Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Hamoud Abuu Jumaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuwa hai mpaka leo hii, na kuniwezesha kufika mahali hapo salama na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya Bajeti ya Wizara husika ya mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara kwa kuandaa Bajeti nzuri yenye mrengo wa kimaendeleo na uboreshaji wa sekta zote muhimu zinazohusiana na Wizara hii, sekta ya elimu, sayansi na teknolojia. Bajeti hii inakwenda kutekeleza mipango mbalimbali iliyopangwa kufanyika katika Awamu hii ya Tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kuendelea kutoa elimu bure nchi nzima kuanzia shule za awali mpaka kidato cha nne. Hii ni hatua nzuri inayopaswa kupongezwa kwani idadi ya watoto wetu wanaoanza shule imezidi kuongezeka maradufu. Hatua kama hizi zinahitaji kupongezwa na kuishauri Serikali pale panapojitokeza changamoto ili Serikali iweze kuboresha na watoto wetu waweze kupata elimu bora yenye tija kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna changamoto kubwa sana kwa upande wa walimu wa masomo ya sayansi, aidha, upungufu huu unachangia pia kutokuwa na wanafunzi wa kutosha katika masomo ya sayansi, aidha, upungufu huu utatupelekea kutotimiza ile ndoto ya Tanzania ya viwanda kwani dhana nzima ya viwanda inahusishwa na sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuendelea kutilia mkazo katika masomo ya sayansi na ikiwezekana kutoa motisha kwa walimu ambao watakwenda kusomea sayansi na wale watakaokuwa wanafundisha masomo hayo, aidha na kwa wanafunzi pia ili kuwafanya wapende masomo ya sayansi kwa upande wa wanafunzi na kwa upande wa walimu motisha hiyo itawafanya kufundisha kwa hamasa kubwa watoto wetu na hivyo kufika lengo la kuzalisha vijana wengi watakaomaliza michepuo ya sayansi na kuja kulisaidia Taifa letu kukuza uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ihakikishe inapeleka walimu wa kutosha hasa maeneo ya vijijini, kwani ndio kuna changamoto kubwa ya upungufu wa walimu na nyumba za kuishi. Aidha, tuna changamoto kubwa ya upungufu wa walimu wa nyumba za kuishi. Aidha, naishauri Serikali kuhakikisha inaongeza matundu ya vyoo katika shule zetu zote nchini na hasa shule za vijijini ndizo zinazokutana na changamoto kubwa za mapungufu hayo kwani hata muamko wa wazazi katika kujitolea na kuchangia kwa hiari masuala ya kujenga matundu ya vyoo, nyumba za walimu na madarasa imekuwa ni mgumu sana kulinganisha na shule za mijini, ambazo nyingi hazina changamoto hizi. Hivyo, ni vema katika bajeti hii hasa ikazingatia masuala muhimu katika kuboresha sekta nzima ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na malalamiko ya muda mrefu kuhusu ubora wa mifumo ya elimu yetu nchini, malalamiko hayo yanapaswa kuchukuliwa kama fursa na Serikali na si ya kuyabeza kwani wadau wa elimu wote ni Watanzania na wanataka maboresho ama mabadiliko yafanyike ili kuokoa sekta nzima ya elimu na mdororo unaoweza kuja kuleta shida hapo siku za mbeleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ikae na wadau wa elimu kuchukua mawazo yao na kusikiliza ushauri unaotolewa na sisi Wabunge na kuufanyia kazi bila kuwa na elimu bora yenye tija, hatuwezi kuwa nchi ya viwanda na tutasababisha watu wetu kuwa watumwa ndani ya nchi yao kwani watakuja wawekezaji kutoka nje na kukosa wataalam kutoka ndani na hivyo kuja na watalaam toka nje kuja kushika nafasi hizo na kuwafanya wazawa kuwa watumwa. Ili kuliepuka hilo Serikali haina budi sasa kuwekeza vya kutosha katika elimu ili kuwa na Taifa bora ni lazima sekta ya elimu iwe imara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakuwa tunajidanganya tukisahau sekta ya elimu na kuzipa kipaumbele sekta nyingine huku tukisema nchi imepiga hatua, ni wajibu wa Serikali kuzipa kipaumbele sekta zote lakini zile zinazobeba mustakabali wa nchi zikaangaliwa kwa upana wake, tukumbuke hakuna hatua nchi inapiga kama watu wake wakiwa wanapata elimu isiyokuwa bora na isiyoendana na viwango vya kimataifa.

Mheshimiwa Spika, jimboni kwangu tuna changamoto nyingi sana katika sekta ya elimu, mimi nikiwa kama mwakilishi wa wananchi na mdau mkubwa wa elimu nimejaribu kutatua baadhi ya changamoto hizo kwa gharama zangu nikishirikisha wadau mbalimbali ili tu wananchi wangu wapate elimu bora, nimeshawahi kutoa vitabu mbalimbali kwa elimu ya msingi na sekondari, kuchangia madawati, ujenzi wa ofisi za walimu, madarasa na matundu ya vyoo na nimekuwa nikifanya hivyo kila mara na pale inapobidi ili kupunguza changamoto hizo pasipo kuisubiria Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda Serikali inapokuja katika jitihada zake za kuleta maendeleo basi ikute sisi kama wadau tumeshaanza kushiriki ili Serikali nayo iweze kumalizia, lakini bado tuna changamoto nyingi ambazo sasa Serikali naiomba ije na majibu ili wananchi wajue zitatatuliwa kipindi gani? Tuna changamoto ya vyumba vya madarasa na kupelekea chumba kimoja kutumiwa na wanafunzi hadi 150 katika shule ya msingi Mtongani, japo changamoto hiyo ipo katika shule zote, lakini kwa shule hiyo tajwa hapo imeelemewa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, tuna changamoto ya samani za ndani katika ofisi za walimu zilizopo, hakuna furniture hivyo kuwafanya walimu wanapokuwa katika majukumu yao ya kila siku kuyafanya katika mazingira magumu sana, na tatizo hilo lipo kwa shule zote, na baadhi ya shule zina upungufu mkubwa wa ofisi za walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo tuna changamoto pia ya nyumba za walimu, walimu wetu Kibaha Vijijini hawana nyumba za kukaa na ikitokea ikawepo basi nyumba moja huwapasa kukaa walimu zaidi ya wawili, hali hiyo sio nzuri kwani huwarudisha nyuma walimu wetu kiutendaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto ya matundu ya vyoo, hali hii huwafanya walimu na wanafunzi kutumia sehemu moja jambo ambalo si utamaduni wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wanalalamika sana kuhusu stahiki zao ambazo ni za muda mrefu, hali hii ya madai haya huwarudisha nyuma kiutendaji walimu wa jimboni kwangu, tuna changamoto ya upungufu wa walimu mkubwa sana, walimu waliopo ni wachache na hawatoshelezi na kukidhi vigezo, naiomba Serikali kupitia Wizara ije na majibu ya changamoto hizo tajwa wakati wa majumuisho ya Bajeti ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kujua ina mkakata gani kutatua changamoto nilizokwisha zitaja hapo juu ili wananchi wa Kibaha Vijijini wapate elimu bora na walimu pia wawe katika mazingira mazuri na ifike mahali walimu wakisikia wanapelekwa Kibaha Vijijini basi wafurahie na isiwe kama ni adhabu kwani kutakuwa tayari na mazingira rafiki ya kufanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.