Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Nichukue nafasi hii kuunga mkono hotuba ya Waziri, aliiwasilisha vizuri na nimpongeze na nimtake asife moyo kwani Roma haikujengwa kwa siku moja. Hizi changamoto na mambo mengine yote yanayozungumzwa kwa maana ya kuchangia na kushauri ayachukue kama ni sehemu ya changamoto kuweza kuyafanyia kazi. Kama ambavyo nimesema Roma haikujengwa kwa siku moja basi mtaendelea kuyafanyiakazi kadri siku zinavyokwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze yeye Waziri pamoja na Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii ya Elimu kwa kazi nzuri ambayo wameendelea kuifanya. Wizara hii ni ngumu na ni nzito, lakini kwa sababu imekabidhiwa kwa Profesa na ndiyo maana hata Mheshimiwa Rais inawezekana aliona kwamba amkabidhi Profesa Mama Ndalichako kwa sababu amebobea katika masuala hayo ya elimu anaweza akasaidia kuendelea kuiboresha elimu katika nchi yetu hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi ya kumshukuru sana na kuishukuru hii Wizara. Shule ya Korogwe Girls ilipata tatizo la kuunguliwa na bweni, lakini walipopata taarifa waliweza kuja kutushika mkono, wakatusaidia na kuhakikisha kwamba lile bweni linarejea ili kuusudi watoto waweze kukaa na kuendelea na masomo, tunawashukuru sana kwa huduma ile mliyotupatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niendelee kushukuru vilevile kwamba shule ile ni kati ya shule ambazo ni shule kongwe ambazo zimepewa fedha za ukarabati. Nalo hilo naendelea kushukuru, tunashukuru sana, isipokuwa labda niombe tu kwamba shule ile ya Korogwe Girls ipo katikati ya Mji wa Korogwe na ni shule ya wasichana. Sisi wenyewe tumeanza kwa jitihada zetu kujenga uzio ili iweze kuwa ndani humo hasa ilizingatiwa kwamba ni watoto wa kike wale lakini humo ndani kuna wenye ulemavu Waziri mwenyewe unafahamu. Nilikuwa naomba sana Mwenyezi Mungu akupe wepesi katika haya nitakayokuomba ikiwezekana mtusaidie angalau tuweze kumaliza uzio wa shule ile ili watoto wale wa kike waweze kukaa mle ndani. Eneo lile ni kubwa sana kwa maana ile kazi tuliyoianza sisi wenyewe tutashindwa kuimaliza, kwa hiyo ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri ulione hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa hotuba yake ya jana pamoja na kwamba inawezekana wengine haikuwapendeza lakini kwa maelezo yake mazuri jinsi nilivyokuwa nimemsikiliza mimi, nimeamini kabisa kwamba ana nia nje na Serikali hii, ana nia njema na
wananchi wake wa Tanzania kwahiyo nampongeza kwa hotuba ile aliyoitoa hasa pale alipozungumza kwamba wako wafanyakazi ambao wamepandisha madaraja lakini walikuwa hawajalipwa zile stahiki zao sasa watalipwa. Ziko stahiki za wafanyakazi ambazo zilikuwa hazilipwi sasa zitalipwa, hiyo ni hatua nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaiomba Serikali kwamba sasa madeni yote yanayohusiana na wafanyakazi maadam Mheshimiwa Rais ana nia njema itakapofika wakati madeni hayo yote na stahiki zao zote waweze kulipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la Shule ya Sekondari Semkiwa ambayo Mheshimiwa Waziri ulikuja ukaiona pale, tuliaku lika ukaja kuweka jiwe la msingi, kwa maana ujenzi wa bweni ambalo sisi tulitumia nguvu zetu na tukalijenga lile bweni kwa ajili ya watoto wetu wa kike. Wazazi wanakushukuru sana Semkiwa. Baada ya kuona ile jitihada ukatusaidia kutupa fedha kwa ajili ya ujenzi wa bweni lingine shilingi milioni 75.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda vizuri Mwenyezi Mungu anatusaidia na tuna uhakika kwamba tutalimaliza na ikiwezekana sasa uje ufungue rasmi yale mabweni yote mawili kwa jitihada zako zile ambazo umeweza kututembelea pale na kuweza kutuongezea. Ila nikikumbushe tu Mheshimiwa Waziri kwamba ulituahidi pale vitanda na magodoro pale lile bweni ilikuwa ni vitanda 48 na magodoro 48, kwa lile bweni ambalo tulikuwa tumeshalijenga. Ni matumaini yangu kwamba utatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikuombe tena Mheshimiwa Waziri kwamba nina Shule ya Sekondari Mgombezi iko nje ya Mji wa Korogwe, ina vijiji sita. Nina shule ya Chifu Kimweri iko nje ya Mji wa Korogwe, ina vijiji vitano. Watoto wa kike wanatembea kilometa nne mpaka tano kwenda shule tena kwenye makatani, mnajua kule kuna mkonge, kwenye mkonge mule kwenda shule na kurudi, nilikua naomba sana. Kwa mfano Mgombezi, kule Mgombezi tayari tumejenga bweni moja, sasa kama utatusaidia kutuongeza bweni lingine ili watoto wa kike hawa waweze kukaa na kusoma wakiwa pale shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hii ya Chifu Kimweri tumeshaanza kujenga bweni. Nimuombe Mheshimiwa Waziri kwa shule hizi mbili ambazo zina umbali mrefu wa watoto wa kike kutembea, niwaombe sana, mimi najua Mwenyezi Mungu atakupa wepesi tu katika haya ninayoyasema ili angalau uweze kunisaidia hizi shule mbili ambazo ziko mbali sana nje ya Mji watoto wa kike waweze kusoma vizuri.

Mheshimiwa Nwenyekiti, suala la upuandishwaji wa madaraja; mimi nashukuru zoezi hili sasa linamuelekeo sasa kuendelezwa. Sasa niombe basi mna ile tabia ya kuwapandisha madaraja halafu hamuwapi zile fedha kulingana na madaraja yao. Niombe liende sambamba, mtu akipandishwa daraja basi liende sambamba na haki yake ile anayostahili kulipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakusudia kuanza kujenga Chuo cha VETA pale Korogwe, tuna eneo kubwa sana kule Mgombezi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.