Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi.

Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima na afya njema. Naipongeza Serikali kwa bajeti nzuri waliyoiwasilisha mbele ya Bunge lako tukufu kwa mustakabali wa elimu ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, iwapo bajeti hii itatekelezwa ipasavyo tuna imani kubwa kwa Watanzania kunufaika na mfumo wa elimu ya sasa. Hata hivyo kuna maeneo ambayo yanahitaji kutiliwa mkazo ili kuhakikisha tunayaboresha na pia vilevile kukuza kiwango cha elimu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mafanikio makubwa ambayo yamefikiwa kwa kipindi kifupi katika sekta ya elimu lakini bado kuna changamoto ambazo Serikali inatakiwa kuzipatia ufumbuzi. Eneo la kwanza ambalo ningependa Serikali ilifanyie kazi kwa haraka ni uhaba wa walimu na miundombinu isiyokidhi mahitaji kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi nchini ukiwemo Mkoa wangu wa Singida kuna uhaba mkubwa wa nyumba za walimu. Kwa mfano, kwa Mkoa wa Singida pekee una uhaba wa nyumba za walimu 1,986 jambo hili linasababisha walimu wengi kuishi uraiani ambako hakuna utulivu na pia linawavunja moyo wa kuweza kuwafundisha wanafunzi wetu inavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu cha hotuba ya Waziri wa Elimu ukurasa wa 89, TEA imetenga shilingi bilioni 9.7 kwa ajili ya kazi mbalimbali zikiwemo ujenzi wa nyumba za walimu, mabweni pamoja na matundu ya vyoo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mkoa wa Singida upewe kipaumbele kwani una uhaba mkubwa wa nyumba za walimu, vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo. Vile vile Mkoa wa Singida unakuwa kwa kasi sana na Jiografia yake ni ngumu na maeneo mengi hayafikiki kwa urahisi. Kwa mfano shule ya msingi ya Mangoli iliyopo Jimbo la Manyoni Mashariki ipo umbali wa kilometa 137 kutoka Manyoni Mjini. Shule hii ni nyumba moja ya mwalimu yenye vyumba viwili, imepelekea kuvunjika kwa ndoa za walimu hao kwani upande mmoja wanalala wake zao na upande mwingine wa nyumba hiyo wanalala walimu hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali hii kweli walimu wetu wataweza kuwafudisha wananfunzi kwa umakini?

Mheshimiwa Ndalichako nakuomba ulichukulie suala hili kwa umakini mkubwa kuweza kuhakikisha nyumba za walimu zinapatikana kwa wingi. Pia naishauri Serikali kuharakisha ujenzi wa nyumba za walimu, mabweni pamoja na matundu ya vyoo na uende sambamba na ujenzi wa vyoo unaozingatia sehemu za kujihifadhia wanafunzi wa kike wanapokuwa katika siku zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine lenye changamoto kubwa ni uhaba wa walimu na hasa wa masomo ya sayansi katika shule za sekondari. Kwa kuwa nchi yetu kwa sasa inaelekea katika uchumi wa viwanda, na tunahitaji kuzalisha wataalam wengi ambao watakuja kuviendesha viwanda hivi, ningeomba Serikali ilichukulie jambo hili kwa umakini mkubwa. Kwa mfano kwa Mkoa wa Singida tu una uhaba wa walimu wa sayansi 660 katika shule zetu za sekondari na kwa upande wa shule za msingi kuna uhaba wa walimu 3,947 kwa masomo ya sayansi na sanaa. Naishauri Serikali iangalie utaratibu wa uhakika wa kuzalisha walimu ili kwenda sambamba na mipango ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa mkakati wake wa kusambaza vifaa vya maabara katika shule zetu za sekondari, ni mpango mzuri na ninaomba uwe endelevu. Kwa kuwa kwa mwaka 2017/2018 kuna shule za sekondari kwa Mkoa wa singida ambazo hazijapata vifaa vya maabara ninaomba Serikali iangalie jambo hili basi ipeleke vifaa vya maabara katika shule zetu za sekondari kwa Mkoa wa Singida. Ninawapongeza sana wananchi wa Mkoa wa Singida kwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa maabara na pia vilevile ninaiomba Serikali iweze sasa kuona umuhimu wa kumaliza maabara zile ambazo zimefikia maeneo ya lenter.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba Serikali iuangalie kwa jicho la tatu Mkoa wa Singida kwani una uhaba mkubwa sana wa vyumba vya madarasa. Kwa shule za sekondari tu kuna uhaba wa vyumba 122 na kwa shule za msingi kuna upungufu wa vyumba vya madarasa 4,849.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitumie fursa hii kuwashukuru Kampuni ya Tanga Cement ambao wamekuwa msitari wa mbele kusaidia jamii kuboresha miundombinu ya elimu. Ahsanteni sana Tanga Cement na nawaomba muendelee na moyo huo huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naipongeza Seriakli kwa mkakati mpya wa kuwasaidia vijana ambao wako mitaani kupata mafunzo ya ufundi kwa njia ya vocha kupitia Bodi ya Mikopo na Mkoa wangu wa Singida ni miongoni mwa Mikoa minne ambayo imeanza kutekeleza mpango huo. Lakini changamoto iliyopo ni kwamba fedha za mafunzo ya ufundi kwa vitendo kutoka bodi ya mikopo hadi sasa bado hazijapelekwa. Ningeiomba Serikali ifanye haraka kupeleka fedha hizo kwa kuwa vijana hao zaidi ya 200 wapo stranded na sasa hawasomi kwa vitendo masomo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nawapongeza Mheshimiwa Ndalichako, Mheshimiwa Ole Nasha na timu yake kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu. Nawapo moyo, endeleeni na moyo huo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.