Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuanzia naomba niwapongeze Mheshimiwa Waziri Profesa Mbarawa, Mheshimiwa Engineer Nditiye na Mheshimiwa Kwandikwa kwa kazi wanazoendelea kuzifanya na kwa ujumla wake chanda chema hivikwa pete. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mpanda – Koga – Tabora kwa maana ya kilometa 373 inayoendelea kutengenezwa, naendelea kuieleza Wizara, tunalo eneo korofi la Mto Koga. Eneo lile ni korofi muda wote, kwa mfano sasa hivi barabara ile haipitiki kutokana na ukorofi wa ule Mto Koga. Naomba hata haya matengenezo yanayoendelea tuzingatie maeneo yale ya daraja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana wakati tukiitengeneza barabara hii kwa kiwango cha lami kwa ajili ya kukomboa maeneo yote ya Mkoa wa Katavi na Tabora kwa ujumla wake, tusisahau barabara ya Mpanda – Ugala – Kaliua – Ulyankulu - Kahama kwa maana ya kilometa 457.
Barabara hii hata kama ikitokea imepata tatizo tunakuwa na escaping route, hii barabara nyingine inatukomboa wakati ambapo barabara moja inakuwa na matatizo. Kwa hiyo, naomba barabara zote hizi ziende sambamba, lakini napongeza jitihada ya kutengeneza barabara ya Mpanda – Koga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la Kiwanja cha Ndege cha Mpanda. Mara ya mwisho niliuliza swali hapa, Naibu Waziri, Mheshimiwa Engineer Nditiye alinihakikishia kupatikana kwa gari la zimamoto katika uwanja ule. Pamoja na kupatiwa gari la zimamoto na huduma nyingine tunaomba tupatiwe route sasa ya ndege kuja eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikizungumzia suala la route za ndege, vigezo vya kusema, je, tutapata wasafiri, hebu leteni ndege halafu muone kama mtapata wasafiri. Kuna maeneo mwanzoni walikuwa wanaona kama hawana wasafiri, nitatoa mfano wa Bukoba, leo hii wanatamani kuongeza route au Tabora, tunaomba mtuletee ndege halafu muone. Hii habari ya kusema tutapelekaje magari hakuna abiria lakii mkipeleka barabara mnashangaa magari yamejaa. Sasa hivi Sumbawanga kwenda Mbeya magari ni mengi lakini mwanzo walikuwa wanasema route ile haina magari. Kwa hiyo, naomba upande wa uwanja wa ndege tuleteeni route halafu muone. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo naomba nizungumzie suala la reli. Kipindi hiki naomba ziendelee kutengwa fedha za kutosha kwa ajili ya ukarabati wa reli kutoka Tabora - Mpanda, maeneo ni korofi. Sambamba na utengenezaji naomba kitu kingine, tuna mabehewa machache na nashangaa reli ile kwa muda mrefu hatujabahatika kupata behewa la daraja la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, najiuliza wananachi wako kule na si kwamba wanapanda bure, wanalipia, vipi tunashindwa kupatiwa behewa la daraja la kwanza? Naomba ufafanuzi wa suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba niwasemee pia wananchi wa maeneo ya Msasani - Tambukareli. Kulikuwa na bomoabomoa, wataalam njooni muendelee kutusaidia, je, ni umbali upi hasa ambao watu wanatakiwa kupewa fidia? Njooni mtusaidie kuangalia kama wananchi wale wako katika maeneo husika na kama kweli wako katika maeneo husika wale ambao wamebomolewa suala la fidia lichukue mkondo wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niseme jambo moja lenye sura ya kitaifa. Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam ni jicho la nchi hii, ni kioo cha nchi hii na ni ubalozi unafanyika pale, wanapokuja watu kutoka nchi za nje inatia aibu. Naomba kasi ya ujenzi wa Terminal III iongezwe maana nimejaribu kuangalia hapa kwa kipindi hiki wametengewa shilingi milioni 179.82 kwa ajili ya ujenzi wake, tuujenge uwanja huo. Watalii wanapokuja, watu mbalimbali wanapokuja tunapata aibu na jambo dogo kama suala la air condition katika uwanja ule linatutia aibu.
Naomba tulifanye hilo kwa sababu mtu anapokuja…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja.