Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Rashid Mohamed Chuachua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Masasi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi nashukuru sana kwa kupata fursa ya kuchangia kwenye eneo letu hili la elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa juhudu kubwa inazofanya kwenye sekta hii, pia kwa namna ya kipekee nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Profesa Ndalichako kwa kazi kubwa anayoifanya katika elimu pamoja na watendaji wake wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila nilipokuwa ninasimama kwa ajili ya kutoa mchango kwenye wizara hii muhimu nimekuwa nikizungumza kuhusu non formal na adult education, yaani elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi. Nina hamu sana ya kuiona Wizara ya Elimu, kisera ikiwa inatambua kwamba ina jukumu la kuwaelimisha Watanzania wote bila ya kuzingatia wale tu ambao wako madarasani kwa sababu Watanzania wote wanategemea wizara hii ili kupata elimu kwa namna moja ama nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapozungumza hili ninaiona kabisa Serikali yetu ilishaamua kuiunda taasisi maalum ambayo itafanya kazi ya kusimamia elimu nje ya mfumo rasmi pamoja na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Hapa ninaitaja Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na ninaitaja hii kwa makusudi kwa sababu miongoni mwa majukumu yake ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanajua kusoma na kuandika hata kama wako nje ya madarasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwango cha kutojua kusoma na kuandika kinaongezeka sana kwa wananchi wa Tanzania. Katika kipindi kilichopita katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alilisimamia sana hili la kuhakikisha kwamba ni lazima kumuelimisha kwanza mtu mzima halafu mtoto baadaye kwa sababu mtu mzima tunamtumia sasa hivi wakati mtoto tuna muda wa kusubiri kumtumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema, ukiangalia Ripoti ya Adult Literacy Survey ya mwaka 2014 inaonesha kwamba kutoka mwaka 1986 Watanzania asilimia 9.6 walikuwa hawajui kusoma, lakini sasa katika mwaka 2012 wameongezeka mpaka asilimia 31, sasa leo ni mwaka 2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima inao mkakati ambao inapanga kuutekeleza, mkakati huu unaitwa National Literacy and Mass Education Strategy. Huu ni mkakati madhubuti waliouandaa kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma pamoja na kutoa elimu na hamasa maalum kwa wale watu ambao hawajui kusoma na kuandika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuishauri na kuiomba sana Serikali kwanza iangalie Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, lakini pia ihakikishe inatoa mchango mkubwa katika kuhakikisha utekelezaji wa mkakati huu unakwenda mbele ili Watanzania waweze kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo lingine ambalo ni lugha, nimekuwa nikisema kila siku. Kama kuna jambo ambalo linatatiza mfumo wetu wa elimu ni lugha tunazozitumia. Hili lazima niliseme wazi. Ukiwasikiliza baadhi ya wataalamu wanaozungumza kuhusu elimu wanazungumza kuhusu tatizo kubwa la ufaulu katika sekta yetu ya elimu, lakini wanapozungumza jambo hilo hawazungumzi kama tuna mkanganyiko mkubwa sana katika matumizi ya lugha, hawasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisikiliza ripoti za TWAWEZA, ukiwasikiliza Haki Elimu pamoja na mashirika mengine wanaofatilia michakato ya kujifunza katika mfumo wetu wa elimu hawasemi wazi kama tuna tatizo kubwa la matumizi ya lugha. Hakuna nchi yoyote duniani iliyoendelea na kupata mafanikio makubwa katika sekta ya elimu kwa kutumia lugha za watu wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili mimi nalisema wazi. Ninaweza nisieleweke kwa sababu hata pengine wasimamizi wa mfumo huu tumepita katika mfumo ambao bado kwetu ni kikwazo. Kwa hiyo, ukiambiwa leo tujifunze kemia au fizikia kwa kutumia kiswahili utaona shida lakini kujifunza kemia au fizikia kwa kutumia