Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa mwanzo jioni ya leo. Naomba Mwenyezi Mungu aniongoze niseme yale yenye busara kwa nia njema ya kuimarisha amani na usalama wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nataka nizungumzie kwenye ukurasa 46 wa hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri inayozungumzia usajili wa vyama vya kijamii na vyama vya kidini. Tunajua kwamba vyama na taasisi zote vinavyosajiliwa kwa mujibu wa sheria ya nchi hii vinakuwa ni vyama ambavyo vinatakiwa kufuata sheria ambazo zinawekwa chini ya usajili wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kidogo hapa niseme kwamba Serikali iwe makini sana hususan na taasisi za kidini, nimeona Mheshimiwa Waziri ameeleza kama kuna baadhi ya taasisi ambazo hawakuzipa usajili na naamini kwamba waliangalia sababu na wakajiridhisha kwamba hazifai kupewa usajili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu hapa ni kwamba, usajili wa taasisi za kidini lazima uendane na masharti kwa sababu nchi yetu haina dini; lakini Watanzania wana dini zao. Nasema hili nikirejea hoja yangu wakati wa hotuba ya Waziri Mkuu Mheshimiwa maneno ya mwanzo ambalo ni suala linanipa shida sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge ni wawakilishi wa wananchi. Si kwamba Mbunge anaposimama hapa anakuwa na yake tu, sometime anakuwa na mawazo yake lakini wakati mwingine anawakilisha. Mimi ni Muislam na naelewa tatizo lililopo sasa hivi. Tatizo ambalo nataka kulisemea ni kwamba taasisi za kidini zote zinapopata usajili wa aina moja lazima isiwepo taasisi ikajiona leo taasisi hiyo ni kubwa kuliko nyingine. Hilo kosa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hili kwa kutambua, kwa mfano sisi Waislam tuna taasisi nyingi na narudia kusema hivyo. Siku ya mwanzo niliyosema nashukuru Mheshimiwa Waziri alinijibu moja kati ya mawili la kusema kwamba hakuna tatizo kwa taasisi zozote kutumia ukumbi wa Bunge. Limeondoa masuala katika jamii kwa sababu lile jambo lililotendeka baadhi ya wananchi wengi walidhani ni jambo geni sana kwa Bakwata kufanya mkutano humu ndani, lakini baada ya ufafanuzi ule wananchi wametulia na wameridhika kwamba taasisi yoyote inaweza kuja na kufuata masharti na ikafanya vikao ndani ya Bunge, hakuna tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hili la kuifanya BAKWATA kuendelea kuwa ni wasemaji wakuu wa Waislam Tanzania, hili kosa! Kwa sababu Bakwata haina usajili wa aina yake. Leo tumemsikia, niliuliza swali kwa Serikali, nilitegemea majibu nipate kwa Serikali, lakini bahati mbaya sana nasema kwamba wametokea Masheikh huko wamenijibu na mimi sijaisema BAKWATA kwa ubaya. Nataka sheria na haki iwepo sawa kwa taasisi zote isitokee moja ikajiona kwamba wao ni juu ya wengine, hilo ni kosa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna hivi leo usajili wa vilabu hivi vya michezo hata Simba akiwa bingwa mara 10 hana mamlaka juu ya vilabu vingine. Hiyo ni club iliyosajiliwa kwa sheria sawa na vilabu vingine hali kadhalika NGO’s na vitu vingine. Kwa hiyo, naiomba Serikali bado itoe majibu ni sheria gani wanayoitumia kuitambua BAKWATA kama ndiyo chombo kikuu cha Waislam Tanzania? Nitashukuru nikipata hilo majibu na sitarudia tena kulizungumza hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ninalotaka kuzungumzia ni hali ya usalama ndani ya nchi. Kwa masikitiko makubwa sana, Taifa hili ndiyo lililokuwa nchi ya mstari wa mbele katika ukombozi wa Bara la Afrika. Kitovu na ndiyo tuliowapa makambi wapigania uhuru wa nchi mbalimbali kupigania amani za nchi zao, kwa sababu hawakuridhika na mateso.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, Mwalimu Nyerere hakuridhika na unyama wa Makaburu uliokuwa unafanyika Afrika Kusini. Alikuwa anaumia sana kwa matendo wanayotendewa Waafrika ndani ya Afrika Kusini. Leo tuliwapigania sisi tunarudi kule ambako tulikuwa tukiwapigania wenzetu. Mauaji ya kiholela, utesaji usio na tija, utekaji wa hovyo hovyo ndani ya nchi, tayari umeshamiri na unashika kasi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vitu vya kusikitisha sana. Ukisikia leo tumelala tumeamka salama hatujasikia sehemu kumetokea tukio ni jambo la kumwomba Mungu. Juzi wiki tatu zilizopita Pemba wameenda kuchukuliwa vijana sita na watu na magari yao na taarifa imetolewa kwa Kamanda wa Polisi kwamba gari zilizokuja kuchukua watu hawa ni namba hizi na zikafuatiliwa mpaka mamlaka wa usajili wa vyombo vya moto na kuonekana gari zile ni za watu fulani. Sasa hebu niambieni mpaka leo hakuna hata gari moja wala mtu mmoja aliyekamatwa kuhusishwa na tukio lile, tunakwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hilo tu! Pale Dar es Salaam lipo tukio lilitokea, mtu mmoja alienda akatekwa nyara, bahati wananchi pale Buguruni wakavamia gari wakalikamata, wakalipeleka kituo cha Polisi Buguruni na washtakiwa, lakini mpaka leo kesi hiyo haikwenda mahakamani na gari lile hatimaye liliachiwa, kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayalea matukio haya, lakini madhara yake yatakuwa makubwa sana baadaye. Kwa sababu uvumilivu wa watu unaweza ukawaishia. Leo kuna watu wanao majina wakipatwa na tatizo nchi nzima inaelewa, lakini kuna watu hawana majina. Mfano, miezi miwili iliyopita pale Zanzibar ameenda kuchukuliwa Mzee wa watu anaitwa Ali Juma Suleiman. Mzee wa watu amechukuliwa na vyombo, magari yanayojulika na watu wanaojulika, wakaenda wakamchukua nyumbani kwake mbele ya watoto wake, wameenda kumpiga siku ya pili kufa hospitali, hakuna anayezungumza, hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa limekaa kimya kwa sababu aliyekufa pale ni mtu hana jina. Hapa akifa mwanasiasa au watu mwingine ndiyo kidogo unasikia. Sasa matukio kama yale yanaleta hasira ndani ya jamii, taasisi iliyopewa dhamana ya kusimamia usalama wetu, badala ya jeshi la polisi kuwa usalama wa raia leo unajeuka kuwa uhasama wa raia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana suala la utekekaji wa kiholela unaoendelea, suala la matukito haya ya kuumiza watu kwa kweli sio masuala ya kibinadamu hayo ni masuala wanayofanya wanyama tena wale wanyama wanapokuwa na njaa ndio wanapokula mnyama mwenziwe. Sio katika hali ya kawaida, hawezi kufanya tukio kama hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi suala lingine niongelee suala la waendesha mashtaka. Juzi tumepata taarifa kama ndugu yetu Aquilina faili lake limefungwa kwamba limeishia limefungwa, kwa nini hatujui! Hata hivyo, upelelezi huu uliotumika haraka kufikia kufunga shauri la Aquilina kwa nini hauendi upelelezi huo katika mashtaka mengine mengi yaliyomo ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wametumia si zaidi ya miezi miwili kujiridhisha kama ushahidi haupo na wameamua kufunga lile jalada, hebu waniambie ni kwa nini leo miaka mitano, Masheikh wa Uamsho kutoka Zanzibar wameshindwa kufunga faili hilo wakati wameshindwa kupata ushahidi. Hebu watuambie lililoko nyuma ya pazia. Kwa sababu ubinadamu hisia za utu lazima zitujie sana, sote ni wazazi, sote tuna baba tuna mama, tuna watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna yeyote kati yetu humu kama ni baba yake wala ni mama yake au ni ndugu yake angeridhika kuona watu wale miaka mitano wameshikiliwa pasipo mashtaka yao kufafanuliwa wakahukumiwa kwa ajili ya kesi zao, hakuna! Kati yetu mmojawapo angekuwa mtu yule anamhusu hakuna, hisia za ubinadamu na utanzania ziturudie. Tuangalieni mateso wanayopata familia za wale, wake wawili wa Wazee wale waliko gerezani tayari wameshafariki. Hawakuonana tena na wapendwa zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaswali kila asubuhi kumwomba Mungu atupe baraka, sisi tuliopewa madaraka kuongoza Watanzania je, tunatenda haki kwa tunaowaongoza ili tupate baraka ya Mwenyezi Mungu? Huwezi kumwomba Mungu akujalie baraka wakati wewe umepewa mamlaka lakini hutendi kwa baraka kwa watu unaowaongoza. Vipi Mwenyezi Mungu atalihurumia Taifa hili. Tuongoze kwa dhahabu Afrika, kwa mifugo, kwa makinikia na mengine lakini kama hatutendi haki kwa tunaowaongoza Mungu hatatujalia baraka katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, suala la kesi ya Masheikh ya Uamsho ni suala ambalo linatukera sana Watanzania na wapenda haki wote na naamini kwa ukimya huu hata Bunge hili hawafurahii tena kuona suala hili la Masheikh wale wanaendelea kushikiliwa katika kipindi kirefu namna hii haiwezekani. Leo ikiwa tukio la kufa mtu Aquilina limechukua miezi miwili, tukio la Masheikh wale waliodaiwa magaidi hajakufa hata kuku ndugu zangu Wabunge. Hata kuku hakuuliwa katika tukio lile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko mifano ya nchi zinazotokewa na matukio haya. Ubelgiji pale palitokea tukio la kutisha airport na wapo watu walishikwa ndani ya miezi mitatu vyombo vya upelelezi vilijiridhisha kama watu wale hawakuhusika na waliachiwa huru mara moja. Leo tumefikwa na nini Watanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nataka kuwasemea ndugu zangu hawa wa Jeshi la Polisi, jambo la kuwapandisha vyeo hawa na wakashindwa kuwalipa stahili zao zinazolingana na vyeo vyao ni jambo linaloumiza sana. Leo askari anapanda miaka minne lakini bado marekebisho ya mishahara yake hayatekelezwi kwa nini? Miaka minne kwa nini? Wengine mpaka wafikia kustaafu na nyota begani lakini mshahara hauongezeki, what is this?