Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Khamis Yahya Machano

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chaani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. KHAMIS YAHYA MACHANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia siku njema. Pia nachukua nafasi hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kuwasilisha bajeti yao leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo kama matatu ambayo nitayazungumza kwa sababu leo siku ya Ijumaa. Jambo la kwanza ambalo nitaanza kuzungumzia ni kuhusu TBC. Kwa upande wa TV nawapongeza sana kwamba wako makini na wanaonekana karibu katika nchi nzima. Kwa TBC Radio hasa kwa upande wa Zanzibar, usikivu wake ni mdogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri ajiimarishe katika Kitengo chake cha TBC Radio Zanzibar ili iweze kusikika na kushindana na Redio nyingine kwa sababu TBC ni Redio ya Kitaifa na ina umuhimu sana katika shughuli za maendeleo ya wananchi,
kuwaelimisha lakini pia burudani kwa wananchi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri akiangalie kitengo chake cha Zanzibar katika TBC Radio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nami kama Waheshimiwa wenzangu nizungumzie michezo; na nitazungumzia mpira wa miguu, riadha na ndondi. Hii miwili naizungumzia zaidi Kimataifa, yaani riadha na ndondi. Kwa muda mrefu tunashiriki katika mashindano mbalimbali lakini ushiriki wetu unakuwa hauna mafanikio sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi uliopita au mwisho wa mwezi huu tulikwenda katika Jumuiya ya Madola, lakini hatukurudi hata na medali moja. Kosa kubwa ambalo tumelifanya, baadhi ya wanariadha wanaotegemewa ambao wengi wanatoka katika vikosi vyetu vya ulinzi hawakushiriki na hatimaye Tanzania imerudi mikono mitupu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri wakae na Wizara ya Ulinzi ili waangalie taratibu gani zitawezekana ili wanamichezo wetu waweze kushiriki katika mashindano haya ya Kimataifa. Ni aibu kwa nchi yetu kwenda katika mashindano yale na tukarudi mikono mitupu wakati majirani zetu Kenya na Uganda wamerudi na medali kibao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la kusikitisha katika riadha, kuna baadhi ya wanamichezo hawakwenda Jumuiya ya Madola na waliruhusiwa ili wajiandae na London Marathon, lakini hatua ya mwisho wanariadha hawa nao hawakuruhusiwa na hawakwenda na Tanzania ikakosa tena medali katika London Marathon ambayo tunaipata kila mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba jambo hili nalo Serkali waliangalie, waweke utaratibu ili tujiandae kwa mwakani kwa sababu kutokushiriki kwetu, kwanza tunakosa medali lakini pili, tunawavunja moyo wale wanariadha wenyewe kwa sababu hili nalo ni suala la ajira yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nizungumzie mpira wa miguu. Kwanza nianze kwa kuzipongeza timu zetu za vijana za Serengeti Boys na Ngorongoro Heroes. Tumeweza kuingia fainali katika Mashindano ya Vijana wa Afrika Mashariki na Kati, lakini pia timu yetu ya Ngorongoro nafikiri inakwenda katika mechi ya mwisho kabla ya kwenda AFCON kwa vijana chini ya miaka 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwapongeze sana Wizara na TFF kwa mafanikio ambayo tumefikia. Kwa bahati nzuri, timu zote mbili hizi ziko chini ya makocha Wazalendo. Kwa hiyo, kama alivyosema Mheshimiwa Chumi, kama Serikali itapanga mpango mkakati wa kuwasomesha makocha Wazalendo, mimi naona kwamba faida kubwa inaweza kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa uendeshaji wa TFF; TFF wamefanya uchanguzi mwishoni mwa mwaka 2017, wamepata viongozi wapya. Wapenzi wa mpira wote wana matumaini makubwa na uongozi huo, lakini hapa katikati tumeanza kusikia migogoro ya kufukuzana na mambo mengine. Naomba Mheshimiwa Waziri ukae nao hawa wakae vizuri kwa sababu tukiwa na uongozi mzuri, imani ya wananchi ya Serikali na mashirikisho ya Kimataifa yanakuwa makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mwenyewe ni shahidi kwamba mwaka huu tulipata ugeni mkubwa wa Rais wa FIFA na akifuatana na Rais wa CAF yaani Shirikisho la Mpira la Afrika. Wamekuja Tanzania, wamezungumza, wametoa ahadi nyingi lakini ahadi zile haziwezi kutekelezeka kama uongozi wenyewe utakuwa wa kuyumba na wa kubabua babua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo pia tetesi za upotevu wa mapato katika mpira kama alivyosema Mheshimiwa Cosato Chumi kwa uwanja mkuu wa Taifa na uwanja wa uhuru. Kamati imesema kwamba mapato haya yachanganuliwe, kila uwanja uwekewe mapato yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lipo tatizo katika uwanja Mkuu wa Taifa. Wakati wa mechi kubwa katika uwanja ule kunakuwa na uuzaji wa madawa ya kulevya na zaidi bangi. Sasa kwa bahati nzuri TFF wanaye Mkuu wa Usalama wa Viwanja. Tatizo hili linalotokea, Mheshimiwa Waziri tunaomba alifanyie kazi ili suala hili lisiweze kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo naomba nizungumzie kwa uchache kuhusu wasanii kwa sababu leo ni siku ya Ijumaa nami nataka kukimbilia Msikitini kama wenzangu, kwanza nawapongeza wasanii wote wa Tanzania kwa juhudi zao za kuendeleza sanaa, tumetoka katika burudani, lakini sasa tumeingia katika ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri ni vyema wasanii wakawa na maadili, lakini taratibu zifuatwe. Kama BASATA wamepewa fursa hii kikanuni, basi na wao watumie nafasi yao kufanya kazi kikanuni ili tuepuke kuwabebesha Mheshimiwa Waziri au Viongozi wa Wizara kufanya kazi ya BASATA ambalo limeundwa kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wapo wasanii wengine wanapotoka, wanazidisha mambo yao, lakini ni ukweli ulio wazi kwamba tunachelewa sana kuwaelimisha na kuwachukulia hatua. Wakati mwingine tunapochukua hatua ni kama tunawazindua watu kwamba kumbe ile nyimbo nayo ina maudhui mabaya. Watu wengine walikuwa hata hawajui kama kuna maudhui mabaya katika hizo nyimbo, lakini tunapowazindua ndiyo tunakuwa tumewazindua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni vyema, kwa sababu BASATA kazi yake inashughulikia, inaangalia na kadhalika, tuchukulie kama Baraza la Michezo la Taifa. Katika mchakato wa club kuingia ubia na wafadhili mbalimbali, wametoa mwongozo wao kwamba ili ukubaliwe kufanya hili, lazima uwe na moja, mbili, tatu. Kwa hiyo, vile vilabu vinaelewa kwamba tukikubaliana katika jambo hili tutafikia hatua hii; tukikosana hapa, hatuwezi kwenda ingawa bado kuna maoni kwamba hata ingekuwa fifty, fifty katika uwekezaji ingekuwa siyo jambo baya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo yangu hayo, naomba niunge mkono bajeti hii ya Wizara ya Habari kwa asilimia mia moja na nawaomba wenzangu waipitishe bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.