Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru sana kwa kuniruhusu nichangie hoja hii ya hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kwanza nianze kwa kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wake kwa maana ya Mheshimiwa Mwigulu na Mheshimiwa Masauni, pia Katibu Mkuu wao na viongozi wote wa Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Vilevile niwapongeze Wakuu wa Idara wote, Jeshi la Polisi, Uhamiaji, Magereza na Zimamoto. Nawapongeza sana kwa kazi nzuri wanayofanya pamoja na matatizo madogo madogo yaliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko changamoto ambazo hatuwezi kunyamaza tusiseme. Changamoto hizo nimezipanga kwa idara, nianze na Jeshi la Polisi, huu ndiyo mhimili mkuu unaotegemewa na raia hapa kwa sababu wao ndiyo wamepewa kazi ya ndani ya ulinzi wa raia na mali zao, lakini Jeshi hili la Polisi halitoshi, kwani askari ni wachache kuliko raia wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi nyingine kampuni za sekta binafsi za ulinzi zinafanya kazi pamoja na Jeshi la Polisi kuendeleza ulinzi wa raia na mali zao. Hapa kwetu tuna makampuni mengi sana ya ulinzi, lakini kwa bahati mbaya sana makampuni haya hayana sharia. Nimekuwa nasimama mara kwa mara nikidai sheria, lakini kumekuwa na dalili ya kupindisha hiyo sheria kama ilivyo katika nchi nyingine, nchi nyingine kote kuna sekta za ulinzi binafsi na kuna sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sielewi kwa nini tatizo limetokea hapa la kutoleta sheria hiyo hapa Bungeni. Naambiwa sheria hiyo inaweza ikapinda ikawa ni uendelezaji wa maboresho ya Sheria ya Polisi. Mimi nasema kote duniani yalikotoka makampuni haya ya ulinzi au idea ya sekta ya ulinzi binafsi kuna sheria yake ya kuyaongoza makampuni haya na Tanzania hatuwezi tukawa na kisiwa. Sheria ya Sekta ya Ulinzi Binafsi ni lazima ije ili makampuni haya yanayoajiri mara tano, mara sita wingi wa Jeshi la Polisi yatusaidie kulinda raia na mali zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nikiongelea sasa hali halisi ya utendaji wa Jeshi la Polisi. Kumekuwepo na suala linalosemekana watu wasiojulikana na wenzetu wa upande wa Upinzani kule wamekuwa wanadai kwamba huenda watu wasiojulikana wanafanya matukio upande wa Upinzani tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina orodha ya maafisa na viongozi wa CCM waliofanyiwa matukio na watu wasiojulikana. Badala ya kulaumu kwamba watu wasiojulikana wanakuja upande wenu, nikiandika orodha ya watu waliofanyiwa matukio upande wa Upinzani hawafiki hata robo ya watu waliofanyiwa matukio upande wa CCM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikichukua tu watu wa CCM waliofanyiwa matukio upande wa Rufiji kule lakini hata jana Katibu Mwenezi…

T A A R I F A . . .

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ndiyo tatizo la watu kuwa na mawazo kichwani badala ya kusikiliza anachosema mtu. Mimi siongelei Jeshi la Polisi kukamata watu au kuua watu, naongelea watu wasiojulikana kufanya matukio. Mimi siongelei Jeshi la Polisi kufanya lolote, naongelea matukio yanayofanywa na watu wasiojulikana kwamba matukio hayo ni machache kwa upande wa Upinzani kuliko yaliyofanywa upande wa CCM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko haja sasa ya Serikali kuiongezea nguvu na uwezo Idara ya Upelelezi.

KUHUSU UTARATIBU . . .

