Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza kuongelea Bodi ya Mikopo. Ili kuweka tija na kuondoa malalamiko ya mara kwa mara ya mikopo kwa wanachuo, nashauri Serikali izingatie suala la Bodi ya Mikopo kuwa na revolving fund ambapo fedha hizo zisiwekwe Mfuko Mkuu ili Bodi iweze kuwekeza na kutunisha mfuko ambao utasaidia kuchangia gharama za kuendesha taasisi na baadae Serikali itaondoka katika kutoa fedha kuwezesha Bodi hii. Hivyo basi, Serikali itoe fedha kwa Bodi na kuwezesha revolving fund kufanya kazi ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri Bodi iwe chini ya Wizara ya Fedha. Kwa kuwa Bodi inahusika na masuala ya fedha ni vema ikawa chini ya Wizara ya Fedha ili kupata msaada zaidi wa kitaalamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mashirika ya misaada, kwa kuwa kuna taasisi nyingi za kiraia na mashirika ya kimataifa ambayo yanahusika kusaidia masuala ya elimu na ufadhili, je, Bodi ya Mikopo inashirikiana vipi na taasisi hizi ili misaada pia ipitie kwao kwa watu wenye uhitaji maalum?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili napenda kuongelea kuhusu sera, sheria na kanuni. Sheria iliyopo ni ya tangu mwaka 1979 ambapo imekuwa ikifanyiwa marekebisho nyakati mbalimbali, lakini sera zake bado hazijafanyiwa maboresho ili kuendana na sheria. Nashauri Serikali ipitie upya sera zake ili zikidhi mahitaji ya sasa kwa kushirikisha wadau wa elimu na ndipo sheria iboreshwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu ni kuhusu mitaala, kumekuwa na mabadiliko katika mitaala, nashauri Serikali iangalie ufanisi wa mitaala kwani mabadiliko yamekuwa hayakidhi uhitaji na kumekuwa na mkanganyiko kwa watumiaji. Hivyo, nashauri Serikali isimamie mitaala na vitabu ambavyo vitakuwa muhimu kwa watoto shuleni kulingana na umri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne ni kuhusu usajili wa shule za Serikali. Serikali ina wajibu mkubwa kutoa elimu nchini na sasa elimu bure. Tatizo ni kuwa TAMISEMI bado ina changamoto ya bajeti na kuhusisha wananchi kujenga miundmbinu ya shule na watoto wa vijijini ndiyo wanapata shida kufika shule zilizo mbali kati ya kilometa sita mpaka 14. Tatizo kubwa na vigezo vya usajili na kusababisha shule zinazojengwa na wananchi kukosa sifa. Nashauri Serikali ipunguze masharti kwa shule za Serikali, iwe angalau na vyumba vinne, matundu sita ya choo, nyumba moja na ofisi moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano ni vyuo vya elimu na shule za mazoezi. Tanzania kwa sasa vyuo vya ualimu vipo vingi kwa ngazi za cheti, diploma na shahada lakini wahitimu wanaotoka shule au vyuo hivyo wamekuwa hawana uwezo wa kuridhisha katika utaalam, ujuzi na maarifa. Hivyo, nashauri Serikali itoe mwongozo kila chuo kikuu kiwe na shule ya mazoezi mfano mzuri ni wahitimu wa DUCE wapo vizuri sana kwa kuwa wana shule ya mazoezi. Mpango huo unaweza pia kushushwa ngazi za chini yaani diploma na cheti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita ni kukariri darasa. Nashauri mfumo uboreshwe ili kusaidia watoto kufaulu pia kuwezesha kuendelea na masomo. Jambo la kuangalia ni kwa kiasi gani mitaala hii inachangia watoto kukariri darasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa pongezi kwa Serikali na Wizara na watendaji kwa kazi wanazoendelea kufanya.