Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Abdallah Majurah Bulembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mimi pia nimpongeze Profesa Waziri wetu, Naibu wake, Katibu Mkuu, watendaji wote na Wakurugenzi walioko Wizarani pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze na sehemu moja Serikali yangu wakati inakuja inipe majibu. Nianze kwenye muundo huu ambao ni sera ya shule za msingi na sekondari ambapo wanafunzi wanatakiwa hawa walioanzia mwaka 2015 tangu sera imetungwa wataenda mpaka darasa la sita. Lakini hapo nyuma mwaka 2014 kuna wanafunzi nao ambao wanamaliza mwaka mmoja huo huo. Kwa hiyo, tuna watu wawili mara mbili, wengine wa darasa la sita wengine wa darasa la saba kutokana na muundo mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ninalolipata Serikali yangu imeshajiandaa kuwapokea hawa wanafunzi watakaomaliza la saba na la sita wote kwenda sekondari kwa mara moja? Kwa sababu hawa wanafunzi watakuwa wengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mtindo huu kwa hawa walioanza kwa maana ya mwaka 2015 wanaoishia la sita na hawa wa mwaka 2014 wanaoishia la saba, sijui mtafanyaje? Tunawapokeaje? Shule tunazo, maandalizi mmenza rasilimali watu na walimu wa kufundisha? Kwa sababu ni double, kwa sababu wamemaliza hawa na hawa wamemaliza, mtihani ni huo huo mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo napata tabu kidogo kwa maana sijui, maana mwaka 2020 tuna mambo mengi, kuna uchaguzi, tuna mambo gani, kuna wanafunzi wengi wanamaliza wenye mitihani miwili la sita na la saba kwa wakati mmoja. Naomba Serikali ijipange kidogo na ikija hapa inipe majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili ni kuhusu suala la elimu. Ndugu zangu Awamu ya Tano kwenye elimu bure ni suala linaloenda kumuangalia mtoto wa maskini, si la bahati mbaya na elimu hii sio wale ambao mmezaliwa ninyi kwenu mnasoma tu, wale watoto wa wavuvi, watoto wa wakulima wasisome, hapana. Awamu ya Tano inaposema elimu bure ina maana huyu mama mpika kitumbua hawezi kulipa mtoto wake asome. Ndiyo dhamira ya Serikali iliyopo, kwamba kila mtoto anayetakiwa kwenda shule na aende na iko wazi, walivyosema elimu bure wametoka milioni moja wameenda milioni mbili, hiyo ni picha halisi inayoonesha kwamba tunao wengi waliokuwa wanabaki nyumbani bila kwenda shule kwa sababu ya mambo ya kulipa, naipongeza Serikali yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kuna watu wanasema elimu imeshuka, elimu sijui kufanya nini, mimi nakataa. Nakataa kwa sababu zifuatazo, nitakataa wewe una miaka 20 mimi nina 57, lazima nikatae. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakataa kwa sababu, zifuatazo; sisi miaka yetu ilikuwa unafanya darasani mtihani vipindi vitano, kila kipindi marks 50. Ukipata marks 244 huendi sekondari, kwa sababu shule hazipo, lakini wale wazazi ambao walikuwa na uwezo akikupeleka private na huyu aliyeshinda kwenye kijiji mtu mmoja mkienda form four wote mnakutana kwenda high school; miaka hiyo ambayo watu hawataki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kila mwaka ukienda watoto wanaendelea kuzaliwa na changamoto ya elimu inaendelea, idadi inaongezeka, haiwezi kufanana. Unalinganisha na nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kila kitu ni historia, historia inakataa kwamba mwalimu fulani aliposoma kwa sababu madarasa yalikuwepo na shule zilikuwa chache wanaenda wachache. Leo hii ukienda elimu ya juu watoto ni kama 150,000 wanaoenda kwenye vyuo wanadahiliwa na wanalipiwa na Serikali, lakini miaka ile walikuwa labda 20,000, sasa tutalinganishaje? Ndio maana nawapa Serikali yangu tahadhari kwamba kuna kitu kinaongezeka hapa. Mnapodahili watoto wa la saba wakawa wengi, je, miundombinu tumeongeza? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi naipongeza Wizara ya Elimu kwamba mnachokifanya ni sahihi na elimu iko vizuri. Marekebisho lazima yawepo, hatuwezi kutoka mbinguni, lakini kuna rafiki yangu mmoja amesema pale kwamba lakini watoto wa Wabunge wanasoma nje, okay, wako watu wanasomesha watoto nje, lakini mtoto wa dada yake je? Wa mjomba wake je? Kwa hiyo, tunapoongelea elimu tunaongelea kwamba elimu ya watu wote sio ya watu baadhi ambao wamechaguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na watu ambao wamelisemea suala la lugha. Mimi nafikiri tufikie mahali Serikali ifanye maamuzi na maamuzi yenyewe yawe magumu tu. Kama tunaanza chekechea mpaka form five mpaka form six ni kiswahili, iwe kiswahili basi. Kwa sababu mtoto ili aweze kujifunza ni lugha gani anatokanayo nyumbani kwao. Hakuna mzazi ambaye ana mtoto akishajifungua ameanza kutambaa akaanza kizungu, ninyi wa mjini ndio mnafanya hivyo, lakini wa vijijini wote ni kiswahili, sasa tunakikwepaje kiswahili kwenda kujifunza lugha za watu wengine? Ndiyo lugha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na leo kiswahili kina nafasi kubwa ulimwenguni, watu wanaotaka kujua kiswahili ni wengi, wanaokuja kujifunza kwetu ni wengi, tunakiogopa kwa nini? Serikali mimi nasema biashara ya kizungu mtakutananayo huko Ulaya, hebu tuamue kwamba tunataka Kiswahili kutoka chekechea mpaka chuo kikuu, dhambi ni ipi? Kwa nini tunakwepa chetu? Fanyeni maamuzi tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuna watu wanasema kweli kiswahili ni kigumu, lakini ni kwa sababu hatufundishwi tunakiongea tu. Wakija wenzetu wanakuja kujifunza kiswahili wanajua fasihi, wanajua fasaha, wanajua nini. Kwa hiyo, Serikali yangu iamue kwamba lugha iwe ni fulani kufundisha kuanzia chekechea mpaka chuo kikuu, sio aibu. Mbona tukienda mikutano ya kimataifa kila mtu anawekewa lugha yake mnaelewana? Kwa nini sisi tunaogopa kiswahili kwa sababu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende Mkoa wa Kagera; Mheshimiwa Waziri Kagera pale tumeona mnadalili za kujenga Chuo cha VETA, pesa mnazo, watu kila siku wanazunguka. Naomba wakati kwa majibu yenu, mnaanza lini na mabilioni mmeshapewa yako benki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wamesema pale watoto wanamaliza la saba hawana mahali pakwenda. VETA ingekuwepo, Mkoa mkubwa kama Kagera ingesaidia sana hawa wazazi. Tunawaomba sana, suala hili la elimu jamani tuhurumieni wengine, Mkoa kama Kagera kwenye karne hii VETA haipo, pesa mnazo mmekaa nazo Wizarani. Pamoja na tunawapongeza, lakini mnatuumiza, haiwezekani. Kama pesa zipo si watu waanze, tatizo ni nini? Naomba wakati Waziri unarudi hapa kuja kuleta majibu uje vizuri maana sisi wengine! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, michango..., Dakika tano au kumi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, michango shuleni. Kuna shule nataka kushauri tu; kuna shule ambako kule michango tumeiondoa, lakini watoto wengine walishazoea kunywa uji, wengine kula mchana, kule kumeporomoka sana, watoto hawarudi shuleni. Hamuwezi kuja na mawazo mapya kwamba pamoja na kwamba michango bure kwenda shule na na nini, lakini ile ambayo wazazi wanafanya kwa hiyari mkaipa nafasi ili angalao watoto wao wasishinde njaa wakapata hata uji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu shule za kwetu kule vijijini kuna hamasa nyingi ambazo watoto wanaenda shule. Akishika kikombe asubuhi anawahi shuleni anaenda, lakini akishajua na uji haupo na mchana hamna chochote hali inakuwa mbaya. Tumeamua tusichangishane, lakini je, ile michango ya hiyari nayo ni migumu? Mtufafanulie kidogo tujue maana tukienda huko nje tunaulizwa maswai mengi na maelezo mengi yanakuwa hayapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, juzi hapa niliuliza maswali hapa kuhusu Vyuo vya Michezo, nikajibiwa haraka haraka na wapenzi wenzangu wale wa michezo. Hebu Wizara ya Elimu mtuambie, zilikuwepo shule kama Butimba ambazo ni special kwa sababu ya elimu ya michezo tu. Ziko nyingi, zilikuwepo shule kama Korogwe, vilikuwepo vyuo kama flani, kwa nini mmezuwia michezo isiendelee shuleni? Kwa nini? Kwa nini hili suala mnaliondoa? Hawa watu watafundishwa wapi? Naomba mnipe majibu mazuri kwenye suala la michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viko vyuo vilienda Wizara ya Habari ambavyo navyo vinachechemea, lakini ninyi kwa sababu ni fani yenu, turudishieni vyuo vyetu. Kama mlikuwa na crush programme imeisha, lakini suala la wanamichezo kupata mahali pa kusoma ni la muhimu sana.

