Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wote wawili wa Wizara na uongozi mzima wa Wizara hii kwa hotuba yao nzuri ambayo imejikita zaidi katika kuhakikisha kuwa sekta ya ujenzi (barabara), mawasiliano na usafiri wa maji unasimama vema. Niipongeze sana Serikali kwa kuweka kipaumbele barabara ya Handeni - Kibereshi - Kijungu - Kibaya - Mjaro - Olbolotiri - Singida kilometa 460. Kujenga kwa kiwango cha lami barabara hii ukiacha kwamba bomba la mafuta kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga bado barabara hii ni muhimu kwa shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa mikoa hii minne (Tanga, Manyara, Dodoma na Singida).

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wananchi wa mikoa hii mimi naamini kabisa barabara hii itasaidia kufungua fursa nyingi za kiuchumi, niombe sasa Serikali ifanye jitihada kubwa kupata fedha za kutosha ili barabara yote iongezwe kilometa 460. Barabara hii ina faida kubwa hata kwa wafanyabiashara wa nchi jirani, mfano Burundi, Rwanda na Uganda. Bandari zikishakarabatiwa wafanyabiashara watanufaika kwa punguzo la gharama za usafiri kwa sababu barabara hii kwa kiasi kikubwa itakuwa fupi.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ningependa kuchangia ni ubora wa kazi za ukarabati, ujenzi wa barabara zetu kwamba baadhi ya wakandarasi wanapopewa zabuni za barabara matengenezo ya barabara yapo chini ya kiwango. Naomba sana tena TANROADS wasimamie kwani Serikali inapoteza fedha nyingi kwa kazi zinafanyika chini ya kiwango. Kwa mfano ukarabati wa barabara ya Handeni – Kibarashi – Sange baadhi ya maeneo vifusi vilivyomwagwa vilikuwa ni vumbi badala ya kuweka vifusi vyenye mawe hasa katika maeneo ya Korosi. Hii imesababisha barabara hii kutopitika kwa takribani siku tano; mimi najiuliza kwa nini viwango vya kazi hivi kusimamia? Jambo hili litazamwe kwa jicho la karibu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu pia naomba uende kwenye Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (USCAF) mfuko huu ni muhimu sana hususani kwenye maeneo yenye changamoto za mawasiliano kama katika jimbo langu la Kilindi. Nipongeze jitahada zilizofanywa na mfuko kwa kupitia maeneo yote yenye uhaba wa mawasiliano ya simu, nimeona orodha ya vijiji na kata ikiwemo eneo langu la Kilindi niombe maeneo yote yapatiwe mawasiliano ukizingatia mawasiliano ni ajira pia maeneo hayo ni Kata ya Sanyi, Kata ya Kilwa - Kijiji cha Kilwa, Kata ya Twande - Kijiji cha lwande, Kata ya Tunguli, Kata ya Kwekivu, Kata ya Kilindi asilia Kijiji cha Misufini Kata ya Masagalu na vijiji vyake vyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho lakini si kwa umuhimu ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga barabara ya lami ya kwa kilometa tano kwa kiwango cha lami, napongeza, jitihada za ujenzi zimeanza lakini kiasi kilichotengwa ni kidogo sana, ni motor zoo tu ndio zimeanza kujengwa. Niombe Wizara itenge fedha za kutosha kuhakikisha ahadi hii ya Rais wetu inatekelezwa naamini kabisa umuhimu wa kujengwa kilometa tano hizi zitasaidia kupandisha hadhi ya mji wetu wa makao ya Wilaya (Songe) na kubadilisha mwelekeo pia na mwisho barabara zote zinazosimamiwa na TANROADS, wakandarasi wahakikishe mitaro yote inayopitisha maji pembeni mwa barabara zetu inakarabatiwa na kusafishwa mara kwa mara ili kulinda barabara zetu. Naunga mkono hoja.