Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Devotha Methew Minja

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Naomba na mimi nichangie mawili, matatu kwa dakika hizi tano ambazo umenipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwa uzito wa bajeti hii ya kilimo ambayo tunafahamu pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 70 inategemea kilimo. Ninachokiona katika kujadili bajeti hii, wakulima na wafugaji hawajui ni nini tunachojadili, ikizingatiwa kwamba changamoto ni nyingi katika sekta hii. Nafikiri, hatuzungumzii habari ya televisheni tu, tunazungumzia pia habari ya redio. Mkulima anapaswa akiwa shamba leo hii ajue mpango wa Serikali wa kununua maelfu ya tani za mahindi; mkulima ajue kwamba ni kiasi gani cha fedha kimetengwa kwa ajili ya kusaidia pembejeo, lakini leo hii tunawanyima fursa wakulima hawa kujua wakati tunakabiliwa na matatizo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo suala tu la kusikiliza redio mkulima akiwa analima, watu wako kwenye bodaboda wanasikiliza redio, wako kwenye daladala wanasikiliza redio, wanajua ni nini hatma ya sekta hii muhimu ambayo inachangia pato zaidi ya asilimia 70.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji katika Mkoa wa Morogoro. Hivi karibuni Waziri wa Kilimo alifika Mkoani Morogoro; mauaji makubwa yametokea, wananchi wameuawa, mifugo imeuawa, lakini hatma ya kutatua migogoro hii kule Mvomero wameamua kujenga korongo la kilometa 13 linalogharimu shilingi milioni 147, lenye urefu wa futi zaidi ya sita kwenda chini, upana zaidi ya ekari moja kutenganisha wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi shilingi milioni 147 zingejenga Zahanati mbili, zingejenga malambo matatu ambayo yangesaidia wananchi hawa ambao migogoro yao mikubwa ni kutokana na kukosa vitu muhimu ikiwemo haya malambo. Leo tumeamua kuanza kuwagawa Watanzania hawa badala ya kutafuta suluhu ya kudumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, enzi za Mwalimu Nyerere migogoro hii haikuwepo, lakini hivi sasa watu wamehodhi maeneo makubwa, wakulima hawana sehemu ya kulima, ranchi zilizokuwa za Serikali zimehodhiwa, Serikali ilitoa maamuzi kwamba zaidi ya ekari 5,000 zigawiwe wananchi hawa lakini hakuna kitu, wamegawana vigogo, sasa hivi wanakuja kuamua kuwatenga wakulima na wafugaji. Sijui tunakwenda wapi katika Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Berlin wameamua kuvunja ukuta ili kuwaunganisha watu, leo sisi tunasema tunajenga korongo kumtenganisha mkulima na mfugaji! Watu hawaombani chumvi, hawaombani kibiriti! Shule wanafunzi wanashindwa kuvuka upande wa pili! Naongea kwa masikitiko makubwa; wananchi hawa wangejengewa mikakati ya kutatua migogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwigulu alifika pale, wananchi wanamnyooshea vidole Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa, RPC, DC, migogoro inatokea hawana habari kinachoendelea, matokeo yake Mahakama ilitoa rulling kutengeneza buffer zone Halmashauri/Serikali iliamua kujenga korongo kwamba sasa korongo litengenezewe. Hata mipaka ya nchi zetu, hakuna makorongo. Inasikitisha sana! Fedha hizo ambazo ni mapato ya wananchi ambayo yangesaidia lakini sasa hivi yanakwenda kutengeneza makorongo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, korongo hili halikuzingatia hata ushauri wa Madiwani wala NEMC zaidi ya kuharibu mazingira. Kwa hiyo, naomba Serikali ifikirie upya jinsi ya kusaidia jamii hizi kurudisha utamaduni.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na siungi mkono hoja.