Sasa msije mkatuambia kuna UMITASHUMTA, kuna UMISETA, lakini vyuo havipo, mmevifunga havifundishi, masomo haya darasani hayafundishwi michezo mmeondoa, kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nawaombeni sana suala la michezo msilifanyie mchezo. Suala la michezo ni ajira.

T A A R I F A . . .

MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa siipokei sana kwa sababu inawezekana mwenzangu hata tangu mwaka umeanza hajagonga passport, kwa hiyo, sio tatizo sana. Lugha ziko nyingi, watu hana anayesafiri na lugha moja ya kizungu kuna nchi zinaongea kiarabu peke yake, kuna nchi zinaongea kireno, kiitaliano, hawajui kiingereza chenu hiki, kiingereza kiko kwenu huku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa namalizia kwa kusema kwamba mimi kwenye michezo, bado naendeleo huko huko, Wizara ya Elimu mrudi mjipange, muangalie vyuo vyetu vilivyokuwa vinafundisha michezo mturudishie ili taaluma hii isipotee, lakini tukiwa na walimu ambao wanajua kucheza, akipiga mpira ndio mtaalam, haitusaidii katika nchi. Tutaacha kizazi ambacho hakiwezi kucheza na utamaduni ule ukipotea Taifa linapotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naishia hapo, naomba kuunga mkono hoja.