Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Rhoda Edward Kunchela

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Katavi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongea kuhusu miundombinu. Miundombinu katika shule za Serikali ni mibovu na ndiyo inayosababisha wanafunzi kufanya vibaya katika shule za Serikali. Ziko changamoto nyingi katika elimu ya Tanzania. Elimu bure, mabweni, upungufu wa vitabu shuleni, walimu kupunguzwa na nyumba za walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhana ya elimu bure Serikali hii ya Awamu ya Tano imekurupuka vibaya na imesababisha matokeo mabaya. Ukiangalia gharama za kumnunulia uniform mwanafunzi, chakula, malazi, umbali na changamoto za familia hususan vijijini unakuta mtoto anasafiri umbali wa kilometa 20 kufuata shule na akifika shule kachoka, ana njaa na anawaza atarudije kwao baada ya masomo kwa umbali huo na huku usalama wake huo ni wa hofu kiasi hicho. Mnawafikiriaje wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu kama hayo hususani vijijini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri maslahi ya walimu yazingatiwe, nyumba za walimu wa shule za sekondari na msingi bado hali ni mbaya na usalama wao vijijini. Hii imesababisha walimu kukosa morale/motisha wa kufundisha kwa moyo kwa sababu ya changamoto hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu shule ya sekondari ya Wasichana Mpanda, shule hii ya wasichana haina uzio na ukizingatia eneo lililobaki kuzunguka shule ni pori na kuna wanyama aina ya viboko kipindi cha usiku huzunguka kwenye mabweni na husababisha wanafunzi kuishi kwa hofu hapo shuleni. Shule ya Mpanda Girls imezungukwa na wafanyabiashara, stand ya magari ya mizigo na biashara za wajasiriamali hivyo usalama wa wanafunzi hawa umekuwa mdogo na wa hofu. Waendesha magari makubwa kuweka stand hii pale imesababisha wanafunzi kupata mimba kutokana na mazingira yaliyopo, ni mabaya. Hivyo Serikali izingatie jambo hili la kuweka uzio ili usalama wa wanafunzi uimarike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu wanafunzi wenye ulemavu. Shule za Msingi Azimio, Kasahato na Nyerere zilizopo katika Manispaa ya Mpanda zimeelemewa mzigo wa wanafunzi walemavu na bado wana changamoto za madarasa ya kufundishia watoto hao, wanafundisha katika madarasa yasiyo na madirisha. Je, Serikali inawasaidiaje watoto hawa pamoja na walimu ambao kimsingi wanafundisha katika mazingira hayo magumu na vitendea kazi pia havitoshi? Serikali ina mkakati gani wa kumaliza matatizo haya ya wanafunzi walemavu na vifaa vyao husika?