulima hawanioni, hawanisikii na Watanzania wanatulalamikia!
Mheshimiwa Naibu Spika, siungi mkono hoja!