Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa mchango wangu kwa Wizara hii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Same Mashariki lina tatizo kubwa sana la usafirishwaji wa mazao pamoja na abiria. Jimbo la Same Mashariki limebarikiwa sana kuwa na mito mingi pamoja na mvua za kutosha. Kwa hiyo, wananchi wanalima sana mpunga, tangawizi, mahindi na ndizi. Pato kubwa la Halmashauri ya Same yanatoka Jimbo la Same Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Same - Kisiwani - Mkomazi ndiyo ilikuwa barabara kuu kutoka Nairobi – Arusha - Dar es salaam, yaani ilikuwa The great North Road. Kutokana na siasa za wakati wa miaka ya 1970’s zilizokuwa zinaendeshwa Wilayani Same (wakati huo ikiwa ni Wilaya moja na Wilaya ya Mwanga) ilisababishwa kuanzishwa barabara ya lami ya sasa kutoka Dar es Salaam kupitia Mkomazi – Bwiko – Hedaru – Makanya – Same – Moshi
– Arusha, matokeo yake wananchi wa Same, Kisiwani, Maore, Ndungu, Kihurio, Bendera, Mkomazi wakawa-cut off, maana usafiri wa mabasi uligeuza njia na kupitia njia mpya. Hili lilisababisha umaskini mkubwa kwa wananchi wa sehemu hii ya Same Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kuna miradi mikubwa ya Kitaifa inayoanzishwa Jimboni Same Mashariki. Miradi hii inaitikia wito wa Serikali wa kuanzisha viwanda. Miradi hiyo ni pamoja na LAPF, tayari wameagiza mashine ya kisasa ya kuchakata tangawizi. Tangawizi hii ina soko kubwa nchi za Uarabuni pamoja na Ulaya hasa Holland na Ufaransa. Wananchi kutoka Majimbo yanayopakana na Jimbo la Same Mashariki ambao pia wanatumia barabara hii ya Same Mashariki - Mkomazi yaani Majimbo ya Korogwe Vijijini, Mkinga, Mlalo na Same Magharibi ni kati ya wakulima wa Tangawizi ambao watafaidika na kiwanda hiki cha LAPF.
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Umoja wa Mataifa (United Nations Capital Development Fund-UNCDF) wamemaliza mchakato wa uanzishwaji wa mabwawa ya kisasa ya uzalishaji wa samaki ambao watatosheleza mahitaji ya ndani ya nchi na pia kusafirisha nchi za jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi mkubwa wa umwagiliaji katika Kata ya Ndungu ambao uligharamiwa na Serikali ya Japan. Mradi huu unazalisha mpunga mwingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nimeleta hiyo background ili niiombe Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ifikirie upya kutenga fedha za kutosha ili hii barabara ya Same –Kisiwani - Mkomazi itengenezwe yote kwa kiwango cha lami. Kiuchumi itaongeza pato la Taifa na kuhakikisha sustainability ya viwanda vinavyoanzishwa. Fedha iliyotengwa kwa barabara hii ni kidogo sana kiasi impact yake haitaonekana kimaendeleo. Zaidi ya hivyo, ijulikane kwamba Jimbo hili la Same Mashariki limekuwa marginalized kwa muda mrefu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hebu iangaliwe fedha iliyotengwa kwa Mkoa wa Kilimanjaro na kiasi kinachopelekwa Jimbo la Same Mashariki utaona Jimbo hili halitengewi haki. Kibaya zaidi, kiwango cha kutengeneza barabara hizi mbili yaani Same – Kisiwani - Mkomazi ina kilometa 96.46 na Mwembe – Myamba - Ndungu kilometa 90 kimekuwa cha chini sana. Wamekuwa wakirudia rudia maeneo yale yale siku zote na kukwepa kutengeneza maeneo korofi. Sehemu kubwa haijengwi mifereji na hata Makaravati huwa yanakuwa yakifukiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hisia kubwa kwa wananchi wa Jimbo la Same Mashariki kwamba kuna mchezo mchafu pamoja na ufisadi unaoendelea katika utengenezaji wa barabara hizi, ndiyo maana naona hata fedha nyingi zinatengwa kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wakati hakuna mpango wa kutengeneza barabara hii ya Same - Kisiwani - Mkomazi kwa kiwango cha lami. Inawezekana fedha hizi zinatumika kwa manufaa ya watu wachache.
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna sababu ya kupoteza fedha nyingi kwenye usanifu wakati hakuna nia ya kuiweka lami barabara hii ya Same – Kisiwani - Mkomazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.