Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ulanga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niweke rekodi sawa, jana katika Uwanja wetu wa Ndege wa Dar es Salaam ilitua ndege ambayo imeaminishwa kuwa ndiyo ndege kubwa kuliko zote kuwahi kutua. Nasema hapana, kwa sisi ambao tulikuwa wa kwanza kwenda Dar es Salaam, tarehe 06 Novemba, 2009 ilitua ndege aina ya Antonov An 225 ambayo ilileta mitambo ya Richmond, ndege hiyo ilikuwa na uzito wa tani 285 wakati iliyotua jana ina tani 276, hiyo ndege ilikuwa na urefu wa mita 84, ile iliyotua jana ilikuwa na mita 73; hiyo ndege ilikuwa na bawa lenye ukubwa wa mita 88, ile ina mita 80; hiyo ndege ilikuwa na injini sita, ile ya jana ina ijini nne; kwa hiyo tupo vizuri. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu la pili, kusifia sio unafiki, hata dini zetu zinatuambia unapotaka kuomba lazima usifie. Kwa sisi Wakristo unapotaka kumuomba Mungu unaanza Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe, ufalme wako ufike, utakalo lifanyike, sasa hapo swala ikishakolea unachomeka matatizo yako. Ndugu zangu Waislam tunasema Bismillah Rahman Raheem, Ewe Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, mwenye kurehemu, mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo; ukimaliza hapo unachomeka matatizo yako.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ndugu zangu, ninyi mkisimama mnaanza kukejeli Serikali, mnaitukana Serikali, mambo ya wapi hayo? Mimi sijawahi kumuona mtu anasema Mwenyezi Mungu ile mvua ya jana iliyonyesha ni mbaya imetuletea mafuriko, leo naomba hiki, mbona sijawahi kuona mkimwambia Mungu, kwa nini mnaikejeli Serikali?
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Lakini nimhakikishie sio kila neema anayoileta kwa Watanzania kuna watu wote wataifurahia, hata Mwenyezi Mungu neema anayotuletea sio wote wanaifurahia. Kwa mfano mvua inaponyesha ni neema kwa wakulima, lakini wauza mitumba, wamachinga wanachukia. Kwa hiyo, nataka nimwambie Mheshimiwa Rais hao wanaochukia neema anayoileta awachukulie sawasawa na wale wamachinga ambao wanaichukia mvua, aichukulie sawasawa na wauza mitumba ambao wanaichukia mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu hawana jema. Katika miradi yote ambayo imefanywa sijawahi kuona hata mradi mmoja ambao wanausifia, imeletwa reli wanalalamika, leo tunaanzisha mradi wa Stiegler’s Gorge wanalalamika, elimu bure mnalalamika, ununuzi wa ndege mnalalamika. Hebu waambieni Watanzania ni kitu gani chema kwenu ninyi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa maana yangu. Hiki kitabu mnachokiona cha hotuba ya Waziri, hii picha ya mbele sio Daraja la Ulaya wala sio Daraja la Kigamboni, ni daraja ambalo limejengwa katika Jimbo langu la Ulanga, daraja la kimataifa. Kwa hiyo, mnapoona ninyi mmepata ndege, mimi napata vitu kaa hivi, nimshukuru Mheshimiwa Rais, na tunalifungua wiki ijayo kwa hiyo vitu vinafanyika, tafuteni utaratibu mzuri wa kushauri na kuomba, mtavipata. Lakini tangu bajeti imeanza mnatukana matusi, sijaona mpinzani ameomba hata bomba la maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niishukuru Serikali kwa kutupa pesa kwa ajili ya ujenzi wa kilometa 68 za lami kutoka Kidatu mpaka Ifakara. Lakini ninachoomba watumalizie na kile kipande kingine toka Ifakara mpaka Mahenge.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kuunga mkono hoja, a luta continua.