Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Martha Moses Mlata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nashukuru kwa kupata nafasi hii ili niweze kuchangia hoja hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na pongezi. Pongezi hizi nazipeleka kwa Mheshimiwa Rais kwa kauli yake ya kuhakikisha kwamba elimu bure kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne. Tumeona mafanikio makubwa ya watoto ambao walikuwa wamekaa majumbani wanashindwa kwenda kuandikishwa kwa sababu ya fedha ambazo zilikuwa zinatakiwa shuleni. Baada ya tangazo la elimu bure sote tumeshuhudia mafuriko ya watoto waliokwenda kujiandikisha. Wapo wanaobeza kaulimbiu hii ya elimu bure wakifananisha na kwamba Serikali haikujiandaa, lakini nataka kupongeza kwa sababu Mheshimiwa wewe ulikuwepo tulipoanzisha shule za sekondari za kata, angalia sasa hivi ukienda kwenye vyuo vikuu vyetu watoto wa shule za sekondari za kata ndiyo waliojaza vyuo vikuu vyetu hapa nchini, hayo ni mafanikio makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili uweze kufanikiwa ni lazima uamue na uthubutu ili uanze. Changamoto zinazojitokeza ndiyo mafanikio yenyewe. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba nikupe moyo, kazi ni nzuri, tuendelee, tuwachukue watoto wote, asiachwe mtu nyuma eti kwa kisingizo kwamba elimu bure inawajaza watoto bila huduma kwa sababu Serikali haikujiandaa. Serikali mmejiandaa na wananchi wamejiandaa, nimeshuhudia kwenye Mkoa wangu wa Singida, nipende kuwapongeza Wabunge wote wa Majimbo ya Mkoa wa Singida wamejitahidi sana na Madiwani wote wa Mkoa wa Singida wameweza kusimamia ujenzi wa kuongeza madarasa ya wanafunzi hawa walioongezeka na watoto wako madarasani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi upande wa shule za kata nimeshapongeza na watoto sasa hivi wako vyuoni wanaendelea na masomo isipokuwa naomba niishauri Serikali kuanzishwa kwa shule maalum kwa ajili ya masomo ya sayansi. Hatuwezi tukazifanya shule zote zikawa na masomo ya sayansi kutokana na upungufu wa walimu tulionao. Kwa hiyo, cha msingi ni kuanzisha shule maalum ili walimu wale wapelekwe kwenye hizo shule ambazo tutakuwa tumezianzisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka nizungumzie suala la mikopo ya elimu ya juu. Mheshimiwa Waziri amezungumzia ni namna gani wanafunzi ambao wamebainika ni wadaiwa sugu takribani 147,000 na ukasema 42,000 ndiyo wameonesha nia ya kutaka kuchangia, sasa mimi naomba niulize, hawa wengine 103,000 au 100,000 wako wapi? Je, wana ajira ya kuweza kulipa? Kama hawana Serikali inaweka mkakati gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali kwamba wanafunzi wetu hawa tunaowakopesha wanapomaliza elimu ya juu tujitahidi wapate ajira, tuwasaidie ili waweze kurudisha mikopo yetu kwa sababu wakibaki mitaani watashindwa kurudisha mikopo yetu. Pamoja na kwamba watatakiwa wakidhi vigezo, lakini bado wanafunzi hawa watambulike hata kwenye Halmashauri zetu kwa sababu kuna mikakati ya ule Mfuko wa Vijana, Wanawake na Walemavu wanaweza wakawezeshwa kwa sababu tunasema uchumi wa viwanda, wawezeshwe waweze kujiajiri wenyewe, Serikali iwafuatilie, isiwaache hivi hivi, iwasaidie ama waajiriwe ama waweze kujiajiri wenyewe.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo nilisimama siku moja hapa nikaomba mwongozo kwamba wanafunzi wanapo-qualify kupata mkopo iwe ni nusu au asilimia 100 cha kushangaza wanapofika vyuoni wanasumbuliwa sana. Inatakiwa walipe wanasema advance payment ambayo inawasumbua sana watoto wetu. Kumbuka watoto wengi wanaotaka mikopo ni watoto wa wakulima wetu, waliosoma shule hizi za kata, baba auze nyanya, mahindi au asubiri auze alizeti kwa mfano kule Singida au vitunguu, unakuta zile fedha hazitoshi, anapofika kule anateseka.

