Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Venance Methusalah Mwamoto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia. Nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kweli kwa kunifanya niwe mzima mpaka leo lakini niwashukuru sana Wananchi wa Kilolo ambao wamenirudisha baada ya miaka kumi kutoka hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Rais iko vizuri na jana wenzetu walipotoka nje, bahati nzuri mimi nilipata bahati ya kuwa wa kwanza kutoka lakini kikubwa kilichofanya watoke ni kwamba hawana sehemu ya kuchangia. Sasa kwenye ile hotuba kama hauna sehemu ya kuchangia itakuwa siyo rahisi ubaki humu ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili wenzetu wanataka kuonekana Live. Mimi nilikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, kuna watu walikuwa wanajua kuzungumza humu ndani mnawajua sitaki kuwataja na ilikuwa wakati anachanga unakuta vikundi vimeshajikusanya ukiuliza kuna nini wanakwambia leo jamaa anaongea na anataka kumchana live Waziri Mkuu, sasa nafasi hiyo haipo tena.
Kwa hiyo, wenyewe wanataka kuendelea kucheza live humu ndani lakini ukiangalia maendeleo kwenye maeneo yao hakuna, na walio wengi ninyi wenyewe mnahakika kabisa hawakurudi waliokuwa wanazungumza sana humu ndani. Wananchi wanataka maendeleo. Wanataka live kwenye maendeleo siyo live kwenye TV.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi kwa kweli kwa muda ule ambao umependekezwa ni muda ambao wananchi wengi kweli watakuwa wanaweza kuona kinachofanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye suala la maji. Wilaya ya Kilolo, Tarafa ya Mazombe - Ilula kuna tatizo kubwa sana. Mimi nina hakika mwaka 2000/2005 nilipokuwa Mbunge, tulipewa ahadi na Mheshimiwa wakati huo Rais Mkapa suala la maji, bahati nzuri haikuwezekana, wananchi walinihukumu wakanipa likizo, na mwenzangu aliyechukua nafasi yangu aliingia akapewa ahadi nzuri na Rais aliyekuwepo, naye inawezekana ni sababu hiyo hiyo amepewa likizo, sasa juzi alipifika Mheshimiwa Rais kuja kuomba kura tukamwambia sehemu moja nzuri anayotakiwa kwenda ni sehemu ya Ilula ambayo ina tatizo la maji. Aliahidi kwamba suala hilo analichukua, na ana hakika kabisa asilimia 100, akawaambia wananchi kwamba nirudishieni Mwamoto na nipeni kura, suala la maji limekwisha. Nitawaletea Waziri ambaye anajua matatizo ya maji.
Mheshimiwa Lwenge naomba uandike vizuri hiyo, kwa sababu ili uende kwenu kwenye Jimbo lako ni lazima upite Ilula. Huwezi kunywa maji, huwezi kupita Ilula. Uhakikishe maji yanapatikana na ni ahadi ya Mheshimiwa Rais. Sasa hivi ukienda pale ukimsalimia mtu wa Ilula, maana yake sisi huwa tunasalimiana kule kilugha kamwene, anakwambia maji, ukimwambia kamwene anakwambia maji, ukimwambia kitu chochote anakwambia maji, hapa kazi tu, maji. Sasa dawa yake ni kutoa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, na ukikaa Ilula ukitaka kupanga chumba unapanga vyumba viwili kama unaanza maisha, unapanga chumba kimoja kwa ajili ya madumu ya maji na chumba kimoja kwa ajili ya kulala wewe. Sasa mimi nawaomba, kwa sababu ni ahadi ya Rais na Mheshimia Lukuvi naomba unisaidie, mimi mdogo wako nipo nisiondoke tena unisaidie maji na maji mengine kwako kule tutakuletea.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ilula hakuna tatizo la maji, tatizo lake ni mgawanyo wa maji, maji yapo mengi, kuna mito mingi pale lakini unaifikishaje kwa wananchi ndiyo tatizo. Kwa hiyo, mimi naomba, Mheshimiwa Lwenge tuende pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la barabara. Kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, iko wazi kabisa kwamba kila Wilaya barabara itaunganishwa kwa lami mpaka Makao Makuu ya Mkoa, lakini pia na kufanya uwezekano mkubwa na kuunganishwa na Wilaya nyingine.
