Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nami nianze kwa kuwapongeza vijana wana Paluhengo Lipuli Sports Club kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Bila kuwasahau Dar Young Africans. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaenda zaidi kwenye ushauri na mchango wangu utakuwa kwenye ushauri zaidi. Kwanza kabisa nianze kuishauri Serikali kwamba chombo kikuu ambacho kinasimamia michezo ni Baraza la Michezo la Taifa (BMT). Kwa mujibu wa sheria na taratibu, Sheria Na. 12 ya Mwaka 1967 ndiyo ilianzishia chombo hiki cha michezo maana yake Baraza na ikafanyiwa marekebisho mwaka 1971.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chombo hiki ndicho ambacho kinapaswa kusimamia, kuendeleza, kustawisha, kuratibu aina zote za michezo kwa kushirikiana na wadau. Ukiangalia chombo hiki kinategemea fedha kutoka Serikalini, sasa ukiuliza wanazo shilingi ngapi utashangaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nafikiria, either tuletewe hapa tubadilishe sheria au ikiwezekana Baraza la Michezo livunjwe kwa maana ya kuanzisha kitu kingine ambacho kinaweza kikajitegema, tukaanzisha labda Shirika la Michezo la Taifa badala ya Baraza kwa sababu ukileta likawa Shirika la Michezo la Taifa na kuna neno wadau pale wanaweza wakafanya biashara. Fedha zile ambazo tunasema ziende kwenye michezo ambazo ni za gaming za mambo ya michezo ya kubahatisha zingeweza kwenda kule wakawa na uwezo wa kujiendesha wenyewe kwa vyanzo mbalimbali ili sasa tukienda kwenye kutayarisha timu zetu tuwe na fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ambayo Mheshimiwa Mwakyembe amepata, kwanza nimpongeze sana kwanza kwa kazi nzuri ni fedha ambayo tungeweza tu kuiweka timu ya Taifa kwenye matayarisho ya michezo siyo ya Wizara. Kwa hiyo, akisema kwamba ataweza kufanya vizuri ni kujidanganya na ndiyo maana niliwahi kuuliza hapa siku moja kwa nini tusiifute michezo Tanzania? Hata hivyo, swali hili lilikuwa gumu kujibiwa. Maana yangu ni kwamba unataka kukamua maziwa wakati hujamlisha ng’ombe majani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, naomba tukae chini, tufikirie kitu gani tukifanye ili Baraza liwe na meno, uwezo kama tunataka kuendelea na Baraza, lakini kama haiwezekani tulivunje kwa sababu leo kazi kubwa ya Baraza la Michezo ni kusajili vyama vipya na kuvifunga na kuvifungia vile ambavyo vimefanya makosa, kazi ambayo siyo nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa michezo ya AFCON wa vijana chini ya miaka 17 itafanyika hapa, maandalizi sina hakika kama yameanza na hayawezi kuanza kwa sababu hamna fedha, kama yapo ni yale ya mechi hizi ambazo zinaendelea. Wasiwasi wangu ni kwamba inawezekana tukatumia fedha nyingi sana na gharama kwenye vikao kuliko maandalizi ya timu, matokeo yake tutakuja kutoa visingizio vingi, ningeomba Serikali iangalie uwezekano wa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, medali nyingi Tanzania tulianza kuzipata kwenye michezo mbalimbali, mwaka 2003 tulipata medali 12 za wanariadha kwenye Special Olympic Ireland. Bahati nzuri fedha zilikuwa hamna tukatayarisha mechi kati ya Mabalozi na Wabunge, fedha iliyopatikana tuliwasafirisha wale watoto kwenda Ireland na walileta medali 13. Baada ya hapo hakuna medali ambayo imeletwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wanapokwenda kwenye riadha bahati nzuri Filbert Bayi yupo nimemwona, wanapokwenda kuwakilisha nchi, hawaendi watatu au wanne. Sisi tumepeleka wanariadha timu nzima nafikiri hawazidi 50, wanariadha waliotoka Kenya walikwenda 200 hawawezi kukosa medali, lakini sisi utapeleka wote hao kwa maandalizi gani? Kwa hiyo, naomba kama kweli tunataka michezo ya nchi iendelee basi tujipange. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri ajaribu kwa sababu Mabaraza hayapo yamekufa kama yapo hayana uwezo, akae na wadau tena aanzie hapa Bungeni, akae na wadau wa michezo tuko wengi tu halafu tuone tunatokea wapi ili tusimwache peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Mheshimiwa Cosato Chumi amelizungumza na mimi niliwahi kuzungumza hapa, kwamba sisi tunataka timu ya Taifa ifanye vizuri. Timu zetu zimesajili wachezaji wengi wa kigeni kutoka nje ambao hawana uwezo. Kwa hiyo kinachofanyika wachezaji wetu wanakosa nafasi. Unasajili wachezaji ambao hata kwenye nchi zao hawana nafasi, unakuja inakuwa dampo. Kwa hiyo, ningeomba Ndugu yangu Karia yupo, hebu waangalie uwezekano wa kupunguza idadi ya wachezaji, ikishindikana basi angalau wale watakaokuja kucheza wawe ni watu ambao wana uwezo kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Timu ya Taifa inapocheza, jezi zile inazotumia hazina hadhi ya nchi yetu kwa sababu hazina bendera, rangi zetu zinafahamika za bendera yetu lakini leo tunavaa jezi nyeupe wapi na wapi, tumekosa rangi.
Kwa hiyo, niombe Karia yupo hapo, Kiganja nimemwona, ndugu yangu Tandau nimemwona, hebu wakae wafikirie, tusitie aibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia najua sana kwamba Wizara kwa kushirikiana na TFF watapita kuangalia viwanja vyenye hadhi vitakavyotumika Kimataifa ili viweze kutambulika na FIFA. Uwanja wa Samora Iringa hebu wapite pale waone umetengenezwa kisasa, uko vizuri na watu wako radhi wana uwezo wa kwenda kuangalia mpira na wameona timu ya Lipuli mambo ambayo inafanya, unaweza ukawauliza watu wa Singida wanaweza kueleza.(Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ningependa kumpongeza sana Mwenyekiti wa Bunge Sports Club ndugu yangu William Ngeleja. Baada ya Wabunge kushiriki michezo tumepata faida kubwa sana; moja, ukiangalia idadi ya watu wanaokwenda hospitali kutibiwa imepungua. Idadi ya watu wanaokwenda kwenye sehemu za starehe kunywa pombe imepungua, ndiyo maana umeona hata walioitwa kwa Mheshimiwa Paul Makonda walikuwa wachache kwa sababu wamekuwa na shughuli sasa nyingine mbadala ya kufanya ambayo ni mazoezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Spika amwangalie Mheshimiwa William Ngeleja amwongeze fungu kwenye fedha zile ili wanamichezo wengine washiriki, lakini sitaacha pia kumshukuru Mwenyekiti pamoja na Majimarefu ambaye kwa kweli wanasaidia kwenye yale mambo mengine na kufanya timu yetu iweze kufanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchangiaji aliyemaliza amechangia vizuri sana, niombe badala ya kulalamikia viwanja vile ambavyo vina wenyewe, tuangalie uwezekano wa kuomba vingine kuna nafasi, ombeni CHADEMA muweze kupata viwanja vingine vya michezo waje waombe, Iringa tuna maeneo, Kilolo tuna maeneo, waje waombe ili nao wamiliki badala ya kugombea hivi ambavyo vipo, kwa sababu hivi tumerithi zamani Chama kilikuwa kimoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.