Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Ally Seif Ungando

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha hapa leo salama salmini nachangia katika Bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na barabara ya Bungu – Nyamisati. Waziri barabara hii ni muhimu sana na ukiangalia ni ahadi takribani ya Marais awamu mbili zilizopita walisema kwamba barabara hii tutajengewa kwa kiwango cha lami. Barabara hii ikijengwa itafaidisha Wilaya mbili, Wilaya ya Kibiti na Mafia. Mimi kila siku napokwenda kwenye mikutano yangu ya hadhara nashindwa kutoa jibu kuhusu barabara hii ya Nyamisati kwamba Serikali ina mpango gani kuhakikisha inajengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna barabara ya kutoka Kibiti kwenda Mloka; barabara hii nayo ni muhimu sana ukizingatia sasa hivi kuna mkakati wa kufua umeme wa maji kule Mloka. Ningeomba sasa Serikali basi iangalie kwa jicho la huruma barabara hii ya Bungu - Nyamisati na Kibiti - Mloka na ukiangalia hivi karibuni Wilaya ya Kibiti tumekumbwa na janga la watu wasiojulikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ziko barabara zetu za mitaa ambazo ni barabara za Kibiti, Bungu na Jaribu, TARURA haina kipato kikubwa cha kuweza kujenga barabara hizi kwa kiwango cha changarawe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna ujenzi wa Gati Nyamisati ambapo tunaambiwa mkandarasi yuko site lakini leo asubuhi nimeongea na wananchi wangu wa Nyamisati bado kazi haijaanza ya ujenzi wa Gati Nyamisati. Tukijenga Gati Nyamisati watafaidika wananchi wa Kibiti, lakini hata wananchi wa Mafia watafaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tatizo kubwa la wananchi wanaokwenda Mafia kutoka Nyamisati hawana usafiri wa uhakika. Tunaiomba Serikali waangalie jinsi gani ya kutununulia meli ili tupeleke kule Nyamisati itoke Nyamisati na kwenda Mafia. Usafiri ambao unatumika sasa hivi ni usafiri ambao siyo salama, siku yoyote Mwenyezi Mungu akileta mtihani wake linaweza likatokea la kutokea. Kwa hiyo, tunaomba Kibiti na Mafia muiangalie kwa jicho la huruma, sababu tunajua ndiyo kasungura kenyewe ni kadogo lakini hiki hiki tugawane na siye wananchi wa Kibiti tufaidike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda katika mawasiliano, Kibiti kwenye baadhi ya maeneo yetu hatuna mawasiliano kwa maana ya minara ya simu. Iko minara miwili ambayo imejengwa maeneo ya Delta, kule Mbwera lakini mpaka leo haijafunguliwa. Uko mnara umejengwa Mbuchi lakini mpaka leo bado haujafunguliwa lakini viko karibu vijiji 20 hatuna mawasiliano ndiyo maana hata kule Delta tukivua samaki wetu tunashindwa kupiga simu sokoni kujua leo soko bei yake ikoje. Kama kungekuwa na mawasiliano tungepiga simu tukajua sokoni leo prawns bei imekuwa juu na sisi tupeleke samaki wetu ili tupate faida yenye tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwa ndugu zetu hawa wa SUMATRA. SUMATRA wanafanya kazi lakini ninachoomba watoe ushirikiano na wadau. Hivi leo Kibiti wamezuia Noah zisipakie abiria kwenda kwenye barabara kuu, lakini wametoa zuio lile hawakuwashirikisha wadau. Kumekuwa na manung’uniko mengi inaonekana Serikali hii ya Awamu ya Tano siyo ya wanyonge kwa sababu wamefanya maamuzi pasipo kuwashirikisha wadau. Wangewashirikisha wadau wangejua mbadala wake ni nini kusingekuwa na manung’uniko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Wizara hii ya Ujenzi kwamba barabara nyingi zinazokwenda mikoani ziimarishwe na washirikiane na Wizara ya Mambo ya Ndani kwa sababu nguvukazi nyingi zinatembea barabarani kwa muda mrefu mchana. Kwa mfano, mtu anapanda basi saa 12.00 Dar es Salaam anakuja Dodoma anafika saa 12.00 jioni, muda ule ukiuangalia ni kwamba watu hawakuweza kuzalisha mchana kutwa walikuwa wanatembea tu barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika takwimu takribani wananchi 12,000 kwa siku wanatembea barabarani kwa muda mfupi. Ningeomba sasa waangalie utaratibu kama nchi jirani ya Kenya wananchi wengi wanasafiri usiku ili mchana waweze kufanya kazi na shughuli za uzalishaji mali. Kwa hiyo, hili liangaliwe kwamba jinsi gani wataboresha ulinzi na usafiri wananchi wasafiri usiku ili mchana waweze kuzalisha mali na kuiletea tija Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine niipongeze sana Serikali yangu ya Awamu ya Tano ambayo inaongozwa na Chama cha Mapinduzi. Ndugu zanguni kila zama ina wakati wake. Tulianza na Mzee wetu hapa Baba wa Taifa (ujamaa na kujitegemea), akaja Mzee Mwinyi (ruksa), kweli tukaona ruksa, akaja Mzee Mkapa (utandawazi) kweli tukaona utandawazi, akaja Mzee Jakaya (maisha bora kwa kila Mtanzania) lakini sasa tumekuja Hapa Kazi Tu. Sasa nashangaa kazi inafanyika bado watu wana maneno maneno. Jamani tubadilike, sasa hivi hakuna maisha ya ujanja ujanja, sasa hivi ni maisha ya Hapa Kazi Tu. Pia inasemwa asiyefanya kazi asile, hata kwenye vitabu vya dini ipo. Kwa hiyo, ndugu zangu kama mlikuwa ni watu wenye ujanja msubiri mwaka 2025 muendelee na ujanja wenu, lakini awamu hii ni awamu ya Hapa Kazi Tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado nipo katika Jimbo langu la Kibiti tunashukuru tumepata pesa ya kujenga daraja katika Daraja la Mbuchi, lakini barabara ya kutoka Muhoro kwenda Mbwera naomba nayo hii muiangalie kwa jicho la huruma.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni kwa kunisikiliza, naunga mkono hoja.