Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. William Mganga Ngeleja

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Nami naungana na wachangiaji wengine kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Wasaidizi wake akiwemo Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wa Wizara hii. Wizara hii ina bajeti ndogo sana lakini tunaona kazi kubwa wanayoifanya kwa manufaa ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa ni sehemu ya utangulizi wa mchango wangu, niungane na Watanzania walio wengi sana katika nchi yetu kuitakia kheri na kuipongeza timu ya Simba Sports Club ambayo sasa iko kwenye maandalizi ya kukabidhiwa ubingwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama ambavyo tunafahamu ukilinganisha, kwa sababu soka ni shughuli ya sayansi na inaweza kulinganishwa kwa kupimwa, kulinganishwa na ligi zinazochezwa duniani kote….

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari ya kweli ambayo ninaizungumza kwamba hapa duniani kwenye ligi ngumu ni timu mbili tu ambazo zimebaki hazijafungwa, iko Barcelona kwenye ligi ya LaLiga na iko Simba sports Club Tanzania. Kwa hivyo mambo yanaenda vizuri na Wanasimba tuko vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma dira kwenye ukurasa wa nne wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri ambayo kimsingi naiunga mkono, dira ya Wizara hii inasema ni kuwa na Taifa linalohabarishwa vizuri, lilishamirika kiutamaduni na lenye kazi bora za sanaa na lenye umahiri mkubwa katika michezo ifikapo mwaka 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ukurasa wa 49 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri na hasa kile kipengele kinachozungumzia sekta ya maendeleo ya michezo, kinaelezea, pamoja na mambo mengine kwamba kinaizungumzia Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Mwaka 1995 ambayo sasa hivi nafahamu Serikali inaipitia, pale yameelezwa malengo makuu ya sekta ya maendeleo ya michezo katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya lengo ambalo limeelezwa katika kipengele hicho kuhusu sera ya michezo ni kuhamasisha umma wa Watanzania kushiriki katika michezo na mazoezi ya viungo, kuwezesha upatikanaji wa viwanja na zana bora kuhusu michezo lakini pia kuandaa na kutayarisha wataalam wa michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze kuchangia kwenye hoja ya Mheshimiwa Waziri kwenye eneo hili. Nianze kwa kulipongeza sana Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Job Ndugai, kwa sababu sisi kama watunga sheria na wasimamizi kimsingi wa utekelezaji wa sera za nchi yetu tumeshiriki kwa vitendo.