Mimi nina watoto ambao walifika mpaka vyuoni leo hii wamerudi kwa sababu walishindwa kulipa ile advance payment ya shilingi 600,000. Naomba jambo hili Mheshimiwa Waziri utakaposimama hapo utufafanulie umelichukuliaje na Serikali inasemaje ili tuwanusuru watoto wetu hawa ambao wanakwenda kuteseka, itawakatisha tamaa wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli naomba nimpongeze sana Profesa Kikula, mimi nilikuwa Mjumbe wa Kamati ya Huduma za Jamii, wakati tunakwenda kukagua maeneo ya kaunzishwa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, tulipofika kule kwanza magari yetu yalikuwa hayawezi hata kupita wakati tunaukagua ule mlima, tukasema hivi ni nani atakayekabidhiwa kuja kusimamia chuo hiki ili kitambulike na kiwe chuo bora? Tunamshukuru Rais wa Awamu ya Nne alimteua Profesa Kikula, wakatafuta pesa, Serikali ikakijenga kile chuo ambacho sasa hivi tunajivunia kwamba ni chuo kikuu ambacho kinachukua wanafunzi wengi sana.

Mheshimiwa Waziri mimi sifahamu wewe kwenye Wizara yako, huyu Profesa angepata award kwa sababu aliweza kusimamia vizuri sana pamoja na changamoto zote ambazo zilikuwa zinajitokeza pale, amesimamia vizuri sana. Hakuna ubadhirifu wa pesa, kwa hiyo, mimi kwa kweli nimeona leo nimpongeze Profesa Kikula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwenye upande wa shule za kata bado kuna changamoto kubwa sana kwa watoto wetu wa kike. Watoto wetu wa kike wanakaa mbali, wanapopangiwa kwenye zile shule wanakwenda kupanga kwenye nyumba za watu wanapata changamoto kubwa sana ya masomo. Wengine wanashindwa kuendelea na masomo kwa sababu wanakatishwa tamaa, miluzi ni mingi sana kwa watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali hii ianze kumjali mtoto wa kike, zijengwe hostel kwa ajili ya kumhifadhi mtoto wa kike. Sikatai kwamba na mtoto wa kiume anapaswa alindwe, lakini bado kwa mtoto wa kike hali ni ngumu sana, anasoma kwenye mazingira magumu sana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana uangalie suala la hostel za watoto wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kuna suala la vyoo mashuleni. Tumegundua watoto wa kike wamekuwa wakiadhirika sana kwa sababu shule nyingi bado hazina vyoo vya kutosha na fedha ziko kwako siyo TAMISEMI. Kwa hiyo, naomba sana fedha zitolewe kwenye shule kwa wingi kwa ajili ya kujenga hivi vyoo lakini ramani ile ya vyoo lazima iwe na choo kinachoweza kumsitiri mtoto wa kike anapokuwa kwenye siku za maumbile ya mtoto wa kike ili aweze kusitirika kwa sababu walio wengi wanakata tamaa hata kwenda shuleni. Akishapitwa ile wiki moja anapokuja wiki ya pili kwa kweli anakuwa amenyong’onyea sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishie hapa, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, aluta continua, tuko pamoja Mheshimiwa Rais, kaza buti, tafuta pesa, tunajua unatafuta pesa ili shule zetu ziweze kuwa za standard, tupate walimu wa kutosha lakini zile shule pia hebu zipekelewe visima vya maji ili kuwe na maji ya kutosha kwenye shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana.