Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Arusha Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge ile biashara ya miongozo, miongozo wakati wangu bora muipunguze kwa sababu nataka niongee mambo serious.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo humu ndani wako viongozi wote wa vyombo vya ulinzi na usalama. Unapokuwa na viongozi ambao mshahara na cheo kwao ni msingi kuliko utu na thawabu, lawama wanazozipokea kutoka kwetu lazima zitaendelea kuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya Upinzani na Wabunge ilikuwa ni kutetea ustawi na maslahi ya Jeshi la Polisi, badala yake Wabunge ndani ya Bunge wanaliongea Jeshi la Polisi kama ni kikosi cha mauaji. Kama hawawezi kuiona hii sense kwamba Taifa limepotea kwamba Wabunge wote wa Chama cha Mapinduzi na opposition wakiongea wanalaumu Jeshi la Polisi na Jeshi la Polisi linalaumiwa kwa sababu tumeli-politicize. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo shughuli za siasa zimekuwa ngumu, mimi leo niko upinzani, kama lengo la demokrasia ni Mbowe, Lema na Mwambe na Mbatia na walioko huku, hawa watu wanaweza wakaamua kurudi kwenye biashara zao. Yeyote anayefikiria kuua demokrasia kwa sababu ya ushindi wa chama chake hampendi mjukuu wake. Wakijua msingi wa demokrasia hawawezi kutengeneza mkakati wa kisiasa wa kuua demokrasia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi siyo maadui, leo hatufanyi mikutano ya hadhara, leo vikao vya ndani vimezuiwa, Polisi wamepewa amri na kwa sababu wao wameapa kutekeleza amri leo kazi ya siasa imekuwa ngumu. Tukimalizwa sisi, tukaondoka sisi, hiyo vita itahamia ndani yenu, na nawaambia mwaka 2020 kwenye uchaguzi unaokuja kama sisi tutakuwa tumeshafukiwa, nyie hamtakuwa na kura ya maoni, mtakuwa na kura ya vidole, imeonekana Songea na sehemu nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulinda demokrasia haisaidii chama tawala inasaidia the next generation of this country. Leo wewe ni Mwenyekiti hapa alikuwepo IGP Mangu leo hayupo leo yupo Sirro na kwa utawala huu Mwigulu kesho anaweza yeye akajikuta amekuwa DC kama ambavyo Deputy DGIS leo ni RAS anaenda kukaa kwenye kikao ambacho RCO anakuwa boss wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wajifunze kwamba tunavyotaka kuhimiza demokrasia maana yake ni kwamba ni kwa ajili ya ustawi wetu. Mimi ni mchaga naweza nikaamua kuuza sumu ya panya, naweza nikaamua kuwa na hardware nikaachana na siasa. Siachani na siasa kwa sababu sifikiria uchaguzi unaokuja, nafikiria next generation. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, linda muda wangu, Katibu nakuomba linda muda wangu. Nyie mliopewa zawadi ya kurekodi naomba hii video yangu niipate baadaye kwa sababu siku hizi hamnipi video zangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nasema hivi Waheshimiwa Wabunge nyie mko wengi, nyie mna kura, nyie mna maamuzi, kuna Mawaziri huko wa nyanja zote saidieni hili Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kila mtu analia, tuna Mashehe Gereza la Arusha, tuna Mashehe Dar es Salaam, tuna Mashehe Songea, unapoweka viongozi wa dini kwa miaka minne bila kumaliza mashauri yao unajenga enemity ya kidini. Hawa watoto wao na wajukuu wao waliokaa kimya hawana maana kwamba wamekuwa wajinga, kuna siku wataamka na siku wakiamka itakuwa ni hatari sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kibiti nauliza lini tumeona Jeshi la Polisi limeita Press Conference ya kusema mambo ya Kibiti, watu wamekufa, watu wanapotea. Hawa watu walitakiwa wapelekwe Mahakamani, wasomewe mashtaka wahukumiwe, leo hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mkristo naogopa uadui unaojengwa kati ya Waislam na Wakristo wako Mashehe 85 karibu kule Arusha mwaka wa nne watu wamekatwa miguu, upelelezi haujakamilika. Huu uadui unaojengwa Waheshimiwa nyie mnaweza mkasaidia nchi hii, nyie mko wengi, kuna Mawaziri huku Maprofesa na namna ya kusaidia nchi hii ni kupuuza vyeo na mshahara against dignity. Dignity ni thawabu kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kesi ya kubambikizwa, mimi najua Mbowe alikuwa anapewa kesi ya mauaji, Halima anapewa kesi ya uhaini, kwa sababu gani! Hakuna Mbunge huku ambaye ana kesi. Kila siku unaona Jeshi la Polisi linapambana na vijana wadogo wa cyber-crime, kijana wa miaka 25 amemkosoa Rais mnakwenda mnamkamata. Mnawapa polisi mzigo ambao ni unnecessary.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ina matatizo mengi baharini, matatizo ya madawa ya kulevya, Sirro anaanza kukimbizana na mtu ame-twitt kwamba Rais Magufuli hafanyi vizuri. Msipomfundisha Rais kukosolewa hamuwezi kupata, mjifunze kukosoana, kukosoana ni tiba siyo balaa”.
