Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kuonesha masikitiko yangu kwa mgogoro wa wakulima na wafugaji katika Kata ya Magindu na Gwata Mkoani Pwani katika Jimbo la Kibaha Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ziara yangu ya kushukuru wapiga kura wa Mkoa wa Pwani hususani Kata ya Gwata na Magindu nimepokea malalamiko toka kwa wananchi juu ya mgogoro unaoendelea kati ya wakulima na wafugaji. Mfano katika Kata ya Magindu, Kijiji cha Mizuguni mgogoro huo umeota mizizi kwani wafugaji (Masai) na mifugo yao huvamia mashamba ya wakulima na kula mazao yao suala linalopelekea mapigano baina ya jamii hizo mbili. Mgogoro ambao hata Kamati ya Kijiji cha Mizuguni imeshindwa kuutatua. Hata wakulima walivyokimbilia Mahakamani bado wamekuwa wakishindwa kesi hizo (za kuharibiwa mazao yao kila siku) kwa kuwa wafugaji jamii ya Kimasai huhonga Mahakimu na hatimaye wanashinda kesi hizo. Hali hiyo pia imejitokeza katika Kata ya Gwata, Kijiji cha Mlalazi, mifugo (ng‟ombe) wanamaliza mahindi ya wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa zaidi hapa Mheshimiwa Waziri, wafugaji hawa walishatengewa eneo la kwenda ambako ni Vinyenze, kijiji hiki kiliwekwa ama kutengwa mahsusi kwa ajili ya wafugaji ili kunusuru mazao ya wakulima lakini hadi leo hii ninavyoongea wafugaji hao wamegoma kwenda Vinyeze hali ambayo inaendeleza migogoro baina yao na wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana hili suala si la kuchukulia mzaha kwa kweli maana huu mgogoro unafukuta chini kwa chini, siku ukija kulipuka hapatatosha. Hivi ninavyoongea katika Kata ya Gwata wakulima hawaoani na wafugaji lakini pia wanapigana mapanga na kuumizana ilhali hapo awali walioleana.
Mheshishimiwa Spika, naomba sana Serikali kuingilia kati kunusuru jamii hizi mbili kuacha kupigana na kuhatarishiana maisha. Pia Serikali iingilie kati ili wafugaji ambao wanasemekana ni matajiri waache kuwaonea wakulima wanaosemekana ni wanyonge. Kesi inapokuwa Mahakamani wafugaji wanakimbilia kuhonga halafu mwisho wa siku Mahakimu huwapa ushindi huo wafugaji only because wamepokea hongo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nimeamua kuchangia hoja hii moja tu mwanzo mwisho kwa sababu ya umuhimu na upekee wake. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri baada ya Bunge hili la bajeti katika ziara zako za kikazi Mkoa wa Pwani uwe kwenye orodha kwa kuipa kipaumbele Kata ya Gwata na Magidu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii, naomba kuunga mkono hoja. Niwatakie kila la kheri Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri katika kutimiza majukumu ya kilimo, uvuvi na ufugaji kwa maslahi ya Taifa letu.