Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Buyungu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Buyungu, Wilaya ya Kakonko linazalisha mazao ya chakula na biashara. Mazao ya chakula huzalishwa kwa wingi kama mahindi, maharage, mihigo, ufuta, mpunga na kadhalika. Mazao haya huuzwa pia kama ya biashara ili kupata kipato. Wakulima wanaouza mazao nje ya nchi yaani Burudi wengine hupata misukosuko bila sababu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, nashauri wakulima hawa waruhusiwe kuuza mazao yao Burundi kwani bei ni nzuri. Aidha, zao kubwa la biashara ni tumbaku ambayo nayo inauzwa kwa deni/mkopo ambao unalipwa kwa tabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mazao kukatwa/kuharibiwa na wakimbizi. Kambi ya Wakimbizi Mtendeli-Kakonko imeharibu mazao/mashamba kwa kiasi kikubwa bila fidia yoyote. Serikali itoe fidia kwa wakulima waliopata madhara haya kwani wameharibiwa mazao ambayo yangewasaidia kwa chakula na kwenye pato la familia.
Mheshimiwa Naibu Spika, vocha za pembejeo Wilaya ya Kakonko kuna chembechembe za rushwa na udanganyifu wa kutosha. Mfano, mbolea na mbegu haziwafikii wananchi kwa wakati na wakati fulani wakulima wanasainishwa vocha bila kupewa pembejeo na hivyo kulipwa fedha kati ya shilingi 10,000 hadi 20,000 au 5,000 tu, hii ni hatari. Nashauri pembejeo zifike Wilaya ya Kakonko mwezi Agosti kila mwaka na ziletwe za kutosha kwa kila kijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo cha umwagiliaji Jimboni kimesusua kwani miundombinu imeharibika maji hayafiki mashambani. Nashauri suala hili nalo liangaliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya ufugaji katika Wilaya ya Kakonko si nzuri sana kwani hata wale wanaofuga ng‟ombe wanakabiliwa na wizi wa mara kwa mara na kwenda kuuzwa Burundi, hali hii inakatisha tamaa. Aidha, wafugaji wanaohitaji kuuza mifugo nchi jirani ya Burundi hupata misukosuko.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hali ya majosho siyo nzuri kwani hakuna josho hata moja wilaya nzima kwa hiyo mifugo inashambuliwa na wadudu ambao mwisho wake huleta magonjwa. Kuna uhaba pia wa dawa za mifugo na chanjo hali ambayo huongeza vifo vya mifugo kama ng‟ombe, mbuzi, kuku, kondoo na kadhalika. Vile vile kuna uhaba wa Maafisa Ugani Wilaya ya Kakonko wakati waliohitimu wakiwepo mitaani bila kupewa ajira. Hali hii husababisha wafugaji kufuga kienyeji mno na hivyo kutokuwepo na tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya uvuvi Wilayani Kakonko haijapewa kipaumbele. Sababu kubwa ni wananchi kukosa mwamko wa shughuli za uvuvi; wananchi kukosa utaalam wa uvuvi; wachache wanaojitokeza kutaka kufanya ufugaji wa samaki hukosa vifaranga vya kupanda kwenye mabawa na uchimbaji wa mabwawa ni mgumu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, maoni ya jumla (general comment) ni kama ifuatavyo:-
(i) Bajeti ya Wizara ni ndogo sana, majukumu mengi;
(ii) Serikali itafute ufumbuzi/utatuzi wa migogoro ya wafugaji na wakulima. Yatengwe maeneo ya kila mhusika. Aidha, elimu itolewe kwa wafugaji kupunguza mifugo yao ili iweze kupata maeneo ya kufugia;
(iii) Wafugaji washauriwe ili wasihamehame ili watoto wao wasome shule;
(iv) Bajeti ya mbolea mwaka huu iongezwe toka shilingi bilioni 78;
(v) Tafiti za kilimo zisaidie kuinua ubora wa kilimo, mifugo na uvuvi; na
vi) Ziwa Tanganyika kuna samaki wengi ambao hawajavuliwa kutokana na zana duni za uvuvi (Low quality fishing gears). Serikali inunue meli za uvuvi zinazovuna na kusindika samaki (fishprocessing).