Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nadhani ninazo dakika kumi hapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Waziri mwenye dhamana, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa pamoja na wasaidizi wake Engineer Atashasta Nditiye na Mheshimiwa Kwandikwa kwa kazi nzuri wanayoifanya. Tuombe Mwenyezi Mungu aendelee kuwabariki na jukumu letu sisi ni kuwatia nguvu na kuishauri Serikali katika yale ambayo wanayatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala la gati katika eneo la Mkinga ambalo tumepata mwekezaji wa kiwanda kikubwa sana cha saruji. Niombe sana Wizara hii ihakikishe kwamba jambo hili linakwenda kutokea. Tunazungumza mara kwa mara humu ndani ya Bunge kwamba tunahitaji kuwa na miradi ya PPP.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii japo sio PPP lakini private sector moja kwa moja ameamua kuwekeza kujenga gati katika eneo hili la Mkinga ili aweze kurahisisha shughuli zake katika kiwanda cha saruji ambacho kitakuwa kikubwa zaidi kuliko viwanda vyote vilivyopo nchini na kitakuwa kinazalisha sana. Kwa hiyo, niombe sana wizara hii iharakishe kutoa vibali vyote vinavyohusika ili jambo hili litokee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunatambua uwepo wa reli ya Tanga - Arusha kwenda mpaka Musoma, reli hii ilikuwa inazungumzwa mara kwa mara lakini sasa tunaomba pamoja na jitihada ambazo zimeanza kufufua reli ya zamani na nimpongeze sana Mkurugenzi wa Shirika la Reli, Ndugu Masanja Kadogosa kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya lakini tunaomba sasa kwenye huu mpango wa standard gauge uchukue hatua za haraka na sisi tuweze kuwa na reli hiyo ya kiwango cha kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni miongoni mwa mashahidi ambao wamepita barabara ya kutoka Mlalo kwenda Lushoto kilometa 45. Barabara hii tumekuwa tukiiombea fedha mara kwa mara katika mfuko wa barabara wa mkoa lakini mara nyingi tunakwamishwa na wenzetu wa Wakala wa Barabara Taifa (TANROADS). Engineer Mfugale ninafahamu kwamba upo katika majengo haya na unasikia, barabara hii ya Lushoto – Mlalo ni muhimu sana kwa shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, shughuli kubwa ya uchumi ya wananchi wa Lushoto ni kilimo cha mboga mboga na matunda. Kwa hiyo, utagundua kwamba bidhaa hizi zinatakiwa zifike sokoni kwa wakati. Sasa kama hatuna barabara madhubuti maana yake ni kwamba wananchi wanapata hasara kwa sababu kwa kuwepo kwa barabara ambazo sio rafiki mazao yanaharibika yakiwa njiani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana tumeshaomba mara mbili kufanyiwa upembuzi yakinifu pamoja na detailed designing ya barabara hii na kila mara tukiomba wenyewe hawaleti mrejesho.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana safari hii barabara hii iingizwe katika mpango, najua mwaka huu tumeshachelewa lakini katika mwaka wa fedha unaokuja tafadhali sana kilometa hizi 45 tupate barabara ya kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la mawasiliano ya simu, katika Halmashauri ya Lushoto maeneo mengi tunashukuru kwamba simu zinapatikana. Changamoto ipo kwa sababu jiografia yetu ni milima baadhi ya maeneo ya mabondeni hakuna mawasiliano mazuri. Kwa hiyo, niwaombe tu wizara pamoja na wadau wote wanaohusika katika eneo hili waweze kuona kwamba namna gani tutaboresha mawasiliano ili wale ambao wapo katika maeneo ambayo yamefunikwa na vilima waweze kupata mawasiliano ambayo yataweza kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Tanga – Pangani mpaka Bagamoyo ni barabara ya siku nyingi sana na ni barabara ya kimkakati kwa maana ipo katika ramani ile ya Afrika Mashariki. Tumeanzia kutoka Horohoro kuja mpaka Tanga sasa tunataka kilometa 45 zile za Tanga – Pangani, lakini pamoja na kuunganisha na kipande cha Mwela – Sakula – Madanga – Saadan mpaka Bagamoyo ili tuweze kusaidia pia kuimarisha shughuli za kiuchumi pamoja na kutangaza mbuga zetu za Saadan kwa upande wa Bagamoyo na Tanga, lakini pia Mbuga ya Mkomazi ambayo ipo katika Mikoa ya Kilimanjaro na Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la ATCL hasa suala la ndege kwamba watu wengi wanazungumzia ndege kama biashara ya chai kwamba asubuhi anapika maandazi na chai, jioni atapata faida, hili ni suala ambalo lina multiplier effect. Yapo mambo mbalimbali ambayo uwepo wa ATCL umesababisha hata bei ya ndege kushuka, tulikuwa tunaona hapa FastJet na ndege nyingine binafsi zilikua zinatoza gharama kubwa sana kutoka eneo moja kwenda lingine, lakini uwepo wa ATCL na bombardier hizi umesaidia hata ku-regulate bei kiasi kwamba sasa hivi wananchi wanatoka maeneo mbalimbali kwa gharama nafuu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia inasaidia kuondoa… kuna rasilimali moja ambayo Watanzania wanaisahau, rasilimali muda. Sisi shughuli zetu zinapoteza muda mwingi sana kwa sababu ya kutumia muda mrefu kusafiri, lakini uwepo wa usafiri wa anga unarahisisha mambo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi ndugu zangu Wangoni hawa walizoea kushinda barabarani kutoka Dar es salaam kwenda mpaka Peramiho, lakini sasa hivi kwa uwepo wa bombardier ni saa moja anaruka kutoka Dar es Salaam kwenda Songea. Kwa hiyo, ninaomba sana tuimarishe shirika letu la ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.