Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kuipongeza Serikali kwa kazi wanayoifanya. Nilichangia kwa kuongea, sasa nataka kuongeza mchango wangu kwa maandishi. Niendelee kumpongeza Mkurugenzi wa TTCL, Mwenyekiti wa Bodi na watendaji wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kwamba Serikali ilipe madeni ya TTCL kwa sababu kuna Mashirika ya Umma na Taasisi za Serikali ambazo zina madeni makubwa na ya muda mrefu sana ili kampuni iweze kujiendesha kiushindani na Vodacom, Tigo, Airtel na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilikuja na mpango mkakati wa kuboresha Shirika la Posta. Je, mkakati huo umeishia wapi? Majengo yao yanahitaji ukarabati, vifaa vya kisasa vya kazi, pamoja na maslahi ya wafanyakazi. Nina imani kama Serikali itafanya maboresho, shirika hili litajiendesha kwa faida kwa sababu lilikuwa na mali za kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa Posta Kodi na Anwani za Makazi ni muhimu sana kwa Taifa letu, utasaidia uchumi wa nchi, utarahisisha kupeleka mizigo na utasaidia hata TRA kukusanya kodi za majengo. Mbaya zaidi mwaka 2016/2017 Serikali ilitenga shilingi bilioni tatu; zilizotolewa ni shilingi milioni 95 tu sawa na asilimia tatu; mwaka 2017/2018 zilitengwa shilingi bilioni tatu lakini Serikali haikutoa pesa yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali italeta sheria, kwani miundombinu katika vyombo vya usafiri inakuwa siyo rafiki kabisa na watu wenye ulemavu hawawezi kutoka point A kwenda point B, kwa sababu baiskeli yake haiwezi kupakia katika chombo cha usafiri. Bado hata baadhi ya majengo siyo rafiki kabisa kwa watu wenye ulemavu. Mfano, majengo ya huduma ya hospitali, vituo vya afya, mashule hata hili Jengo tu la Bunge pamoja na kufanyiwa ukarabati bado Wabunge wenye ulemavu hawawezi kuyafikia majengo yaliyopo katika maghorofa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kazi nzuri sana inayofanywa na Serikali yetu, lakini ni vema sasa deni la makandarasi na wahandisi washauri wa miradi ya barabara wakalipwa pesa yao ya shilingi bilioni 711.13.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kitengo cha TEMESA ni muhimu sana hasa Kitengo cha Ufundi (karakana). Ni kwa nini Serikali isiweke mkakati wa kuwa na vitendea kazi na ukarabati katika karakana za mikoa ili kitengo hiki kiweze kusaidia matengenezo ya magari yote ya Mashirika ya Umma na Taasisi za Serikali na iweke bei ambazo zingeweza kuvutia hata taasisi za watu binafsi ili waweze kutumia karakana hizo na kuweza kujiendesha kifaida kuliko ilivyo sasa kwamba karakana hizi huduma zake zimekuwa na bei kubwa sana?

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali kwa kuwashirikisha wanawake katika kazi za barabara kwa makandarasi wanawake. Ushauri wangu ni kwamba ni vema ushirikishwaji huo ungewekewa utaratibu wa kila Ofisi za TANROADS Mkoa kuendesha hayo mafunzo ya kuwajenga uwezo wanawake ili wanawake wote wapate fursa sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.