Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja hii ya Wizara ya Elimu iliyoko mbele yetu, pia naomba ni-declare interest kwamba mimi ni mdau wa elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianzie alipoishia dada yangu Mheshimiwa Bura kwa suala zima la TEHAMA katika shule zetu hasa za Serikali, siyo tu kwamba mtoto anaiona computer akiwa labda secondary, I mean O-Level pia hatuna mtaala wa TEHAMA katika kidato cha tano na cha sita, kwa hiyo kuna connection inakosekana hapo katikati kutoka kidato cha nne mpaka Chuo Kikuu, ninaiomba Wizara ya Elimu ione namna gani wataandaa mtaala wa TEHAMA wa kidato cha tano na cha sita ili watoto hawa waweze kupata muendelezo mzuri wa masomo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze sana Rais Dkt. John Pombe Magufuli, nimpongeze pia Waziri wa Elimu, Naibu Waziri na watendaji wote kwa kazi nzuri wanayoifanya tunafahamu kwamba changamoto ni kubwa, Tanzania ni kubwa na mahitaji ni makubwa hilo tunalitambua, tuseme tu kwa yale ambayo tayari yamekwishakufanyika kwa kweli binafsi kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu niendelee kuwapongeza, pongezi kubwa sana zimuendee Profesa Ndalichako najua anajitahidi sana na timu yake lakini yale ambayo bado hamjaweza kuyafanya ndiyo haya ambayo tutayasema na tunaendelea kuwaombea Mungu awasaidie ili muweze kuyafanikisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala zima la ufaulu wa wanafunzi kuanzia kwenye level ya primary kwenda sekondari. Ni kweli kwamba wanaomaliza shule ni wengi, lakini wanaofaulu kwa ufaulu unaotakiwa ni wachache, elimu ni uwekezaji tuwekeze sana kwenye elimu ili kwamba nchi yetu iweze kupona. Elimu ni uhai, elimu ni maisha nilikuwa nafikiri kwamba hata bajeti ya mwaka huu itakapoletwa kusomwa hapa badala ya kuwa na priority lukuki hebu tuanze na priority namba moja mwaka huu iwe elimu halafu tuone kama hatutaoka hapa tulipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila elimu bora nchi hii haiwezei kukombolewa, naomba niseme machache kupitia Wizara hii hasa Mkoa wa Manyara, wanafunzi wa shule wanaosoma katika shule za Wilaya ya Simanjiro na Wilaya ya Kiteto wanasoma umbali mrefu sana hizo ni Wilaya ambazo ni za kifugaji, watoto wanatembea mwendo mrefu kwa mfano pale Orkesment ile shule ndiyo inayotegemewa na Kata nyingi Kata za Kitwahi na vijiji vyake mtoto anatembea kilometa 20 mpaka 30 kwa siku, mtoto huyu akifika shuleni ni lazima atakuwa amechoka na hawezi kumsikiliza mwalimu vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ninaomba ile shule ina hosteli waongezewe miundombinu ya hosteli ili wale watoto wa kifugaji waweze kupata mahali pa kuweza kutulia na kusoma. Vivyo hivyo katika Kata za Ndedo na Kata zingine za Wilaya ya Kiteto. Wilaya hizi zimekuwa za mwisho muda mrefu katika Mkoa wa Manyara kwa sababu ya miundombinu yake ya umbali wa kutoka watu wanakoishi na shule ziliko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nizungumzie ufaulu wa Kidato cha Nne kwa miaka mitatu minne mfululizo, wanafunzi ambao wamekuwa wakifaulu kwa division one mpaka three ni wachache mno. Kwa miaka mitatu 2015 – 2016 - 2017 ni wanafunzi 95,000 tu kati ya wanafunzi zaidi ya laki moja wanaomaliza kidato hicho, ifike mahali tukae kama nchi tujadili mustakabali wa elimu nchi hii, vinginevyo kila siku tutakuja na huu wimbo na bahati mbaya sana ni hii tunatumia Sheria ya Elimu ya mwaka 1978, Sera ni ya mwaka 2014 hivi vitu havi-match ndiyo maana mambo mengi yanashindwa kwenda. Sheria iletwe, ibadilishwe, iendane na wakati tulionao sasa vinginevyo huu wimbo bora elimu na siyo elimu bora hautokaa uishe kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba sana Profesa Ndalichako atakapokuja hapa aseme ni namna gani sasa tutaondoa hizi zero nyingi na four nyingi kwenye matokeo haya ya kidato cha nne niliwahi kuzungumza hapa kwamba hivi tunachokifanya ni kuhakikisha mwanafunzi amemaliza
shule ama ameelimika? Kwa hiyo, niwaombe sana watu wa Wizara ya Elimu mtakapokuja hapa hebu mje na mkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kwa vile sasa hatuna ajira za kutosha niliwahi kushauri hata kwenye Kamati nilikokuwepo mwanzo ya TAMISEMI kwamba na niliwahi kuomba Wizara ya elimu pia tuweke mtaala wa ujasiriamali (entrepreneurship) kwenye elimu kwa sababu ni kweli hatuna ajira za kutosha ili wanafunzi wetu watoke wakiwa na skills, wale watakaokuwa wameshindwa kuendelea na masomo waweze kujiajiri ili kupunguza changamoto ya ajira. Siyo hivyo tu, ninajua kwamba Mheshimiwa Rais na Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikipambana sana na suala zima la rushwa, Biblia inasema: “Mfundishe mtoto katika njia impasayo naye hataiacha hata atakapokuwa mzee.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeomba mara nyingi ikiwezekena hata suala la rushwa na ubaya wake liwekwe kwenye mtaala ili watoto wafundishwe kuanzia kindergarten ubaya wa rushwa watakapokuja kuwa watu wazima kama sisi wanafahamu madhara ya rushwa, sasa hivi tunaongea na samaki mkavu ambaye ameshakuwa mkubwa unamkunja anavunjika, kwa hiyo, haisaidii, vile vitu ambavyo vinahitaji moral discipline viwekwe kwenye mitaala yetu ili kuweza kusaidia kuwajenga Watanzania ambao watakuwa wazalendo na nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie Chuo cha Ualimu Mamira kilichopo Mkoani Manyara. Chuo kile ni chuo cha Grade A, wameomba kuanzisha diploma pale kwa maana ya waweze kuwekeza kwenye Walimu wa wa sayansi tu, ombi lao nina hakika lipo kwenye meza ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, wameomba walimu kama watano wa sayansi ili waweze kuwafundishwa walimu wa diploma wa sayansi ili kuweza uondokana na upungufu wa walimu wa sayansi tulionao, ninaomba ombi hilo kama inawezekana lishughulikiwe haraka ili mwaka huu waweze kusajili walimu wa level ya diploma na tuweze kuendelea kupunguza huo upungufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wa sayansi ni kilio nchi nzima; naomba kushauri kwamba badala ya ku-split hizi effort ndogo ambazo zinafanywa na Serikali, kwa vile shule ziko nyingi hususani shule za kata za Serikali kama inawezekana shule chache ziwe identified kama ni ni kila Wilaya tuwe na shule mbili sinazo-deal na sayansi, maabara zake ziboreshwe na walimu wa sayansi wapelekwe kwenye shule hizo badala ya kuhakikisha kila shule inafundisha sayansi wakati walimu wa sayansi hatuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna upungufu wa zaidi ya walimu 26,000 wa sayansi, walimu hawa wanastaafu, wanabadilisha taaluma, wengine wanafariki, kwa hiyo itatuchukua zaidi ya miaka 15 mpaka kuhakikisha tunapata walimu, juhudi za makusudi zinahitajika kuhakikisha kwamba kupanga ni kuchagua, kwa hiyo, tuchague kwamba shule kadhaa zifundishe sayansi na shule zingine ziendelee na masomo mengine ili kuweza ku-utilize walimu tulionao badala ya kuzalisha zero za sayansi kila mwaka, ifike mahali sasa tufikiri nje ya boksi.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisemee kwa haraka shule ya watoto walemavu ya Katesh A iliyopo Wilayani Hanang’, shule ile ina watoto walemavu wapatao zaidi ya 150 na ni shule ya mchanganyiko kuna watoto wasio walemavu pia. Shule ile ni kama imesahaulika sana, pale kuna watoto wenye albinism wanapata shida, hawapati yale mafuta kwa ajili ya ngozi zao, miundombinu ya ile shule ni kama imesahaulika kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri aweze kuangalia namna gani wale wanafunzi wa ulemavu tofauti kwenye shule ya Katesh A pale Hanang’ waweze kupatiwa msaada ili na wao waweze ku- enjoy masomo yao kama watoto wengine wasio na ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme suala la ukaguzi. Ni kweli kwenye kudhibiti ubora tunaona wapo Wadhibiti Ubora wengi lakini zaidi wamekuwa wakidhibiti ubora kwenye private schools wanasahau kudhibiti ubora kwenye shule za Serikali. Ukiona shule hizo wanazosema ni za private zinafanya vizuri ni kwa sababu wao wamejikita zaidi kwenye kudhibiti upande wa pili badala ya shule ya Serikali ambazo pia ndiyo nyingi. Automatically mtu mwenye shule binafsi yeye mwenyewe ni mdhibiti namba moja, maana hakuna anayetaka ku-invest kwa hasara.
Kwa hiyo, wao wange-focus zaidi hata kwenye shule za Serikali maana watoto wetu wengi wako kule na mengi hayafanyiki kule. Ninawaomba sana watu wa ukaguzi wapatiwe vifaa kama walivyosema wenzangu kama ni bodaboda hizi ama pikipiki kwa ajili ya ukaguzi ili waweze kuzifikia hizo shule, shule ni nyingi na miundombinu ni…
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.