Wilaya ya Kilolo toka mwaka 2002 mpaka sasa katika kilomita 35, kilomita zilizojengwa kwa lami ni kilomita saba, sasa sielewi ni kwa nini. Kwa hiyo kwa kuwa Profesa Mbarawa nilishazungumza naye, tutaona jinsi ya kutusaidia, lakini ni pamoja na kutuunganisha ile barabara ya TANROAD inaishia Idete, tulishaipitisha kwenye mpango wa barabara ya TANROAD kwamba iishie sasa Muhanga ili tuunganike na watu wa Morogoro, kwamba itoke Kilolo - Dabaga - Idete - Itonya ifike mpaka Muhanga ili tuende mpaka Mbingu kule Kilombero, Morogoro tuweze kuunganisha nao ili tuweze kufungua uchumi wetu kwa sababu uchumi wa Kilolo unategemea sana Kilimo na ili wananchi wale wapate fedha inabidi wauze mazao yao yale lakini kama barabara zitakuwa ni shida watanyanyaswa, watauza mazao yao kwa bei ambayo haifai.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la pembejeo za kilimo. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo alifika Iringa na tukamwambia matatizo ya pembejeo. Lakini tatizo la Pembejeo Mheshimiwa Waziri wa Kilimo naona unanisikia, naomba hebu washikirishe Wakuu wa Wilaya kwenye suala hili la usambazaji wa pembejeo na ikiwezekana Wakuu wa Wilaya wasiwe Wenyeviti wa pembejeo kwa sababu wao ndiyo wanatakiwa wasimamie, kwa hiyo linapotokea tatizo hakuna wa kumuuliza! Mkurugenzi yupo mle, Mkuu wa Wilaya yupo mle, wao wasimamie tu mwenendo mzima wa pembejeo kwa sababu kuna ujanja mwingi sana kwenye pembejeo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi ndiyo wanapeleka mbegu Kilolo wakati sasa hivi ni wakati wa kupalilia, wanatakiwa wapeleke mbolea ya kukuzia, kwa hiyo kuna matatizo pale, tunaomba utusaide. Lakini pia na bei ya mbolea iko juu sana, tuangalie uwezekano wa kupunguza kama ni kodi, kama mambo mengine basi yapungue.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia suala la Mabaraza ya Kata. Mheshimiwa Waziri wa Sheria yupo, TAMISEMI yupo, Utawala Bora yupo, Wizara ya Mambo ya Ndani yupo. Mabaraza ya Kata kuna tatizo, tatizo ambalo lipo wanaoendesha hayo Mabaraza uwezo wao ni mdogo, hawapati mafunzo, lakini kazi ile ni kubwa sana na wamesaidia sana kutatua migogoro.
Kwa hiyo mimi nikuombeni tusaidiane kwenye hilo sambamba na madawati ya jinsia. Mheshimiwa Kitwanga, madawati ya jinsia yamesaidia sana kupunguza kero nyingi sana lakini matatizo ambalo lipo, yale Mabaraza ni vema ofisi zikawa kwa Mkuu wa Wilaya, kwa sababu watu walio wengi Mheshimiwa ukipigwa kibao na mke wako unaona aibu kwenda Polisi lakini ikiwa kwenye Baraza anahisi ni sehemu ya usuluhisho kwa hiyo inakuwa rahisi kwenda na kutoa elimu. Maana yake madawati ya jinsia siyo wanawake peke yake, hata wanaume. (Makofi)
Mimi naomba ikiwezekana tuma watu wako waende pale Kibondo wakaone lile Dawati linavyoendeshwa na kesi nyingi pale ni za wanaume kushtaki kwa kupigwa tena. Kwa hiyo unaona jinsi ambavyo elimu imefika kule. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni suala la ujenzi wa ofisi, Wilaya ya Kilolo toka mwaka 2002 tumekuwa Wilaya lakini Mheshimiwa Kitwanga huna hata jengo moja ambalo limejengwa. Huna Makao Makuu ya Polisi ya Wilaya, huna nyumba ya Polisi Wilaya ya Kilolo. Kwa hiyo mimi naomba, baada ya Bunge hili mimi tutakwenda pamoja na nitachangia na mafuta maana haukuwa mpango wako ili tuende ukaone hali jinsi ilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia na suala la hospitali hamna hospitali Wilaya ya Kilolo. Majengo yapo pale lakini mpaka leo hakuna hospitali ya Wilaya na kuna majengo ambayo wananchi wamejitolea wamejenga zahanati lakini hazijaisha, wamejenga vituo vya afya havijaisha, ukiwauliza wanakuambia bajeti tuliomba lakini tumeletewa bajeti finyu. Kwa hiyo nafikiri Mheshimiwa Kigwangalla tusimsumbue Mheshimiwa Waziri, tuende ukaone hali jinsi ilivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa muda bado ninao, kuna hili sula la uchangiaji wa elimu ambapo Mheshimiwa Rais amefuta...
Mheshimiwa Naibu Spika, basi naunga mkono hoja.