Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mwakyembe kwa hotuba nzuri na yenye kutia matumaini makubwa kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchezo wa mpira wa miguu bila shaka ndiyo mchezo unaopendwa na Watanzania wengi kuliko mchezo mwingine wowote hapa nchini. Ni ukweli usio na shaka shirikisho linalosimamia mchezo huu TFF, lina changamoto nyingi zinazohitaji kurekebishwa ili kuleta faraja na furaha kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa changamoto hizo ni Katiba ya TFF ina mapungufu mengi sana, mojawapo likiwa ni hili la uchaguzi wa kumpata Rais wa TFF. Ushiriki wa wadau ni mdogo sana na vigumu kuamini Rais wa TFF Taifa anapigiwa kura na Wajumbe 128 tu nchi nzima. Kuminywa huku kwa demokrasia kunasababisha kupata viongozi wabovu. Tatizo hili linaanzia kwenye ngazi ya chini kabisa mpaka Taifa. Nimuombe Mheshimiwa Waziri aangalie namna ya Katiba ya TFF kufanyiwa marekebisho makubwa ili kuongeza ushiriki mkubwa wa wadau kwenye chaguzi za ngazi zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuanzishwa kwa kituo kikubwa na cha kisasa kwa wanariadha Wilaya ya Mbulu, Mkoa wa Manyara ni jambo muhimu katika kukuza vipaji vya wanariadha wetu. Nchi yetu miaka ya 1970 na 1980 ilikuwa haikosi kwenye orodha ya nchi zinazopata medali kwenye michuano ya Kimataifa na kwa kiasi kikubwa wanariadha hao walikuwa wanatoka maeneo ya Mkoa wa Manyara, hivyo ni muhimu Waziri ukalifanyia kazi wazo hili ili tuwe na chuo ama kituo cha kisasa cha michezo pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuzorota kwa michezo katika Majeshi yetu ni jambo ambalo Mheshimiwa Waziri alitupie macho vilevile. Zile zama za kina Willy Isangura, Nassoro, Michael, Kingu na kadhalika zimeyeyuka na tumekuwa wasindikizaji kwenye michezo ya Kimataifa. Ipo haja ya kuliangalia jambo hili kwa undani kujua chanzo chake na kupata ufumbuzi ili turudi kwenye zama zile mchezo wa ndondi na mingine iliyokuwa inatuletea sifa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii.

Ahsante.