Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Mwantum Dau Haji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia kuwa na hali ya uzima na afya kwa wakati huu na pindi hizi kusimama katika Bunge hili Tukufu ili kuichangia Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu wake kwa kazi zao nzuri wanazozifanya na kuzitekeleza katika masuala yao ya utendaji wa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachangia kuhusu suala la hali ya usalama barabarani, hali ya usalama barabarani ni nzuri na niwapongeze sana maaskari wetu wanafanya kazi nzuri, wanajitahidi kuifanya kazi hii ya barabarani lakini kuna suala la barabarani la kuhusu yale mataa. Katika vile vitengo vya mataa pale wananchi wanakuwa wanakasirika sana baadhi yao madereva. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taa zile zimewekwa pale ili kupitisha zile gari lakini askari wanatoka wanakwenda kusimama pale kuzipeleka zile gari kwa mikono na kasi, imekuwa wanaungana msururu mkubwa sana huku wa magari na muda mrefu sana watu wanapeleka wakati zile taa pale zipo zina kazi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumwambia Waziri kwamba lile suala walizingatie kwa kina wale askari. Hatutaki kwamba wasiwepo, wawepo maana wapo kwenye kutengeneza suala la usalama lakini wanapokuwepo pale wakae pembeni wangalie zile gari na zile taa zinazopitisha; kuna taa kijani, nyekundu lazima utajua hii nyekundu sasa hivi kule siendi lakini hii kijani ni yangu mimi lakini ndio ataposimama kuleta zaidi msongamano wa magari katika sehemu hiyo ya mataa barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie kuhusu mradi wa ujenzi wa majengo na vituo vya polisi. Nilizungumzia suala hili hapa katika Bunge hili Tukufu, nikalizungumzia suala la vituo vya polisi ambavyo havina hadhi na mpaka hivi sasa bado vituo havijawa na hadhi hasa katika Mkoa wa Kusini Unguja. Mkoa wa Kusini ni mkoa mama, Mkoa wa Kusini unajulikana kila kitu kwamba ule mkoa ni mkoa wa utalii lakini vituo vya polisi bado havijawa na hadhi na hili nililiomba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tena hii Wizara ya Mambo ya Ndani kwamba Mheshimiwa Waziri anasikia na Mheshimiwa Naibu Waziri nimshukuru kwamba alitembelea huu Mkoa wa Kusini lakini alikwenda akatembelea kuhusu suala la madawa ya kulevya, vile vituo navyo pia kaviona, hali ni mbaya. Vituo vya Mkoa wa Kusini, Wilaya ya Kati na Wilaya ya Kusini sio vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kusini, Wilaya ya Kusini kituo cha Paje bado hakijawa kituo na pale ukatarajia ni msafara mkubwa sana wa gari zinazokwenda kwenye suala la utalii. Wilaya ya Kati Jimbo la Chwaka kituo chao cha polisi wamejitahidi, niwapongeze. Wamejenga kwa nguvu zao wenyewe, hawakusaidiwa na Serikali wala na mtu. Kituo kipo kizuri, kinang’ara na hivi sasa hivi kinafanya kazi kituo kile, hakina wasiwasi. Akamatwe mwanamke kama hivi apelekwe mahabusu basi chumba chake kawekewa maalum cha kwenda kuhifadhiwa, Kituo cha Polisi kile cha Chwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nishukuru kwamba Kituo cha Polisi cha Makunduchi tayari sasa hivi kimeweka foundation, nishukuru. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri kwamba vituo hivi nilivyovitaja hapa ajitahidi katika kuviendesha na katika kutekeleza huu mpango wao waliouweka wa kuhusu utengenezaji wa vituo hivi vya kwenye mikoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nizungumzie kuhusu uboreshaji wa maslahi ya askari, maslahi ya askari bado hayajawa moja kwa moja mazuri, yanatoka lakini kuna askari ambao wanapandishwa vyeo, mfano koplo au sergeant, koplo yule anayepandishwa cheo kwenda u- sergeant basi bado maslahi yao yanakuwa yameganda kwenye ule ukoplo, hawajapata maslahi yao mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala nililileta mpaka kwenye swali langu la msingi , lakini bado sikuwa nimejibiwa lolote mpaka sasa hivi. Naomba sasa nilizungumzie hili suala, kwamba maslahi ya polisi wale ambao walikuwa wamepandishwa vyeo, u-sergeant na ukoplo, wafanyiwe haraka maslahi yao wanapopandishwa vyeo vyao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikuwa na mengi, nizungumzie hayo ambayo nimeyaweka ndani ya nafasi yangu na ndani ya moyo wangu kwamba niyatoe leo hapa katika Bunge lako Tukufu, naomba kuunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa ruhusa yako.