Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Tauhida Cassian Gallos Nyimbo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa jioni hii kuweza kuchangia Wizara hii ya Habari na Michezo. Kwanza kabisa nichukue fursa hii ya kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake lakini kwa umuhimu mkubwa nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri, naamini kwamba anafahamu na anaelewa kwamba yeye ni baba na baba siku zote kazi yake ni kulea, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri nichukue fursa hii kumshukuru kwa sababu anajua kwamba ni wajibu wake kulea. Wizara alionayo takribani vijana wengi wa Tanzania wapo hapo. Vijana wa Tanzania shughuli kubwa wanazozifanya kwa sasa wamekimbilia kwenye suala la sanaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajielekeza zaidi kwenye vijana nizungumzie chombo chetu cha TBC. Chombo cha TBC kiumri mimi siwezi kuipata lakini inafikia wakati inatubidi tuizungumze na nategemea kwamba kuna baadhi ya Viongozi wa TBC watakuwepo mahali hapa. Kwa kweli mfumo wao wa kazi wengine hauturidhishi na maeneo hususan yasiyoturidhisha TBC ni pale ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Mawaziri wanapokuwa na mambo mahsusi kwenye taarifa za habari niliwahi kuzungumza miaka mitano nyuma iliyopita, lakini sidhani hili kama nina hoja ya msingi kuishawishi Serikali yangu iwaongezee bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi suala la kukaa la kupanga vipindi vipi wafanye, hili linahitaji bajeti gani kwa sababu mimi ninavyofikiria, nadhani kwamba ni suala la karatasi na peni na kukaa na Watendaji Wataalam wakajipanga. Sidhani hili kwamba linanishawishi kuishawishi Serikali kwamba waongeze fedha ili kuweza kulifanikisha hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu ni jambo la aibu, tena ni aibu kweli kukuta chombo kama cha TBC tunachokitegemea wanafanana na vyombo vingine vya habari ambavyo vinamilikiwa na watu binafsi au wao kupitwa na vyombo vya watu binafsi. Hivi leo TBC Rais amekwenda kufungua miradi tofauti na mikubwa, kweli kwenye taarifa ya habari unachukua dakika tatu, anasimama Mheshimiwa Tauhida leo kaenda Jimboni kwake dakika tatu, akisimama sijui nani dakika tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais ni Rais wa nchi hii tuwape fursa viongozi wetu hususan Rais wetu, apewe fursa na hakuna chombo kinachoweza kumpa fursa zaidi ya TBC. TBC wametutia aibu, chombo chao tulitegemea ndiyo kiwe mkombozi wa Watanzania kwenye kutoa habari, hivi leo TBC nikwambieni ukweli, hivi kweli leo Wabunge tukasimame hapa tukaisifie ITV, Azam tena na Wasafi TV sasa wanaikimbiza TBC, kitu ambacho kwangu ni aibu najisikia vibaya kusimama hapa kuizungumza TBC. Hamu yangu na shauku na niliwahi kuzungumza kwenye Bunge, siyo vibaya ku-copy kwa ndugu yako. Leo Zanzibar wanaweka vipindi wanaweka mpangilio wa TV kujua sasa taarifa ya Rais inatoka kwenye chombo cha habari. Leo unakuta watu wanakimbia wanaenda kuwahi kufungua taarifa ya habari anafungua TBC, baada ya dakika tatu anaona sherehe ya harusi ya mfanyakazi wa TBC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Azam, mmoja wao niliangalia katika shughuli ya Ali Kiba niliangalia, walifanya vizuri walijua muda wa kutenga kuweka shughuli ile. Leo TBC tunategemea waweke vipindi vyao vizuri wapange mpangilio kwa itifaki kwamba inakuja ripoti ya Rais, inakuja ya Makamu wa Rais, inakuja Waziri Mkuu tunakwenda kwa itifaki hii, nchi inaongozwa na itifaki. Huwezi kumpangia Rais anazungumza kwenye taarifa habari dakika tatu au dakika nne siyo kitu kizuri, TBC kwa hili naomba wabadilike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri alichukue, nililizungumza miaka mitano nyuma imepita, naomba alichukue alifanyie kazi. Hivi hili niliombee bajeti gani, liongezwe bajeti gani, hivi Rais anaongelea masuala ya ndege, anaongelea masuala ya Tanzania kwenye miradi ya reli, anaongelea wananchi jinsi gani wanaweza kunufaika na mazao yao, anapewa dakika tatu kwenye taarifa ya habari na hizo TV nyingine zinafanyaje? Naomba Mheshimiwa Waziri walifanyie marekebisho hili. Bajeti ijayo nafikiri nitakuwa namba moja kukamata shilingi ya mshahara wa Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri tuje kwenye suala la sanaa, kwa wasanii limekuwa sawa na ng’ombe wa nyuma kutandikwa bakora, wakati ngombe wa mbele hatembei. Kwa kweli, Mheshimiwa Waziri inatubidi tuseme, atusamehe watoto wake, wasanii wanaonewa, tufike wakati tuseme wanaonewa. Hii BASATA inafanya kazi gani? BASATA kabla ya nyimbo ya msanii kutoka wao ndiyo wanaotakiwa kujua anaimba nini, kwa sababu kwenye Kiswahili kuna kitu kinaitwa tungo tata. Sasa inawezekana wasanii kuna maeneo wanatumia tungo tata, kama wanatumia tungo tata Baraza lipo, wanafanya kazi gani? Mheshimiwa Waziri hebu atupe mfano hii BASATA hebu awatoe, wanachokifanya wanawaonea wasanii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani wapewe posho, mishahara, kazi wanayotakiwa kuifanya hawaifanyi matokeo yake msanii ameshajituma, ndani ya mwaka mmoja ndio anakuja kufungiwa nyimbo yake. Hatumaanishi kwamba kila kinachofanyika ni kizuri hapana, nyimbo inawezekana ikawa mbaya na inawezekana maneno yaliyotumika yakawa mabaya na wanavyofanya baadhi ya wasanii na sisi haturidhiki navyo, lakini kuna chombo kinatakiwa na wao wawajibishwe ili twende sawa. Asipigwe bakora ngombe wa nyuma wakati wa mbele hatembei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie vilevile kitu ambacho dada yangu Devotha hapa alizungumzia, Waziri aje na sheria, aje na kanuni kila kinachohusu sheria kama kuna sheria zimekaa upande huko atuletee maana Mheshimiwa Devotha anavyozungumza kazungumza kwa kujua anakizungumza nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hili kwa sababu sheria lazima zije Bungeni tuziweke sawa. Haiwezekani Mmiliki wa Vyombo vya Habari akaamua kufanya anachokitaka yeye mwenyewe kisa tu kwamba wana uhuru, uhuru usiokuwa na mipaka una tatizo. Uhuru wowote anaopewa binadamu ukiwa hauna mipaka unakuwa na matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo utamkuta mmiliki wa chombo binafsi kakorofishana tu. Nimtolee mfano Ali Kiba samahani kama italeta shida. Leo anaenda kuimba kakosana na mmiliki wa vyombo anafunga hata nyimbo zake kutokuimba, sidhani kama ina tija, sidhani kama ina faida. Sasa hizi sheria anazozizungumza dada yangu zije Bungeni hii ni nchi inaongozwa na watu makini. Sheria Waziri alete Bungeni tuzifanyie kazi lazima watu wote tufuate sheria twende na utaratibu, siyo kila mtu aamue anavyotaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue fursa hii ya kuwapongeza wasanii wengi wanaofanya vizuri kuliwakilisha Taifa letu. Kwa siku ya leo nimpongeze dada yangu Monalisa amefanya vizuri, amevaa bendera ya Tanzania na picha zake zote ukiziona nyingi takribani ana bendera ya Tanzania. Siyo yeye tu na wengi wapo wanaofanya kwa ajili ya kutetea Tanzania. Hili linaonesha sura fika kwamba sanaa ni faida kwetu, sanaa ina uwezo wa kuongeza kipato kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongezee kidogo Waziri atakapokuja kufanya majumuisho siyo mtaalam sana kwenye mambo ya michezo, lakini kipindi cha nyuma tulikuwa Zanzibar sana tunalalamikia masuala ya michezo ila kwa sasa shwari imepatikana...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)