Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Lucy Fidelis Owenya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara iliyopo Mkoa wa Kilimanjaro Wilaya ya Moshi, Kata ya Old Moshi Mashariki kuanzia Kiboriloni – Kikarara – Tsudini mpaka Lango la Mlima Kilimanjaro, barabara hii ilikuwa ahadi ya Mheshimiwa Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete na baadae kupewa ahadi na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli. Ni zaidi ya miaka 10 imekuwa ikitengewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa lami lakini mpaka leo inafanyiwa upembuzi yakinifu. Je, zoezi hili linachukua muda gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ile kwa umuhimu wake kwenye sekta ya utalii ambayo Wizara ya Maliasili inaifanya njia ya Old Moshi kwa ajili ya watu mashuhuri lakini cha kusikitisha barabara ile imeharibika sana, haipitiki kabisa. Kinachoonekana kule ni vibao vya TANROADS vinavyoashiria wataanza kutengeneza lakini hakuna kinachoendelea!

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inahamia Dodoma rasmi lakini bado kuna Wizara pamoja baadhi ya barabara zipo TARURA sababu hapa ndiyo kioo cha nchi yetu ni lazima tuanze kuwa na mipango ya kuhakikisha barabara zote zinapitika kwa lami na kuwepo na njia za ring roads ili kuzuia msongamano, la sivyo, kile kichefuchefu cha foleni ya Dar es Salaam kitahamia Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwanja wa ndege uliopo Moshi umesahaulika kabisa, kwa sasa uwanja ule wananchi wanautumia kwa ajili ya kilimo cha maharage. Uwanja ule upo very strategic kwa ajili ya kukuza utalii, unaweza kutumika kwa dharura, pia kutumika kwa ajili ya ndege ndogo kupeleka watalii Serengeti National Park baada ya kupanda mlima. Je, Serikali ina mikakati gani ya kukikarabati au kukifufua kiwanja cha ndege cha Moshi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu karakana iliyopo Kilimanjaro International Airport, karakana hii ipo pale KIA lakini haitumiki ipasavyo, ingeweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuongeza fedha za kigeni. Ndege kutoka nchi jirani zingeweza kuja pale na kufanya service, kupiga rangi na kadhalika, lakini Serikali haioneshi nia ya dhati ya kukarabati karakana ile. Je, ni lini Serikali itaanza ukarabati katika karakana ya KIA ili iweze kuchangia katika Pato la Taifa?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu TAMESA, nia ya kujenga TAMESA kila Mkoa ilikuwa ni njia mojawapo ya kupunguza matumizi kwenye magari ya Serikali na magari yote ya Serikali yatengenezewe kule na kufanyiwa service kule, lakini karakana hizo vipuri vyake vimepitwa na wakati na magari yaliyopo sasa ni automatic na teknolojia mpya, badala yake TAMESA inatumika kuegesha magari ya Serikali yasiyofanya kazi kabisa na kwa sasa gari ya Serikali inapelekwa TAMESA halafu TAMESA wanawapa kibali kwenda kutengeneza au kufanya service kwenye garages za watu binafsi. Hii inasababisha Serikali kuwa na madeni makubwa sababu kule private malipo huwa zaidi ya hata mara mbili na sababu ni kwamba pia Serikali inachukua muda mrefu kuwalipa madai yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kujua Serikali ina mikakati au mipango gani ya kuhakikisha inaweka teknolojia ya kisasa katika karakana zote sababu miundombinu ipo ili magari ya Serikali sasa yaanze kutengenezewa TAMESA hatimaye kupunguza gharama kwa Serikali?

Mheshimiwa Naibu Spika, nyumba nyingi za TBA zipo katika hali mbaya sana, mfano hapa Dodoma, nyumba zilizokuwa chini ya CDA ni mbovu kupita kiasi na Serikali imewapangia wafanyakazi wanaohamia hapa kuishi kule. Naiomba Serikali itambue wafanyakazi hawa walitoka majumbani kwao, nyumba zenye hadhi leo hii TBA mnawapangia nyumba ambazo bado hamjazikarabati kabisa? Majengo mengi yamefubaa hakuna sababu ya kuyabomoa lakini wakarabati ili kuwepo na kumbukumbu ya majengo hayo kwa vizazi vijavyo kujua Dodoma kabla ya Makao Makuu kuhamia Dodoma ilikuaje. Historia ni muhimu sana.