Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Tanga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na kuweza kuchangia Wizara hii muhimu katika nyanja mbalimbali za maendeleo, hususan katika uchumi, mawasiliano na usafiri wa anga, baharini, reli na barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Pangani ni kongwe na ya kimkakati (East Africa and Southern Roads Projects). Barabara hii kama itajengwa kwa kiwango cha lami itainua hali ya uchumi wa Mikoa na Majimbo ya Tanga, Muheza, Pangani, Bagamoyo na maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, mwaka jana barabara hii ilitengewa shilingi bilioni nne, naomba ziongezwe na barabara tuambiwe itaanza kujengwa lini? Barabara hii ni ya kihistoria na tayari ilishaahidiwa na Marais wanne waliopita akianzia Mheshimiwa Mwalimu Nyerere, Mheshimiwa Ally H. Mwinyi,
Mheshimiwa Benjamin Mkapa na Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwanja wa ndege wa Tanga ni wa kizamani lakini tangu umeachiliwa na wakoloni haujafanyiwa ukarabati mkubwa wa maana. Nimezungumza katika bajeti mwaka 2016/2017, 2017/2018 na leo hii 2018/2019 nimeona shilingi bilioni 7.6; naomba fedha hizi zifanye kazi ya kubadili sura na hali ya uwanja, pia nataka nijue fedha hizi ni pamoja na fidia ya nyumba tatu zilizofanyiwa tathmini (evaluation) 2008 na nyumba 802 ambazo nazo zinatakiwa kubomolewa, zote hizi naomba wamiliki wake wafidiwe kuepuka mgogoro unaoweza kusababisha kesi mahakamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali kufuatia miradi mikubwa ya bomba la mafuta toka Hoima - Uganda hadi Chongoleani - Tanga viwanda vya saruji vipya vya Kilimanjaro na Sinoma China chenye thamani ya shilingi trilioni saba. Naomba Tanga tujengewe uwanja wa ndege wa kisasa wa Kimataifa. Naomba pia huduma za bombadier kupitia ATCL zifike Tanga kwa kuwa Tanga kuna shughuli nyingi za kiuchumi, ukiwemo utalii, viwanda, uvuvi na bandari.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia mipaka ya uwanja wa ndege wa Tanga iwekwe wazi na Waziri utaje vipimo vyake kwa kuwa kuna mgogoro ambao unasumbua wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirikia la Ndege ATCL pamoja na ununuzi wa ndege sita, lakini naiomba Serikali inunue ndege tano na fedha za ndege mbili zinunue ambulance, helicopter mbili ambazo zitasaidia kuokoa maisha ya wananchi wetu pindi zinapotokea ajali barabarani au katika vyombo vya usafiri. Ndege hizi zipatiwe routes za nje na ndani ili shirika lijiendeshe kwa faida na lisijiendeshe kwa hasara kama ilivyokuwa Air Tanzania. Shirika letu la ndege liajiri wataalamu na watumishi wenye weledi na ubunifu ili kuweza kufanya competition na mashirika mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, reli ya standard gauge katika bajeti ya mwaka 2017/2018 nililieleza Bunge na Serikali kuwa reli ya Tanganyika ilianza kujengwa mnamo mwaka 1905 ikianzia bandari ya Tanga hadi Kilimanjaro, Kigoma na hatimaye kufika Mwanza. Baada ya kuja standard gauge Tanga imeachwa, nashauri kama wasemavyo wanafalsafa kuwa mwiba unapoingilia hutokea hapo hapo, hivyo naomba standard gauge ifike Tanga ili uchumi wa Tanga nao uweze kukua kwa kasi kwani uchumi wa Tanga unategemea reli, barabara, bahari na anga.
Mheshimiwa Naibu Spika, bandari ya Tanga ni miongoni mwa bandari kubwa nne za Tanzania (Dar es Salaam, Tanga, Zanzibar na Mtwara) na kihistoria bandari ya Tanga ndiyo ya kwanza katika East Africa. Katika enzi za sayansi na teknolojia, bandari ni lango kuu la biashara, lakini bandari zetu zilizoko katika Bahari ya Hindi hazitumiki vizuri, ukilinganisha na bandari moja ya Mombasa nchini Kenya. Serikali yetu imeelekeza shughuli nyingi katika bandari ya Dar es Salaam na zingine za Tanga na Mtwara hazitumiki vizuri na kusababisha kujiendesha kihasara.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto katika bandari ya Tanga tarehe 28 Februari, 2018 nilialikwa katika kikao cha Bodi ya Bandari na wadau wa bandari, wafanyabiashara, wajasiriamali na kadhalika. Katika kikao hiki zilizungumziwa changamoto nyingi zikiwemo ukosefu wa zana mkononi, hakuna cranes za kubeba kontena za 40 fts, magari ya kutosha, urasimu ni mkubwa, pamoja na udokozi katika bidhaa zinazoingizwa toka nje, kina cha bandari ni kifupi, meli haziwezi kukaa longside na kusababisha gharama kubwa katika ushushaji mizigo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali bandari ya Tanga ipatiwe vifaa vya kisasa kama cranes, matishari, malori, fire department, waletwe watumishi wenye kujituma kuondoa urasimu, wazalendo/weledi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali ianzishe categories za mizigo ambapo kila bandari ingepangiwa utaratibu wa kupokea na kusafirisha mizigo kama ifuatavyo; Bandari ya Tanga ingepokea ama kusafirisha mizigo ya Arusha, Kilimanjaro, Simanjiro, Manyara, Musoma, Bukoba, nchi za nje, Uganda, Rwanda, Burundi na Congo DRC. Bandari ya Mtwara ingepokea ama kusafirisha mizigo ya Mtwara, Ruvuma, Mbeya, Katavi, Rukwa, Sumbawanga, Kigoma na Tabora, nchi za nje mizigo ya Malawi, Zambia, Zimbabwe na Mozambique na Bandari ya Dar es Salaam ingepokea ama kusafirisha mizigo ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora na Mwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nchi za nje mamlaka ikiona ipo haja baadhi mizigo ya baadhi ya nchi zipitie Dar es Salaam lengo kuu liwe bandari zote zifanye kazi kwa kiwango kinachofanana na faida.
Mheshimiwa Naibu Spika, wito wangu ni kuwa together we build our nation.