Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Sixtus Raphael Mapunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. SIXTUS R. MAPUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilivyokuwa nasikiliza michango dhidi ya utendaji wa Jeshi la Polisi, ilifika hatua nikajiuliza kwa hizi sifa kwa nini tunakuwa na Jeshi la Polisi? Wamepewa sifa mbaya ambazo kwa kweli hawastahili hata kuendelea kufanya kazi. Nikajiuliza, kwa nini bado wanaendelea kuwepo? Pamoja na hizi sifa zinazotolewa dhidi yao, kwa nini bado wapo? Ikabidi nijipe homework kidogo ya kusoma na kujua kwa nini kulikuwa na Jeshi la Polisi? Kabla ya kuwa na utaratibu huu rasmi wa kuwa na vyombo vya Ulinzi na Usalama na kuwa na Serikali yenye mihimili mitatu inayojitegemea, dunia ilikuwa inaishi kama wanyama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwa wewe ukilima shamba lako, mtu anakuja anaswaga ng’ombe zako, anaondoka nao. Mbabe akikuona mtaani, akijisikia kukuchezesha makofi ya kutosha, anakupiga makofi ya nyota nyota, utaratibu ulikuwa hivyo. Baadaye dunia ikaamua kuja na Jeshi la Polisi likiwa na kazi tatu ambazo dunia nzima kazi za Polisi ni hizo. Kazi ya kwanza ni kulinda raia na mali zao; kazi ya pili, ni kuzuia uhalifu na uvunjaji wa sheria; na kazi ya tatu, ni kusimamia utekelezaji wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi kazi tatu ukiziangalia katika mtitiriko, karibu wote hapa tunaipenda sana kazi ya kwanza. Kazi ile ya kwanza ambayo ni kulinda watu na mali zao, kila mmoja hapa anapenda kulindwa; na kila mmoja hapa anapenda mali yake ilindwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya pili na kazi ya tatu ni ile kazi ambayo uhuru wangu unapoisha ndipo unapoanza uhuru wa mtu mwingine. Hapo tunatofautiana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikajiuliza, hivi hawa Askari wetu ni kweli wachache wana mambo ya hovyo, hivi kweli wote tunawapa lugha mbaya namna hii za kuwachoma, hatutambui mema yao hata kidogo? Walichofanyiwa Askari leo huku ndani kwenye mjadala ni ule msemo wa samaki mmoja akioza, wote wameoza. Ule msemo umepitwa na wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msemo wa siku hizi, samaki mmoja akioza, atolewe yule mmoja, waliobaki tunaweka ndimu, pili pili na chumvi tunawala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani Askari wote wakabebeshwa mzigo hapa ikaonekana ni watu wa ovyo kama hawafanyi kazi. Hivi leo, tukubaliane tu kimsingi hapa. Sirro aamue traffic wote leo Dar es Salaam ondokeni kwenye zile traffic lights. Kwa sababu kati ya kazi za msingi za Askari siyo ku-control zile robot, kuita magari. Taa zifanye kazi yake; lakini inafika kipindi, taa zinashindwa, Askari pale wanatusaidia. Siku ikitokea wote waondoke pale, kitakachotukuta, Mungu nisaidie. Au leo ondoa Askari wa doria wote, halafu Panya Road waingie barabarani, tutatafutana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kawaida sana ya kuwaona Askari ni wema pale wanapofanya yanayotupendeza, lakini pale wanapofanya kazi ya pili ambayo inawezekana imemgusa jamaa yako, imemgusa jirani yako; hata inawezekana hata mimi akaguswa mtu ambaye kanigusa sana, sitaweza kufurahi. Hiyo ndiyo hulka ya mwanadamu. Siyo kila mwanadamu hufurahia pale anapopata msukosuko wa kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba kwa Wizara ya Mambo ya Ndani pamoja na IGP afanye mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, anapojitokeza Askari akaenda kinyume na maadili na utendaji wa Askari, hatua zake anazopaswa kuchukuliwa ziwe tofauti sana na raia wa kawaida. Nafahamu kuna Askari wanachukuliwa hatua za kinidhamu kwenye Kambi zao, lakini inapofika mahali Askari anafanya uhalifu against raia, aina za hatua ziwe tofauti na umma ujulishwe kwamba nini yule Askari mkosefu alifanyiwa. Wakiendelea kuwapa adhabu za kule ndani, jamii haitawaelewa na ndiyo maana wanakuja kuambiwa samaki mmoja akioza, wote wameoza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana RPC wa Mara alivyoi-handle issue ile, ni issue mbaya sana. Unapokutana na Askari anamuua raia aliyemkamata, ni jambo baya, hatupaswi kulifurahia, hatupaswi kulichekea. Ila hatua alizozifanya RPC akasema tumemkamata, tumemfanyia moja, mbili, tatu na kesi inaendelea hivi na tumethibitisha hili liko sahihi. Sasa Askari, IGP ukiwaeleza Ma- RPC wako wote na Ma-OCD wa-handle suala kwa design hii hatutapata shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, nchi yetu inapakana na nchi nane. Kati ya hizi nchi nane tunazopakana nao hakuna nchi hata moja ambayo iko salama. Tafsiri yetu, usalama wa nchi yetu ni tenge, una matege, hauna miguu iliyonyooka. Nchi zote nane zinazotuzunguka ukianzia Kenya mpaka unakuja kumalizia Mozambique, hakuna nchi ambayo iko stable. Nchi zote zina chokochoko, zina mambo yasiyokuwa sawa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingine zina population iliyozidi kiasi kwamba ardhi haiwatoshi, nyingine zina njaa kali ambazo zinahitaji chakula. Katika mazingira haya, mikoa yetu ya mipakani ina hali mbaya sana sasa hivi. Kwa taarifa nilizozipata rasmi, Idara ya Uhamiaji tafadhali, wafanye kazi sana mipakani kuhusu raia. Mara baada ya kuona nchi yetu ina ardhi ya kutosha ya kulima na chakula kiko cha kutosha, jirani zetu wengi wameingia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tulipo- introduce elimu bure, kuna watu wameingia kwa sababu tuna jamaa zetu; nchi zote za mipakani haya makabila, kuna Wamakonde kwa ndugu zangu akina Bobali kule wako wengine Msumbiji. Ukienda Masai kule ndugu zangu wa Tarime wanapakana kule na Migori ni ndugu, ni jamaa tu wale. Kwa hiyo watu ku-cross ni kitu cha kawaida. Naiomba Idara ya Uhamiaji, sasa hivi ifanye kazi yake ya kukagua Uraia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, tumeitumia demokrasia vibaya na tumeshindwa kuitafsiri demokrasia vizuri. Demokrasia kwa asili yake haikuwahi kuwa ya Kiafrika. Demokrasia kwa asili yake haikuwahi kuwa ya Kitanzania. Demokrasia inatokana na maneno mawili ya Kigiriki na ndiyo wenye asili ya demokrasia; “Demons” inayomaanisha “people” na “Cratos” inayomaanisha “Power.” Kwa tafsiri nzuri na fupi “The people holds power.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya wanaoitazama demokrasia juu juu wameshindwa kujua vitu gani vinapima demokrasia. Kuna sehemu tunapima demokrasia inayoendana na watu ili tuthibitishe kweli hii demokrasia ni ya watu, ni pale ambapo kila Mtanzania anapochagua. Kwa hiyo, kipimo namba moja cha demokrasia na kuisema nchi hii ina demokrasia, yaani ina nguvu zinazotokana na watu, lazima kuwepo na election.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa election zinatofautiana. Kuna wengine wanachangua mtu, wengine wanachagua vyama, wengine wanakwenda winner takes it all, wengine wanakwenda PR System; kuna mifumo mingi duniani kutokana na mila na desturi. Sasa ninyi ndio mnajiamulia kwamba kwa mazingira yetu mfumo huu ndio unaotufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa kampeni za uchaguzi kupita kila kijiji ni mila na desturi za watu husika. Leo mnaweza mkauona huu mfumo unawafaa, kesho mkaona hauwafai. Tukumbuke kwamba unapoishia uhuru wangu, ndipo unapoanza uhuru wa mtu mwingine. Demokrasia nzuri ni ile inayotetea the right of individual. Unaposema the right of individual ni pamoja na kutokunikwaza, kwa nini haki yako wewe iwe kunikwaza mimi? Wewe unakuja na mkutano wako, mimi nasali. Kwa nini haki yako ilindwe, yangu isilindwe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwambieni ndugu zangu, nchi yetu anayefanya active politics hatujafika asilimia 10. The rest 90 percent hawana habari na siasa zetu hizi, active politics za Majimbo, hawana kabisa. Wao wanakwenda asubuhi kulima, wanakwenda kufanya kazi zao, wanarudi makwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo hili tukilichukua demokrasia kwa kisingizio cha upuuzi wetu na upumbavu wetu, hatupaswi kuwa watu wa namna hiyo. Tuisome demokrasia tuijue. Demokrasia nzuri ni ile inayoendana na mila na desturi za watu husika na ile inayolinda haki za mtu mmoja mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.