Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Martha Moses Mlata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kumbukumbu zangu kuna kauli aliyoitoa Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano kwamba COSOTA na BASATA ziunganishwe pamoja ili kuboresha utendaji kazi na kuwahudumia kwa ubora zaidi wasanii wote. Hii ni kutokana na COSOTA kushindwa kabisa kuwasaidia wasanii na kulinda kazi zao, kiasi kwamba zinaibiwa kila kukicha ilhali COSOTA wapo. Je, ni lini COSOTA na BASATA zitaunganishwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali au Wizara inatamka nini juu ya Msama Production ambaye yeye amekuwa akifanya kazi ya COSOTA ya kuzuia wizi wa kazi za sanaa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni kuwa TRA wanapoteza mapato mengi sana kwa kutodhibiti wizi wa kazi za sanaa? Kwa sababu kudhibiti wizi huu na kazi zote zikauzwa kihalali, Serikali itapata na msanii atapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri kuwe na one stop center ya wasanii pamoja na vyama mbalimbali vinavyoanzishwa, lakini kuwe na mahali pamoja ambapo msanii au chama cha sanaa kingeweza kuripoti kwa maana sasa hivi Maafisa Utamaduni wako TAMISEMI, COSOTA iko Viwanda na Biashara na BASATA iko Wizara hii ya Habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hii kero na usumbufu wa TRA kuchelewesha kutoa sticker, kitu ambacho kimekuwa ni usumbufu mkubwa na kurudisha maendeleo ya wasanii wetu. Je, Serikali inalisaidiaje hili maana hizo ndizo kero za kutokana na kutokuwepo kwa one stop center ya wasanii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya nyuma COSOTA walikuwa wakiwalipa wasanii mirabaha ya kazi zao ambazo COSOTA hukusanya kupitia TV, Radio na kadhalika, lakini siku hizi hawalipi na kama wanalipa nadhani wanawalipa wasanii wachache sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kumnyang’anya COSOTA jukumu hilo na kutafuta chombo kingine kifanye kazi hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu COSOTA hawawezi, hata ukienda kuuliza wanadai kuwa mashine ya kufanya mahesabu ya mgao wanasema mpaka wapate mtaalam kutoka Uswisi. Je, hivi ni kweli hii nchi hakuna mtaalam wa hiyo mashine mpaka wamsubiri kutoka Uswisi? Kama ni kweli jambo hilo naomba kupatiwa majibu. Pia ningependa kujua hizo fedha zipo na ziko ngapi na ziko wapi? Hapa naomba majibu ya kina ama lah, nitashika shilingi na naweza kubaki nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba ya COSOTA imetoa muda wa kugawa hiyo mirabaha kwa wanamuziki lakini utaratibu huo haufuatwi. Katiba inasema mgao utakuwa Desemba lakini hautazidi mwezi wa Pili, lakini hadi sasa hawajalipa kwa muda mrefu sasa. Kauli yao ni mashine mbovu, mtaalam aletwe toka Uswisi! Jamani, Please!

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu warejee enzi za Mzee Steven Mtetewaunga alikuwa Afisa wa COSOTA, malipo yalikuwa mara mbili kwa mwaka mwezi wa Sita na Desemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasita sana kuunga mkono hoja. Naomba tu ieleweke wazi kuwa na mimi ni msanii wa muziki wa Injili Tanzania hivyo na-declare interest kuwa ni mdau wa sanaa ya muziki na nimesajiliwa COSOTA, BASATA na kadhalika.