Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba ya bajeti ya Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara kwa kazi kubwa na nzuri ya kuboresha elimu kwa watoto wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono mapendekezo ya Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, ushauri na mapendekezo yazingatiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maombi ya kusaidiwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni shule ya sekondari Mgombezi ambayo ipo nje ya Mji wa Korogwe Mjini, ina vijiji sita na vitongoji kumi. Watoto wa kike wanatembea kilometa tano kwenda na kurudi, kwenye mashamba ya mkonge, usalama wa watoto hawa ni mdogo na mwendo ni mkubwa kiasi kwamba wanachoka kwa kutembea kabla ya kuanza masomo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule ya sekondari Chifu Kimweri iko nje ya mji, ina vijiji vinne, vitongoji saba watoto wanatembea umbali mrefu kiasi kwamba wanachoka kabla ya masomo. Naomba iangaliwe kupewa fedha za ujenzi wa mabweni ili watoto wa kike wabaki shuleni kwa ajili ya kuwanusuru na majanga yanayowasibu barabarani na nyumbani kukosa muda wa kujisomea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Korogwe Mjini tumetenga eneo la kujenga chuo cha ufundi Mgombezi, tunaiomba Serikali isaidie kuwaunga mkono wananchi ambao wameanza kwa nguvu zao wenyewe kama inavyosaidia kwenye vyumba vya madarasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kutoondoa masomo ya uraia na historia shule za msingi na sekondari na vyuo vya ualimu. Aidha, wakuu wa vyuo, walimu wa shule za msingi na sekondari wanaokaimu nao wapewe mafunzo ya uongozi (ADEM - Bagamoyo) kama zamani na kukaguliwa mara kwa mara kuinua elimu vyuoni na sekondari pia hasa Chuo cha Ualimu Korogwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.