Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Kilombero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PETER A.P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kuna mambo ambayo yanafanyika kwenye nchi yetu mimi natafsiri ni kama vile yanaleta fedheha kwa Jeshi la Polisi. Mambo haya yanafanya jeshi letu lionekane kama vile halina weledi, sijui ni kwa nini. Kwa mfano, utaona kuna bwana mmoja alimtishia Nape bastola, Waziri akasema huyu mtu tutamshughulikia, huyu mtu atafutwe, lile suala jinsi lilivyoenda mpaka leo kimya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu yule anaonekana mtaani, yupo na hata juzi amefanya kazi mbele ya kamera. Sasa sielewi matamko haya huwa yanatoka kwa nia gani, ina maana Polisi hawaoni kwamba haya mambo yanachafua Jeshi letu la Polisi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo amekamatwa akiwa ofisini kwake mpaka leo amepotea, haifahamiki yuko wapi. Taarifa zinasema aliyemkamata ni DSO, Mzee Mkuchika hapa anasema siyo wao, anasema hii ni kazi ya Polisi, Polisi wako kimya hawasemi chochote. Hii inafanya Jeshi letu lionekane kama vile halina taaluma hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, RPC wa Iringa anasema Nondo alikwenda mwenyewe Polisi kwenda kusema kwamba yeye hakutekwa wakati Kanda Maalum ya Dar es Salaam inasema Nondo amekamatwa. Haya mambo yanaonesha hili Jeshi letu linafanya kazi siyo kwa taaluma. Niwaombe sana Polisi wetu, kama wanapewa mashinikizo kwenye kazi yao, wajue kabisa kwamba wao ndiyo wanakuwa answerable mambo yanapoharibika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine ni Roma Mkatoliki. Roma ametekwa, akasema ameteswa na akasema anashindwa kuongea kwa sababu anaogopa maisha yake yako hatarini, Polisi wanasikiliza tu hawasemi chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni huyu Ndugu yangu Musiba. Musiba anaongea maneno hapa mabaya kabisa, Polisi wanasema wanachukua hatua. Mheshimiwa Lissu alisema maisha yake yapo hatarini, yapo kwenye shida, Polisi wanasema kama Mheshimiwa Lissu hakwenda Polisi kushtaki wenyewe hawana mpango lakini Musiba anaongea mambo ya hovyo kabisa, Polisi wanasema wao wanafanyia kazi, this is so unprofessional na hii inasababisha Jeshi letu kuonekana halina weledi. Watu wamekaa juu hapo wamesoma, wana uwezo mkubwa, kwa nini wanafanya vitu ambavyo vinaonesha kwamba hawana uwezo, kwa nini wasioneshe uwezo wao ambao sisi tunaamini wanao? Kwa nini wanafanya hivi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mambo ambayo yana-brand Taifa letu kuwa ni Taifa ambalo lina taasisi ambazo hazijielewi. Taifa letu lilikuwa linaheshimika duniani kwamba ni sehemu ya amani, ni sehemu nzuri ya kuishi. Leo Taifa letu linakuwa branded ni sehemu moja ya hovyo kwa sababu watu ambao mmepewa kazi za kufanya mnashindwa ku-act professionally mnafuata maagizo ambayo ni politically. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa hili likienda sehemu mbaya, juzi hapa Mkuu wa Polisi wa Arusha alipata ajali watu wana-comment bora afe tu, no, no, no! Wazee huko juu msifurahie mambo haya. Mheshimiwa Waziri asifurahie mambo haya, ni lazima wajiulize kuna shida wapi? Kwa nini mtu afurahie kifo chako? Wanakosea wapi? Kama Taifa tunakosea wapi? Haya mambo lazima wajiulize! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize kwa kusema maneno yafuatayo. Diwani wangu Luena alifariki, taarifa zinasema treni ama kipisi kilipiga honi mara tatu kwenye eneo la tukio. Hii inaleta picha kwangu inawezekana ile treni ilikuwa imewachukua watu ambao walimuua Diwani wangu kwa sababu ni kwa mara ya kwanza tangu kipisi kimeanza kazi ndiyo imepiga honi mara tatu nusu saa baada ya tukio, haiwezekani! Naomba hili walifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa, nimwombe Mheshimiwa Waziri amwambie IGP wetu aje Ifakara aongee na Polisi wangu Ifakara, asikie na wao wana shida gani, asiende tu sehemu zingine anaongea nao, kule kuna shida nyingi sana, kituo kibovu. Aje, akae na sisi hata kama ni kuchanga, tuchange, kama ni kusaidia tusaidie, kama ameshindwa kujenga, sisi hela zipo, wananchi watatoa. Kwa hiyo niwaombe hilo, nashukuru sana.