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sijaongelea uraia wa mtu, wala chama naongelea watu wasiojulikana kufanya matukio. Watu wanaofanya matukio na hawakamatwi ndiyo ninachoongelea. Nasema Serikali ifanye juhudi kubwa ya kuiongezea nguvu Idara ya Upelelezi ili watu hawa wanaofanya matukio kwa pande zote mbili waweze kukamatwa. (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naongelea ombi langu kwa Serikali kuiboresha Idara ya Upelelezi ya Polisi ili iweze kuwakamata watu wasiojulikana wanaofanya matukio. Hiyo ndio message yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihamie upande wa magereza. Sisi tumetembelea magereza na mambo makubwa yanayotokea kule yanahitaji msaada wa Serikali. Changamoto kubwa tuliyoikuta kule kwanza ni makazi yao na vilevile wafungwa wengi wamerundikana katika magereza. Kwa hiyo, programu hii ya adhabu mbadala ni muhimu sana ikachukuliwa umuhimu wake ili kupunguza mrundikano magereza. Vilevile ni bora magereza wawe na kiwanda chao cha kutengeneza sare ili waweze kuwa na sare za wafungwa na sare zao wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumekuta upungufu wa chakula na yako madeni makubwa sana ya wazabuni wa chakula kwenye magereza yetu ambayo hayajalipwa na mbadala wake ingefaa kama magereza ingerudia mfumo wa zamani wakati sisi wadogo magereza walikuwa wakilima mashamba makubwa wakijilisha wao na kuuza chakula kwenye idara nyingine za Serikali. Kwa hiyo, napendekeza magereza wapewe uwezo wa matrekta ili waweze kufungua mashamba makubwa waweze kujilisha wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la zima moto. Zima Moto wana kazi kubwa kabisa ya kuokoa maisha ya raia na mali zao lakini hali ya jeshi hilo kwa sasa ni mbaya. Kwanza hawana vifaa vya kufanyia kazi lakini pia madawa ya kuzima moto hawana. Kwa hiyo, ningependa Serikali inapopanga bajeti yake iiangalie idara hii kwa macho mawili ili waweze kupewa kile ambacho kimepangwa katika bajeti ya kila mwaka. Kwa kufanya hivyo itasaidia kupunguza ukali wa upungufu wa Idara ya Zima Moto ili waweze kutusaidia yanapotokea majanga ya moto hasa mijini na maeneo ambayo ni sensitive sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la Idara ya Uhamiaji. Hivi karibuni kumekuwa na matukio mengi ya kukamatwa wahamiaji haramu hapa nchini lakini wahamiaji hawa wanapita katika nchi jirani. Mimi sielewi huko nchi jirani wanawaruhusu waje kwetu hapa kwa sababu sisi tunapata gharama kubwa sana kuwatunza hawa wahamiaji kwa maelfu halafu kuwasafirisha walikotoka na tukiwafunga magereza yetu yanafurika, lakini wanapita katika nchi jirani kule bila kusimamishwa. Inawezekana ni mkakati waende Tanzania kama ngao tu, ni gharama kubwa sana, kwa nini nchi jirani hawawazuii hawa wahamiaji mpaka waje wakamatwe hapa kwetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza sasa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi jirani wakutane wajadiliane suala hili la wahamiaji. Haiwezekani kila mwaka tukamate maelfu ya watu wanaopita katika nchi jirani wanakuja kukamatwa hapa kwetu, ni gharama kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefuatilia Idara ya Uhamiaji wanatumia hela nyingi sana kuwatunza lakini mahakama pia inachukua muda mrefu kujadili kesi ambazo sio za lazima. Kama kuna uwezekano wa kuongea na nchi jirani kwamba wazuiwe kule wanapoingia mpakani badala ya kuvuka nchi tatu waje wakamatwe hapa, ikiwa na sisi tutawaruhusu wapite itakuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa kuwa wanasema hawaji Tanzania wanaenda nchi fulani, wanapita transit hapa, kama hatusaidiani ujirani huu mwema basi na sisi tufunge mikono piteni, si wanapita tu bwana ila watakaobaki hapa tuwakamate. Kama wanapita waacheni wapite waende zao huko wanakotaka kwenda maana hakuna ushirikiano kati ya nchi na nchi. Hili ni tatizo kubwa sana na ni lazima Idara ya Uhamiaji isaidiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Idara ya Uhamiaji pia kwa hizi passport ambazo tulikuwa tunaziona kama ndoto ziko mikononi mwa wananchi wa Tanzania. Hili ni jambo zuri sana, nawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii moja kwa moja, ahsante sana.