Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza Serikali kwa miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea katika nchi hii. Licha ya pongezi hizo, kumekuwa na changamoto nyingi mno zinazoikabili Wizara hii nazo ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa bandari hususani Bandari ya Dar es Salaam ina changamoto kubwa ya ujenzi wa magati na kina kirefu cha maji. Yapata miaka kumi na zaidi Serikali inahangaikia changamoto ya upanuzi wa gati hizo (gati namba 7 hadi 13). Licha ya changamoto ya gati na changamoto zote zinazoikabili Bandari yetu ya Dar es Salaam kushindwa kushindana na bandari jirani, ni vema Serikali ikajitathmini upya miaka 10 au 20 baadae hii bandari itaelemewa kupita kiasi hivyo muda umefika sasa kuigeukia Bandari ya Bagamoyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bandari ya Bagamoyo ni bandari ya kimkakati, ni mbadala mzuri kabisa wa Bandari ya Dar es Salaam. Mchakato wa bandari hii ulianza muda mrefu sana tangu mwaka 2012 - 2018 haujakamilishwa hususani wa fidia kwa wananchi wa Kata ya Zinga. Mwekezaji yupo tayari kuanza kulipa fidia wananchi wa kata hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna minong’ono kwamba mwekezaji atakuwa tayari kuchukua na kufidia ndani ya hekta 3,000 ila Serikali inahitaji mwekezaji achukue hekta 9,000. Yeye ameshajipambanua atakuwa na uwezo wa hekta 3,000 sasa hekta 9,000 hazihitaji hizo zote ni nyingi mno yeye anahitaji hekta 3,000 aendelee na kazi hii habari ya hekta 9,000 tunaweka mkwamo usiokuwa na msingi. Mnakwamisha zoezi kwa kung’ang’ania hekta 9,000 badala ya hekta 3,000 alizozihitaji mwekezaji. Serikali ifike mahali imruhusu mwekezaji a-develop hekta 3,000 kama alivyoomba ili kurahisisha eneo la bandari kuwa wazi na wananchi kuanza kulipwa fidia zao haraka na miundombinu ya kijamii ihamishwe haraka kama shule na zahanati.
Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kutoa masikitiko yangu kwa Serikali. Inasikitisha sana watu hawajaondoka, hawajafidiwa, bado wanaishi pale lakini Serikali inaondoa wahudumu kwenye shule na zahanati ikiwa ni njia ya kushinikiza wananchi wapishe eneo la bandari. Watapisha vipi ilhali bado hawajafidiwa?Kibaya zaidi hiyo shule na zahanati zimejengwa kwa nguvu za wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kampuni ya Mawasiliano ya Simu (TTCL) ni Shirika la Umma ambalo linaushindani na mashirika ya simu ya binafsi (Tigo, Voda, Halotel na kadhalika). Shirika letu la umma lina madeni makubwa linadai taasisi na mashirika ya umma kitu kinachopelekea kushindwa kujiendesha na kushindana na mashirika binafsi. Hivyo ni vema wakalipwa madeni hayo ili wafanye kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi wa TAZARA wana madai ya muda mrefu ya malimbikizo ya mishahara, overtime na marupurupu yao. Ni vema Serikali izingatie suala la ulipaji madeni ya watumishi ili wafanye kazi kwa ufanisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na hilo deni la mishahara ya watumishi, pia TAZARA imekuwa inakabiliwa na changamoto ya sheria yake kupitwa na wakati na kutoenda na wakati ulipo. Suala la CEO wa TAZARA kwa sheria ya sasa ni lazima atoke Zambia jambo ambalo sio sawa kwa maendeleo ya reli yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwa mapungufu makubwa ya sheria hiyo hiyo kumekuwa hakuna condition juu ya masuala ya fedha, kitu ambacho mwaka huu wa fedha unaisha Serikali zote mbili Tanzania na Zambia tumetenga fedha za maendeleo shilingi bilioni 26; shilingi bilioni 16 toka vyanzo vya ndani vya TAZARA na shilingi bilioni 10 kutoka Serikali Kuu. Kwa upande wa Tanzania fedha hizo shilingi bilioni 10 tayari zimeshatolewa ila kwa wenzetu wa Zambia hadi hivi tunavyozungumza bado hazijatolewa. Sasa hapa tunaongelea maendeleo ya reli ya TAZARA, je, yanaafikiwaje kama upande wa Muungano mwingine wa reli hawatengi fedha hizo?
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana Serikali ilete mabadiliko ya sheria, sheria hiyo ya TAZARA ifanyiwe marekebisho na viwekwe vifungu vinavyoweza kuweka masharti juu ya masuala ya fedha kwa maendeleo ya reli yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.