kireno, kifaransa, kichina, kijerumani tunaona inawezekana. Kwangu mimi hili ni tatizo kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hakuna lugha iliyo bora kuliko lugha nyingine, na hii ni kwa mujibu wa Profesa Noam Chomsky ambaye ni mtaalamu wa isimu ya lugha, anasema hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lugha ndiyo inayotufundisha namna ya kutazama na kuutafsiri ulimwengu wetu. Hakika tuna mkanganyiko mkubwa. Leo hii katika zile shule ambazo wanatumia lugha ya kiingereza kujifunza kuanzia darasa la kwanza mpaka darasa la tatu hautakiwi kugusa kiswahili. Katika shule wanazotumia kiswahili kama lugha ya kufanyia mawasiliano ya kujifunza hawatakiwi kugusa kiingereza mpaka wanafika darasa la tatu. Lakini wakifika darasa la nne wanafanya mtihani mmoja hawa wanafanya kwa kiingereza, hawa wanafanya kwa kiswahili, lengo letu ni nini? Lengo letu ni kuwashindanisha wanafunzi kwenye umahiri wa lugha au kuwashindanisha wanafunzi kwenye umahiri wa maudhui ya masomo yetu! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana katika jambo hili na ni lazima Serikali ifike wakati wa kufanya maamuzi magumu. Mimi nataka nikwambie kama Serikali inaamua leo, kwa mfano wanafunzi wajifunze kwa kutumia lugha yetu inawezekana kabisa wakajitokeza watu wakasema tunataka tusisaidie mfumo wa elimu ya Tanzania kwa sababu tunaondokana na kujifunza kwa lugha ya wakoloni, hili ni jambo gumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikwambie kwamba ni vyema sasa hivi tukafikiria namna bora ya kujifunza, kwa sababu watoto wetu wana kikwazo kikubwa sana katika kujifunza wanajifunza kwanza kukielewa kiingereza halafu wanajifunza kuelewa maudhui ya somo. Lakini hivi ni kitu gani kinaweza …

T A A R I F A . . .

MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kukataa ni kwamba ni Wabunge wote na Mawaziri wote, lakini wapo ambao watoto wao wanasoma katika mfumo huo wa kukwepa kiswahili na kwenda kwenye kiingereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme jambo moja, kwamba umefika wakati wa Watanzania kufanya maamuzi. Tunawaweka watoto wetu katika mfumo wa lugha ya kiswahili mpaka wanafika darasa la saba, tukitoka darasa la saba tunakwenda form one mpaka form four tunabadilisha ghafla wanasoma kwa kiingereza, halafu baadaye wanakwenda tena chuoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nchi gani duniani inafanya mambo haya? Tumebakiwa ni nchi za kiafrika ambazo tunalazimika kutumia aidha kifaransa au kiingereza kwa sababu ni lugha ambazo tuliachiwa. Tufanye maamuzi, nchi nyingi ambazo zimeendelea wanatumia lugha zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningependa kuwe na chombo maalum kitakachoangalia na kusimamia mfumo wetu wa ubora wa elimu, hili ni tatizo pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema ukweli kabisa ni kwamba zipo shule binafsi ambazo zinaanzishwa na zinasimamiwa vilivyo na Serikali ili kukidhi mahitaji, lakini pia tunazo shule za Serikali ambazo nazo pengine zingeweza kusimamiwa na chombo kinachojitegemea ili kuziongezea ubora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo lazima tufike wakati wa kuona tuwe na chombo maalum ambacho kinaangalia pia shule zetu za Serikali, kwa sababu shule za private kukiwa kuna walimu watatu kuna uwezekano wa kusema tunafunga shule, lakini katika shule za Serikali ili ku- maintain ubora wa elimu mimi naishauri Serikali ione umuhimu wa kuwa na independent board ambayo inaweza pia kuzisimamia shule hizo. Lengo ni kuondoa pia matabaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna matabaka makubwa wapo watoto ambao wanaonekana wanasoma shule bora sana wanatumia lugha bora sana lakini wapo watoto ambao wanaonekana wanasoma shule za chini sana. Ili kuondoa haya matabaka pia kingekuwepo chombo kinachoweza kuiangalia Serikali na kuisimamia ili tuweze kwenda vizuri na shule zetu pia nazo ziwe shule bora kama ilivyo katika shule zingine za private.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno haya nashukuru sana naunga mkono hoja.