Bunge Sports Club inawakilisha, kwamba tumekuwa tukishiriki katika masuala ya michezo na hasa kufanya mazoezi viwanjani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kesho nawaalika Wabunge wote tushiriki kuanzia saa 12 asubuhi kwenye lango kuu kama tulivyotangaziwa asubuhi, Wadhamini wetu NMB watashirikiana na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye matembezi ya mwendo wa pole, kwenye shughuli ya kukimbia kwa mwendo wa taratibu lakini pia na matembezi kuanzia hapa mpaka uwanja wa Jamhuri. Hii ni mojawapo ya utekelezaji wa sera ya michezo Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Taifa letu iko michezo mingi kwa sababu hatuwezi kuzungumzia yote kwa pamoja kwa mtu mmoja kwa dakika kumi, nataka nijielekeze kwenye mchezo unaopendwa sana duniani. Siyo kwamba najielekeza huko kwa sababu michezo mingine haipendwi, hapana! Nazungumzia soka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto kubwa. Nimesoma dira ya Serikali inasema kufikia mwaka 2025 tuwe Taifa ambalo limeshapiga hatua kubwa sana kimichezo, lakini leo ukiwauliza Watanzania toka miaka ya 1980 ambapo timu yetu ya Taifa ilifanikiwa kushiriki kwenye mashindano ya kombe la Afrika kwa kipindi chote hiki tumekuwa tukiugua maumivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali itufungulie na ijifunue wakati Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anafanya winding up atusaidie kuelezea mikakati ya Serikali ya kututoa hapa tulipo kwenda kulifikisha Taifa lilipokuwa miaka ya 1980, miaka ya 1970 na hata mwanzoni mwa miaka ya 1990. Tuna uwezo mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona maelezo ya ujumla ya kisera na kisheria lakini kwakweli ukiangalia soka letu ilipo hapa sasa hivi tuko mahututi. Sasa hivi kwenye ranking za FIFA tuko 130 na kitu. Ni jambo ambalo linatia aibu lakini naamini kabisa juhudi anazozifanya Mheshimiwa Waziri zinaweza kututoa hapa na kutusogeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiona changamoto kwenye Baraza la Michezo ni tatizo, hapa nataka niseme ambacho nimekiona kwa sababu mwaka kesho tumepewa heshima ya kuandaa, tutakuwa wenyeji wa mashindano ya vijana walio chini ya miaka 17 kwenye mpira wa soka, mashindano yanafanyika hapa Tanzania, lakini kuna Kamati ya Maandalizi ambayo Mheshimiwa Waziri ameitaja katika ukurasa wa 49 na 50.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiona hapa tunafanya yale yale kwa miaka yote. Nataka nishauri, hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesema imezingatia maelekezo na maudhui ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyotoa hapa wiki mbili au tatu zilizopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Kamati ilivyoundwa hapa, Mheshimiwa Waziri Mkuu alisisitiza kwamba katika kufanya mambo yetu Kitaifa lazima tuishirikishe Sekta Binafsi. Sasa ukiangalia hapa kilichopo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, sijaona hata kipengele kimoja ambacho kinaelezea kwa dhamira ya dhati kabisa kuishirikisha sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo rahisi sana tukafanikiwa bila kuishirikisha sekta binafsi, kwa sababu ukurasa wa 71 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu anaizungumzia sekta binafsi ishiriki katika kuendeleza habari ya shughuli zetu za maendeleo na michezo ni mojawapo. Kwa hivyo, ushauri wangu ni kwamba tushirikishe sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunazungumzia habari ya maendeleo ya michezo na sanaa kwa ujumla, yako maeneo ambayo lazima tuyape kipaumbele, ‘Bongo Fleva’ sasa hivi imetutoa. Tunamzungumzia Msanii kama Diamond, tunaungana na Watanzania wote kumpongeza kwa hatua aliyofikia kutambuliwa kwamba awe mojawapo ya watu wanaotunga wimbo maalum kwa ajili ya Kombe la Dunia mwaka huu, hii ni heshima kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikusudii kusema kwamba hatuthamini sanaa zingine, lakini muziki wa Bongo Fleva, nafahamu akiwemo ‘Profesa Jay’ ambao wameshiriki sana kuufikisha muziki hapo ulipo, Diamond, Ali Kiba na wengine wote lazima tuwape kipaumbele katika shughuli hii ya kuendeleza sanaa hii kwa sababu ni heshima kwa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini na naishauri Serikali kwamba huko tunakoelekea sasa hivi ambapo Diamond atakwenda kutuwakilisha, Wizara ya Maliasili na Utalii itam- package kwenda kuitangaza nchi yetu, Diamond kwa sababu yeye ni nembo ya Taifa. Kwa hiyo ni muhimu sana kuwapa ushirikiano watu kama hawa kwa sababu kuna faida kubwa kuwa nao katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera inazungumzia kujenga viwanja na kuimarisha miundombinu ya michezo. Tumezungumzia Chuo cha Malya hapa. Kwa bajeti ya Serikali kama ilivyo hatuwezi kufanikiwa lakini tutakuwaje na Wataalam waliobobea kama hatuna vyuo ambavyo vinaendeleza na kutengeneza weledi maalum kuendeleza michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu tena kwa mara nyingine, kama tulivyozungumza kwenye Kamati kwamba Mheshimiwa Waziri aendelee kushirikisha sekta binafsi aone, wapo watu wanapenda tu. JK Youth Park pale Dar es Salaam Kidongo Chekundu umejengwa uwanja mzuri kwa ufadhili na udhamini wa kampuni binafsi. Tuendelee kushirikiana tuone namna gani sekta binafsi inaweza kutusaidia katika kuboresha viwanja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri kwamba kwenye ile ruzuku ambayo tunaipata kila mwaka kutoka FIFA pengine tuitumie pia kujenga, kuimarisha viwanja huko Wilayani kwa sababu nafahamu kwa ngazi ya mkoa angalau

tuna viwanja, lakini wachezaji wengi siyo lazima watoke Makao Makuu ya Mikoa tu. Ombi langu ni kwamba hili fungu ambalo tunapata kutoka FIFA kila mwaka tulitumie pia kuendeleza viwanja vya vijijini na Wilayani ambako tunaamini kwamba pia kuna uwezekano wa kuwapata wachezaji wengi wazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.