Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Silafu Jumbe Maufi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa pongezi kubwa ya dhati kwa kazi nzuri chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, bila kusahau kwa Waziri mwenye dhamana wa Wizara hii pamoja na Naibu Mawaziri kwa kushirikiana na wataalam, watumishi kwa ujumla wa timu hii imefanya kazi nzuri kwa nchi yetu na kwamba wametutendea haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na mawasiliano kwa mitandao kadhaa na yote yanatoa huduma ya kibenki, lakini mtandao wa Vodacom – Mpesa kumekuwa na wizi wa fedha, mteja akikosea namba akiwa ametuma fedha akitoa taarifa Vodacom jibu kuwa fedha hizo zimekwishatolewa na mhusika hana salio hivyo hesabu maumivu tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali hii ni wizi kwani hawezi kufuatiliwa huyo mhusika anapokuwa na fedha hiyo basi irejeshwe kwa mteja aliyetoa taarifa, kuliko kumjibu hivyo au kwenda kuripoti polisi. Ni vema Wizara kuingilia kati kwani wakati mwingine ni pesa ya ada kwa wanafunzi vyuoni, kwa majibu hayo, hivyo mwanafunzi hatasoma chuo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mawasiliano ni muhimu kwani ni kiunganishi madhubuti kwa wananchi wetu hasa waliopo mipakani kuwa na mitandao yenye mitambo mikubwa kwa kuwa huwa wanaingiliana na mitandao ya nchi jirani hasa Zambia na Bujumbura. Mfano; Kata ya Kala, Kata ya Wampembe, kata ya Mambwenkoswe (Rukwa), mitandao inayumba. Tunaomba Wizara kuangalia mawasiliano kwa mikoa ya pembezoni, Bonde la Tanganyika na Bonde la Rukwa kuwa na mawasiliano kamili kuanzia milimani tuteremkapo bondeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejitahidi sana katika kuiunganisha nchi yetu, lakini wananchi wetu asilimia kubwa na wazalishaji wakuu hawana barabara (vijijini) na sasa na TARURA asilimia 30, hatutakuwa tumetenda haki kwa maendeleo ya uchumi wa viwanda, hivyo ni bora wakati huu tukachukua maamuzi magumu ya kuwapa asilimia kubwa TARURA. Tuwaunganishe wazalishaji hawa tusonge mbele kwenye azma ya maendeleo ya nchi hii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa msemaji wa kila mara katika Bunge hili kuhusu na barabara zinazoteremka kwenye mabonde ya Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa kwa sasa zimefikia mwisho wa kuendelea kuwa za changarawe/ udongo au kuweka viraka vya sementi na matengenezo ya maeneo korofi haya mara kwa mara kwa sasa basi. Tunaomba Serikali kuzingatia na kuzitengeneza kwa kiwango cha lami kama Milima ya Kitongo na Nyang’oro kuliko kuendelea kupanga bajeti kila mwaka kama 2018/2019 kwa kilometa 108.0 shilingi milioni 3,315.852 na kadhalika. Tuziangalie kwa huruma tupo pembezoni, tumechelewa kimaendeleo pamoja uzalishaji mkubwa wa chakula na biashara kwa ndani ya nchi na nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, bila kusahau barabara ya Kibaoni (Katavi) hadi Kilyamatundu – Miangalua (Rukwa), ukifahamu Serikali inajenga daraja kubwa la Mamba (Rukwa/ Songwe) halafu barabara zake changarawe/udongo hali hii ngumu na haiwezekani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali na Wizara kiutalaam wana haja ya kuinua Shirika la TTCL na kuweza kujiendesha, basi ni bora kuhakikisha kwa kuliwezesha kusambaa nchi nzima na vifurushi vyao kuwa rafiki kwa wananchi wetu, pamoja na simu zao kuwa na uwezo wa huduma zote za kimtandao kwa bei nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mawasiliano ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi, na Serikali tusiendelee kuingizamitandao kutoka nje, naomba nguvu kubwa tuelekeze TTCL iweze kusimama na tujivunie shirika letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.