Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye hoja hii muhimu na nianze kwa kuunga mkono hoja. Niitumie nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa sbabau naongea kwa mara ya kwanza kutoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo yaliyojitokeza namshukuru sana Mungu kwa nafasi hii lakini nimshukuru kipekee Mheshimiwa Rais kunipa nafasi, kuniamini niweze kumsaidia Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru wewe, nimshukuru Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge maalum niishukuru Kamati tumefanyakazi nayo, tumepokea ushauri wa Kamati na wameendelea kutuboresha katika utendaji wa kazi kwahiyo Mheshimiwa Kakoso pamoja na timu ya Kamati nzima nawashukuru sana.

Nitoe shukrani kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwa sababu mara zote tumepata ushauri wao, tumepata mijadala mbalimbali tukiwa ndani ya Bunge na nje ya Bunge kwa hiyo, Wabunge tunawashukuru ushauri wenu, maneno yenu kwa kiasi kikubwa yametusaidia kufanya shughuli zetu, lakini pia niwashukuru wapiga kura wa Jimbo la Ushetu muda mwingi kabla ya nafasi hii nimekuwa na muda mwingi wa kuwepo Jimboni, lakini sasa wananikosa na niishukuru pia familia yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka niseme kwamba bajeti hii katika sekta ya ujenzi peke yake imechangiwa kwa kuzungumza hapa zaidi ya wachangiaji 95 na zaidi ya wachangiaji 50 wamechangia kwa maandishi. Niseme tu Katibu Mkuu na timu yake wanaendelea kukamilisha kabrasha la majibu kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge mtayapata na mtaona namna Serikali kupitia Wizara hii inavyochukua hatua mbalimbali kuweza kutekeleza na saa nyingine kuona namna mambo ambayo yamefanyika kupitia pia michango ya kwenu kwa hiyo msiwe na wasiwasi mtapata.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii, niseme tu kwa ufupi sana nilitaka nitoe na ufafanuzi kidogo kwenye hali ya mtandao wa barabara nchini ili angalau tuwe na picha ya pamoja. Ukiisoma sheria yetu ya barabara hasa hasa ile section ya 12 inatoa mchanganuo wa aina za barabara. Sasa nilitaka nizungumze sambamba ili tuone pia jukumu lililopo kwenye Wizara, lakini jukumu pia ambalo lipo kwa upande wa wenzetu TARURA ili tuone tukifanya mchanganuo pale inaweza ikatupa picha kwamba michango mingi ya Waheshimiwa Wabunge imezungumza juu ya namna TARURA iwezeshwe zaidi ni kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka niseme tu kwamba kwa upande wa barabara kuu, tukizungumza barabara kuu tunazungumza juu ya barabara ambazo zinaunganisha Makao Makuu ya Mikoa lakini pia barabara ambazo zinaunganisha Makao Makuu ya Mikoa pamoja na majiji au inaunga nchi za nje ambapo kwa sasa tuna barabara zenye ukubwa wa zaidi ya kilometa 12,000 hivi. Lakini tukizungumza barabara zile za Mikoa tunazungumza juu ya barabara ambazo zinatoka kwenye Makao Makuu ya Mikoa zinaunga barabaa kuu.

