Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Aeshi Khalfan Hilaly

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumbawanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, naamini dakika tano kwangu zitanitosha, nitaongea haraka haraka tu.
La kwanza, nikupongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wako kwa hotuba nzuri uliyotutolea, lakini kuna mambo matatu ambayo ningeomba utusaidie wakati ukija kutujibu hoja zetu. La kwanza, nimesikia kwamba Serikali itanunua mahindi tani laki moja mwaka huu, lakini naomba kujua Mheshimiwa Waziri, tunanunua mahindi lakini hatujataja bei tutanunua mahindi haya kwa bei gani? Ni vizuri mkawaeleza wananchi wakajua mahindi haya tutayanunua kwa shilingi ngapi ili wawe wanajua wasije wakauza mahindi yao, wakalanguliwa na walanguzi wengine kwa bei ya chini. (Makofi)
Kwa hiyo, ni vizuri utakapokuja hapa, uwatangazie wananchi hawa tutanunua mahindi tani laki moja, japokuwa ni ndogo, hazitoshi, lakini muwaambie wananchi hawa na wakulima kwamba tutanunua mahindi kwa bei kadhaa kama ilivyokuwa ikitokea siku za nyuma ambazo mlikuwa mkitusomea bajeti. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri ukija hapa utujibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, naomba kuchangia kwenye suala la mbolea. Nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake, lakini niseme kitu kidogo. Kuna mbolea aina ya Minjingu ambayo imekuwa ikipelekwa katika mikoa mbalimbali. Naomba, hebu lichukulie suala hili kwa umakini sana na kwa uzito. Naamini wataalam wako wanafahamu; kama kweli mbolea hii inafaa, basi naomba mlichukulie kwa uzito wa hali ya juu na kama haifai, njooni mtuambie hapa, hii mbolea haifai.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimkukumbushe tu Mheshimiwa Waziri, tulikuwa na mbolea ya aina nyingine ya DAP iliyokuwa inauzwa sh. 90,000/= mpaka sh.100,000/=, lakini kilipokuja Kiwanda cha Minjingu kuanza ku-supply mbolea hii, mbolea nyingine zote zikashuka bei. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, mbolea hii ya Minjingu, uende kiwandani, ukawatembelee, mje mtuambie kama mbolea hii inafaa. Kama inafaa, Serikali iongeze nguvu pale, kwa sababu hii ndiyo inaweza kusaidia kushusha mbolea nyingine zote ambazo zinatoka nje.
Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa kama kweli mbolea ya Minjingu inafaa na wataalam wako wanasema inafaa, basi tuipe kipaumbele sana tuweze kuwaangalia hawa na kuweza kuwasaidia kwa sababu kaulimbiu yetu ni ya viwanda na viwanda tulivyonavyo ni hivyo, tuanze navyo, tuweze kuvi-support. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, naomba nikiri hapa, mwaka 2015 makampuni mengi ya mbolea yalikataa kuikopesha Serikali mbolea, lakini wapo mawakala wadogo wadogo walioamua kwenda kuchukua mikopo benki wakaenda kununua mbolea ku-supply kwa wananchi lakini mpaka leo hawajalipwa. Mheshimiwa Waziri hebu, lichukulie hili, hawa mawakala ni wadogo, wamekopa fedha za riba, lakini mpaka leo mwezi wa Saba huu mawakala hawa hawajaweza kulipwa fedha zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, hawa mawakala mara nyingi wanakuwa wakituokoa sana; hawa wakubwa wanapogoma, mawakala wadogo wanaweza wakatusaidia, nasi tuwaone!
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, ni suala la uvuvi. Naomba nizungumzie uvuvi kidogo kwa sababu nimebakiwa na dakika tatu. Mheshimiwa Waziri wavuvi hawa wanaumizwa sana. Leseni zimekuwa za kila aina! Ukimwangalia mwenye mtumbwi, anachajiwa leseni, mwenye wavu anachajiwa leseni, mvuvi mmojammoja anaachajiwa leseni, akivua tena dagaa hizo hizo leseni, akisafirisha Dar es Salaam leseni. Hebu angalieni hili Mheshimiwa Waziri mfute hizi leseni maana yake kodi zimekuwa nyingi mno kwa mtu mmoja. Kwa hiyo, tumekuwa tukiwaonea sana wavuvi bila kuangalia ni jinsi gani wanavyoteseka katika uvuvi kwa wanaokwenda huko kwenye shughuli za kujitafutia maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siongei mengi, nilitaka kukumbusha tu haya machache ambayo nimeona kwamba Mheshimiwa Waziri anapokuja kutujibu atuambie, suala la bei ya mahindi, atuambie mbolea ya Minjingu kama inafaa, lakini vilevile atuambie mawakala hawa wataweza kulipwa lini fedha zao?
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, naunga mkono hoja. Ahsante.