KUHUSU UTARATIBU . . .
MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Jenista namshukuru kwa sababu pia amekuwa mtetezi wa Mwenyezi Mungu. Mungu akubariki sana, basi nahama kabisa. Sasa dakika 3 .6 nimetumia, Katibu usije ukaleta mambo yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokisema ya kwamba kuna matatizo makubwa katika Jeshi la Polisi. Nimesema wabunge wote hapa asilimia karibu 60 wana kesi, wote wana kesi, wote wapinzani wana kesi, sasa haya mambo yanaongewa na Wabunge lawama kwa Jeshi la Polisi. Jeshi la Polisi likiwa imara siyo kwa faida ya CHADEMA wala CCM ni kwa faida ya generation ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwa Mbunge ni thamani kubwa. Mbunge maana yake unawakilisha wananchi, unatunga sheria kuhusu nchi. Nilisema Bunge lililopita Wabunge wote mlioko hapa asilimia 70 hatukuwa wote term iliyopita. Tunapotunga, tunaposimamia maadili na integrity ya Jeshi la Polisi tushikamane pamoja kujenga jeshi imara ambalo hata kama wewe siyo Mbunge litakupa nidhamu, hata kama wewe siyo Rais litakupa nidhamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Jeshi la Polisi leo lina lawama nyingi, mimi nimekaa magereza miezi minne na siku 16 nimeona mambo ya kutisha. Nimeona watu wanaishia magereza, leo polisi kupata dhamana ni mpaka uka-apply habeas corpus Mahakamani. Leo polisi bail haipo, sasa kuna chuki inajengwa kati ya polisi na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo sababu leo Mheshimiwa Spika alisema mbona Sirro alivyotajwa makofi hayakupigwa upande huu? Siyo upande huu huko nje hawapigi makofi wakimuona polisi, kwa sababu gani, Marekani ukimuona polisi unaomba kupiga naye picha, hapa ukimuona polisi unakimbia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ninachosema ni kwamba Waheshimiwa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi nawaomba sana hakuna kazi muhimu tutakayofanya kama ya kujenga integrity ya Jeshi la Polisi. Ukiangalia undani kabisa Jeshi la Polisi wao wenyewe wanaharibiwa na sisi wanasiasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna uadui kati ya raia wa kawaida na Jeshi la Polisi. Unasikia mtu ameuawa Mbeya, mdogo wake Heche amepigwa kisu akiwa na pingu kwenye gari ya polisi, wanaenda kutupa mwili bodaboda ikaona. Boda boda imeona, watu wakasema, wakapiga kelele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado dakika tano, mimi zangu dakika 10 bado naangalia saa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yuko hapa IGP. IGP ushauri wangu ni huu mimi nimekuwepo Bunge hili nimeona Bunge hili likisema Sethi Harbinder zile pesa za IPTL zilikuwa ni mali binafsi. Nimeona Bunge hili hili wakisema asulubiwe, kabla jogoo halijawika mara tatu hawa watu hawa wanaokutuma kazi leo kuna siku watakuning’iniza, ushauri wangu ni huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwambia IGP, sio kila maelekezo ya kuumiza watu mnayachukua Mheshimiwa Lissu kapigwa risasi hapa, Naibu Waziri Kalamani anang’oa CCTV Camera kwake, kuondoa ushahidi. Ben Sanane kapotea, Azory kapotea, maiti zinaokotwa mchangani Mwigulu Waziri anasema hizi maiti zimeuawa na watu wasiojulikana. Kama wewe ni Waziri wa Mambo ya Ndani, kama kuna IGP maiti zinaokotwa zaidi ya elfu moja, huwezi kujua aliyeuwa unakaa ofisini kufanya nini, nenda kauze maandazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba integrity ya Jeshi la Polisi ni ya msingi kuliko chochote. Waheshimiwa Wabunge nawaambia...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)