Lakini barabara pia za Makao Makuu ya Wilaya na Makao Makuu ya Mikoa na hizi sasa kwa ukubwa tunazo kilometa yapata zaidi ya 23,000 sasa utaona kwa upande wa barabara kuu sehemu ambazo sasa zina kiwango cha lami ni zaidi ya kilometa 8,000 na zile ambazo ziko kwenye matengenezo na hata Waziri Mkuu akiwasilisha hapa, kilometa zaidi ya 1,700 ziko kwenye hatua mbalimbali. Sasa ukijaribu kupima utaona upande wa barabara kuu karibu sehemu kubwa tunaunganisha na Kamati imetoa ushauri tumeuzingatia na utaona Mikoa michache ambayo harakati zinaendelea katika hatua mbalimbali kuziunganisha ikiwemo maeneo ambayo yamebakia kama barabara kubwa ikitoka Mkiwa ukipita Itigi kwenda Mbeya, iko barabara kubwa ukitoka Morogoro sasa tunajenga Kidatu kwenda Ifakara lakini ukitoka Ifakara - Lupilo - Malinyi - Londo - Kilosa kwa Mpepo tunakwenda kutoka kule Namtumbo na hiyo barabara harakati zinaendelea vizuri. Kwa hiyo, ziko barabara zingine, barabara ya Mheshimiwa Chenge wakati akichangia jana alizungumza juu ya barabara ambayo itakuwa ikitoka Lalago kuja Sibiti na pale Sibiti tutakuwa na route mbili, moja itapita Eyasi kwenda Karatu, lakini nyingine itapita Mkalama itakwenda Haydom - Katesh - Mbulu Mjini itakwenda hadi Karatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na hii ni barabara muhimu sana kwa sababu itaunganisha Mikoa kwa maana ya Simiyu, kwa maana ya Shinyanga, Mwanza, Singida na baadae tutakuwa na vipande vichache ambavyo vitaunganisha ukitoka Singida Mjini kwenda Mkalama, lakini ukitoka Singida Mjini kwenda Haydom. Kwa hiyo, unaona kwamba muunganiko wa barabara nchi nzima unakwenda vizuri na wale ndugu zangu wa Kigoma, maeneo ambayo yalikuwa yamebakia yako kwenye hatua nzuri kwa maana tutaiunganisha barabara kutoka Nyakanazi kuja Kibondo, unakuja Kidahwe mpaka Kigoma Mjini pamoja na matawi yanayounganisha nchi za jirani kwa maana sasa tunakwenda vizuri. Kwa hiyo, karibu maeneo mengi yanaunganishwa na hii ni itakuwa inatupa fursa kwenda kuunganisha barabara hizi ambazo tunaziita barabara za Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa maana hizi barabara za Wilaya ni barabara ambazo zinaunganisha Tarafa, makao Makuu ya tarafa na tarafa zingine, inaunganisha pia makao makuu ya kata na tarafa, inaunganisha pia kutoka kwenye kata na kwenda vijijini lakini pia na barabara za mitaa. Kwa maana hiyo sasa utaona kazi ambayo inafanyika na TARURA sasa hivi ni kufanya tathmini ya hali halisi ya ukubwa na mtandao wa barabara zetu kote nchini na hili zoezi linafanyika vizuri, liko hatua za mwisho sasa wanaendelea kuhakiki, zitakuwa na roughly na takribani kilometa 108,000. Sasa baada ya kukamilisha hiyo itatuwezesha sasa katika kupanga rasilimali hii kwa ajili ya uboreshaji wa barabara ili sasa tuje kuwa na mgao mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niwahakikishie Wabunge na Bunge lako tukufu kazi kubwa inafanyika, ujio wa TARURA ni mkombozi kuhakikisha sasa uwiano wa barabara za kwetu unapata fedha vizuri na tunaendelea pia kuunganisha maeneo yaliyobakia ya nchi yetu pamoja na nchi za jirani. Ukiona hivi karibuni kuna mkataba umesainiwa pia ukitoka kule Mbinga kwenda Mbamba Bay, mkandarasi yuko site, lakini tunaunganisha na wenzetu upande wa Msumbiji naona Mheshimiwa Chief Whip wa kwetu hapa anazungumza, tutatoka Likuifusi tutakwenda Mkenda na tukitoka Mkenda tutarudi Tingi ili tuunganishe na barabara kubwa inayotoka kule Mbamba Bay lakini kule Mbamba Bay tutaunga na nchi za jirani pamoja na wenzetu wa Mbeya kwa maana ya ujenzi wa meli, lakini pia barabara nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitoka pale Kitai ukienda Ruhuhu ziko kilometta 139 mwambao wa Ziwa Nyasa tunakwenda kuziboresha ili wananchi wa Ludewa waweze kwenda Kyela na kwenda Mbeya kwa wenzetu kule kwa maana muunganiko nilitaka nitoe mfano kwa maeneo machache muone namna Serikali inafanya juhudi ya kuunganisha Mikoa, lakini pia kutekeleza sera ambayo inataka tuanze kuunga Mikoa, tuunge na wenzetu wa nchi za nje ili tuweze kufungua fursa kwa sababu barabara pia itachangia katika maendeleo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka niseme tu kwamba kitabu hiki cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri kimezungumza mambo mengi na niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge tusome. Barabara zimeanishwa vizuri, saa nyingine ninataka niseme hivyo kwa sababu yako maeneo ambayo tumetaja kwa mfano, uboreshaji wa miundombinu katika Jiji la Dar es salaam na upande wa Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kwamba wananchi wanahitaji wachangie katika uchumi wasikae muda mwingi barabarani ndiyo maana utaona nilikuwa nimejaribu kuonesha hapa maana yake nilishangaa juzi wakati Mheshimiwa Kubenea akichangia alisoma jedwali ila hakusoma kama Mheshimiwa Tambwe alizungumza hapa, alisoma jedwali akasema kuna barabara hewa nikaanza kushangaa nikitambua kwamba Mheshimiwa Kubenea ni mwandishi na nafikiri anahitaji kuwa makini zaidi ili saa nyingine ukizungumza jambo ulizungumze ukiwa na uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukianda ukurasa wa 20 kama Mheshimiwa Tambwe alivyozungumza, Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake amesema wazi barabara ile ya Nzega - Puge - Tabora imetengewa fedha kwa ajili ya kumlipa mkandarasi, lakini yeye alisema kuna barabara hewa ambayo imekamilika na imetengewa fedha sasa hiyo siyo sahihi nilitaka niweke kumbukumbu sawa. Ni kwamba barabara zimeainishwa vizuri na mipango imeapangwa vizuri kwahiyo nilikuwa napenda Waheshimiwa Wabunge tukipitia tutaona.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nitoe mfano kwa upande huu wa barabara za Dar es Salaam, mtandao wa barabara ambao utakwenda kupunguza msongamano utakuwa na urefu wa kilometa 156 lakini ziko barabara ukitoka Tegeta tutakuwa tunakuja Mbezi sasa tunaendelea na usanifu, kutakuwa na barabara ambazo zitakuwa na njia sita. Lakini pia ukitoka Mbezi mwisho kwenda Pugu tunaendelea kufanya usanifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilitaka tu niseme kwa ufupi kwa sababu ya muda yako maelezo mazuri sana ukienda ukurasa wa 17 hadi ukurasa wa 21 tutaona namna tulivyojipanga ili kufanya mtandao wa barabara katika Jiji la Dar es salaam lakini pia upande wa Dodoma tumelitazama. Upande wa Dodoma tumejipanga kwa sababu ya uzoefu wa conjection katika Jiji la Dar es Salaam tumejipanga vizuri. Ziko barabara ambazo zimetajwa katika kitabu hiki utaona kuna barabara za mzunguko zina kilometa 104; lakini ziko pia barabara za ndani ambazo tutaziboresha ili Waheshimiwa Wabunge na wananchi wa Dodoma kwa ujumla waweze kupita na kufika katika maeneo yao na kuchangia katika uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naona nitazama kwa sababu ya muda, sasa naomba nimalizie tu kwa kushukuru kwa nafasi hii lakini niwaombe Wabunge tu hata baada ya kikao tuweze kubadilishana mawazo hii nchi ni ya kwetu wote, kama kuna mawazo sisi kama Serikali tunayachukua kwa ajili ya kuyaboresha, muda wote tuzungumze, tubadilishane mawazo ili tuweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana.