Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Kasuku Samson Bilago

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Buyungu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la Teachers Professional Board (Bodi ya Kitaaluma ya Walimu). Bodi hii iliwahi kuandaliwa Muswada na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwenye utawala wa Awamu ya Nne na kuiwasilisha Serikalini ili iweze kufanyiwa mchakato wa kuunda chombo hiki. Mpaka sasa chombo hiki hakijaundwa pamoja na malengo yake mazuri kabisa, kusimamia taaluma ya walimu nchi hii pamoja na nidhamu ya walimu wa nchi hii. Kwa mfano, lengo lilivyokuwa zuri la Teacher’s Professional Board ikitokea mwalimu wa nchi hii amefanya makosa akafukuzwa kazi anaendelea kwenda kufundisha shule za private and nobody will ask him or her! Lakini lengo la hii Teacher’s Professional Board ilikuwa inaandaa leseni pamoja na vyeti vya ualimu unapewa leseni ya kufundishia. Uki-mess up wanakunyang’anya leseni, hautafundisha shule yoyote katika nchi hii. Kwa hiyo, nimuombe Waziri hiki chombo kiundwe kama zilivyo Bodi za Taaluma zingine kiweze kulisaidia Taifa hilika katika upande wa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni suala la ufaulu wa wanafunzi katika Taifa hili. Kidato cha nne, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamati nilitarajia Wabunge wote wawe wamesononeka sana juu ya hali hii na ingekuwa inaruhusiwa kusimama Bungeni kama kwenye msiba kwamba tusimame kidogo kumuombea marehemu nalo tungesimama kwa suala hili kuiombea elimu nchini, lakini watu waliposoma ni data tu, wanaziona data tu, sawa tu walifaulu hawa sawa tu! Hapana! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo hapa, shule binafsi mwaka 2016 shule 10 bora zilikuwemo asilimia 10 za Serikali. Katika shule 50 kulikuwa na asilimia sita za Serikali; shule 100 asilimia 11. Mwaka jana katika shule bora 10 zilikuwemo za Serikali asilimia sifuri. Katika shule 50 asilimia moja katika shule 50 ni za Serikali, shule 100 zilikuwemo asilimia sita. Maana yake elimu ya Taifa hili imebebwa na shule binafsi. Shule za Serikali hakuna chochote. Tungeondoa private hapa tungekuwa na wanafunzi sita mwaka jana bora ndani ya wanafunzi mia moja! Halafu tunashindwa kuisaidia Serikali na kuisimamia iboreshe elimu. Hili halikubaliki! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungewauliza watu wa shule binafsi wanafanyaje? Hii kitu Waziri mngeenda tu mkanong’ona nao, ninyi mnafanyaje mnapata performance nzuri kama hii, sisi huku tumekwama, hebu mtusaidie. Siri yao wamesema hivi, kuna motisha ya kutosha kwa walimu, Serikalini hakuna motisha. Shule za Serikali walimu hawana motisha yoyote, hata madai yao wanayodai hawalipwi kwa wakati, madaraja hayapandi hata wanaopandishwa hawarekebishiwi, wanaorekebishiwa hawalipwi arrears, mnatarajia nini? Shule binafsi wanao walimu wa kutosha, sisi kila siku hatuna walimu na tumepigia kelele ndani ya ukumbi huu, walimu hawatoshi shuleni, tunaliona jambo la kawaida! Hivi hiki kitu tunakwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetoa walimu wa sekondari tumepeleka primary, tumeenda kuongeza frustrations kwa walimu. HakiElimu walituambia asilimia 37 ndiyo wamebaki na morale ya kufundisha, hawa 60 na kidogo hawana morale kabisa! Ualimu siyo kitu cha kusema lazima utafundisha tu, haiwezekani! Morale kwanza, itoke moyoni na kutoka moyoni lazima huo moyo uwe umetengenezwa ukubali kufundisha kwa bidii na nguvu zako zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine, shule binafsi wana kitu wanaita mfumo imara shirikishi wa udhibiti elimu, mfumo wao imara una mkakati wa kukaririsha wanafunzi wanaofanya vibaya ili wasiendelee na makapi.

Sasa nataka Waziri utakapokuja hapa utuambie ni kwa nini unazuia shule private zisikaririshe? Kwa sababu mimi ni mzazi nimeamua kumpeleka mtoto wangu private, hata angekaririshwa mara mia naendelea kulipa karo, Serikali inawahusu nini? (KIcheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niacheni na mtoto wangu nikomae naye mpaka nitakapojiridhisha kwamba viwango vyake vya elimu vimekuwa vizuri na hili mwisho wake ndilo linalosababisha, tumejiuliza kwa nini Serikali ina ugomvi na private, ni wivu tu! Wana performance nzuri, kwa hiyo, ni kama inaidhalilisha Serikali. Kwa hiyo, lazima wivu uwepo ili na wao ufaulu ushuke wote mfanane, muende mnafanana fanana. Matokeo yake sasa ufaulu ukiharibika kwenye shule za private tunaanza kupeleka watoto Uganda na Kenya wakati hii biashara ilikuwa imekwisha. Ziko shule hapa zinafanya kama Uganda kama Kenya na zaidi ya hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu wivu uishe, Serikali iachane na wivu, shule za private ziachwe zi-perform, wakaririshe, mwanafunzi atoke ni the best student. Sisi tunataka wote waende. Subirini muziki utakaokuja wa hii elimu bure! Matokeo ya elimu bure yatakuwa zaidi ya haya tutashangaana wote. Tumeweka elimu bure miundombinu imebaki ile ile, hatujajiandaa vizuri, maana batch ya kwanza nadhani mwaka kesho au kama mwaka huu ya kidato cha nne yenye elimu bure, tutashangaana hapa. Kwa hiyo, tusijifiche kwenye kichaka cha elimu bure tukidhani iko bomba. Tuangalie elimu bure inafanana na miundombinu tuliyonayo? Inafanana na tunachoweza kubeba kwenye elimu bure? Inaweza kutusaidia zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la walimu wa sayansi, nimepata taarifa walimu waliosoma masomo ya art wamepelekwa Chuo cha Kleruu kwenda kujifunza methodology ya kufundisha shule za ufundi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie hii, walimu waliosoma masomo ya arts baada ya kuona wamezidi kule sekondari wamewachukua wakaenda kusoma methodology ya kufundisha practical shule za ufundi. Wamekwenda Iyunga Sekondari, wame- prove failure kwenye BTP wameshindwa! Sasa niambieni hivi mimi nimesoma history, geograpghy labda HGL, HGK, mimi na metholodgy ya sayansi wapi na wapi? Nikajifunze namna ya kufundisha kutengeneza gari, namna ya ku-operate viwanda, eeh, hii kiboko! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siri nyingine masomo ya lugha, kiswahili na kiingereza Tanzania yanaanza kufundishwa darasa la tatu. Hawa shule za private wanaanza chekechea kule na wakitoka chekechea hawa walioanza la tatu wanakwenda kukutana kwenye mtihani wa darasa la nne, wale walioanza… (Makofi/Kicheko)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)