Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Lucy Fidelis Owenya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Viwanja vya Michezo. Mkoa wa Kilimanjaro kila mwaka wiki ya kwanza ya mwezi wa tatu panakuwepo na mbio za Kilimanjaro Marathon. Mbio hizi kwa sasa zimezidi kukua mwaka hadi mwaka na zinahusisha wageni kutoka nje ya nchi na wenyeji Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbio hizi zinachangia sana uchumi kwa wakazi wa Moshi na Taifa kwa ujumla kwa sababu wageni zaidi ya kukimbia pia hufanya utalii wa kupanda mlima na kutembelea mbuga zetu za wanyama. Mbio hizi kwa sasa kuanzia uwanja wa Chuo cha Ushirika Moshi na kumalizikia pale. Hata hivyo, kwa jinsi mbio hizi zilivyopata umaarufu uwanja ule unalemewa na wingi wa watu ambao ni hatari kwa maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Moshi tuna uwanja mkubwa wenye michezo zaidi ya saba unaoitwa King Memorial Stadium, lakini uwanja huu hautumiki ipasavyo ukizingatia kuwa hakuna viwanja vya michezo Moshi na huu uwanja unamilikiwa na mkoa. Kwa sasa ni sehemu ndogo tu inayotumiwa na wauza nguo za mitumba. Je, ni kwa nini Serikali isitafute watu binafsi kwa kushirikiana na Serikali wakakijenga kile kiwanja ili kiweze kutumika hata kwa michezo mingine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa kuwa kilipewa jina la mfalme wa Uingereza naamini likiandikwa andiko zuri mfalme anaweza kukijenga kiwanja kile na tukaendelea kukiita King Memorial Stadium. Hii itachangia Serikali kupata

mapato yatokanayo na uwanja huu, itatengeneza ajira na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utamaduni; hivi utamaduni wa Mtanzania ni upi? Ni siku nyingi tumekuwa tukilizungumzia Vazi la Taifa na kuna wakati ilitolewa mifano ya Vazi la Taifa lakini hadi leo hatujaelezwa mchakato ule ulifikia wapi. Ni lini tutapata Vazi la Taifa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, misingi ya utamaduni wetu Watanzania ulijengwa tuwe na utu, upendo, amani na utulivu lakini kwa sasa nchi yetu tunaelekea kupoteza vyote hivi na mpaka sasa hivi Serikali haijaweza kutueleza hao watu wasiojulikana ni akina nani? Watu wamekuwa wanatekwa, wanauawa na kuokotwa baharini kwenye viroba, waandishi wa habari wanatekwa, yote haya ni amani, upendo, utu na utulivu kutoweka. Je, Serikali inatueleza nini kuhusu utamaduni wetu huu kupotea?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Haki ya Kupata Habari. Hii ni haki ya msingi ambayo ipo kikatiba kabisa ya watu kupata habari; lakini tumeshuhudia sasa hivi Serikali imekuwa ikivifungia vyombo vya habari pindi wanapoikosoa Serikali. Pia ni haki ya Watanzania kuona wawakilishi wao Bungeni kama wanazizungumzia kero zao, lakini haki hii wamenyimwa kwa kuzuiwa kwa Luninga (TV) kutokuwa mubashara (Live) wakati vipindi vya Bunge vikiendelea. Huu ni uvunjwaji wa sheria, inapelekea nchi kuendeshwa bila kufuata sheria.