Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Zubeda Hassan Sakuru

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ZUBEDA H. SAKURU: Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu unalenga moja kwa moja katika changamoto ya masoko ya kilimo pamoja na bidhaa za kilimo. Wakulima wengi wanapata faida ndogo kutokana na ukosefu wa masoko na uhakika wa bei za mazao yao. Kushuka kwa shilingi mara kwa mara kumepelekea wanunuzi kununua mazao ya wakulima kwa bei ndogo sana na kumuacha mkulima akifanya kilimo cha hasara. Leo hii, ubovu wa miundombinu nchini unasababisha wakulima kukosa masoko ya uhakika na hivyo kupelekea kuuza mazao yao kwa hasara.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto za kilimo, Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ulialika wataalam wa kilimo ili kuchambua na kutoa mapendekezo juu ya namna bora ya kutatua changamoto ya masoko ya wakulima. Tena kuna maabara ndogo ya siku tano iliandaliwa ili kutathmini mifumo ya masoko kwa mazao ya mahindi na mpunga. Je, programu hii ilitoka na matokeo gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Serikali kupiga marufuku uingizaji wa sukari nchini bado ipo haja ya kuzuia pia uingizwaji wa bidhaa za mifugo nchini kama vile nyama, maziwa kwani wafugaji wengi wa Tanzania wanaendelea kuwa na mifugo mingi na uzalishaji hafifu. Leo pamoja na kuwa na Soko la Pamoja la Afrika Mashariki, Tanzania hainufaiki na fursa hizo hasa kwa bidhaa za maziwa na ndiyo maana leo katika maduka mengi ya rejareja bidhaa za nje za mifugo zimejaa na hazina ubora wala usalama kwa mtumiaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika sekta ya uvuvi hasa katika Bahari Kuu ya Hindi haujapewa kipaumbele kama mojawapo ya shughuli muhimu ya kiuchumi. Je, Serikali ina mikakati gani ya kuwezesha wavuvi wa Kitanzania kujishughulisha kwa manufaa na kuongeza pato la Taifa?
Mheshimiwa Naibu Spika, ripoti ya FAO ya mwaka 2014 inaonesha kuwa Uganda na Tanzania ziliongoza katika uvuvi wa maji baridi ambapo Tanzania ilishika nafasi ya nane. Changamoto kubwa ambayo ilitolewa kama tahadhari ni kupungua kwa samaki hasa katika maziwa makuu (Victoria ikiwa ndio mojawapo). Je, ni mkakati gani wa makusudi uliowekwa kuhakikisha uvuvi wa maji baridi unakuwa endelevu katika kuchangia uchumi wa Taifa?